< Zaburi 38 >
1 Zaburi ya Daudi. Maombi. Ee Bwana, usinikemee katika hasira yako, wala kuniadhibu katika ghadhabu yako.
Yahwe, usinikemee katika hasira yako; usiniadhibu katika ghadhabu yako.
2 Kwa kuwa mishale yako imenichoma, na mkono wako umenishukia.
Kwa kuwa mishale yako hunichoma, na mkono wako huniangusha chini.
3 Hakuna afya mwilini mwangu kwa sababu ya ghadhabu yako, mifupa yangu haina uzima kwa sababu ya dhambi zangu.
Mwili wangu wote unaumwa kwa sababu ya hasira yako; kwa sababu ya dhambi zangu mifupa yangu haina afya.
4 Maovu yangu yamenifunika kama mzigo usiochukulika.
Kwa maana maovu yangu yamenielemea; yamekuwa mzigo mzito kwangu.
5 Majeraha yangu yameoza na yananuka, kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu.
Vidonda vyangu vimeoza na vinanuka kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu.
6 Nimeinamishwa chini na kushushwa sana, mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.
Nimepindika na kuwa mnyonge kila siku; ninaenenda katika maombolezo siku zote.
7 Viuno vyangu vimejaa maumivu yaunguzayo, hakuna afya mwilini mwangu.
Kwa maana ndani yangu, ninaungua; hakuna afya katika mwili wangu.
8 Nimedhoofika na kupondwa kabisa, nasononeka kwa maumivu makuu ya moyoni.
Nimedhohofika na kulemewa sana; ninaugua kwa sababu ya dhiki yangu.
9 Ee Bwana, yote ninayoyaonea shauku yako wazi mbele zako, kutamani kwangu sana hakufichiki mbele zako.
Bwana, wewe unaielewa shauku ya ndani kabisa ya moyo wangu, na kuugua kwangu hakujifichika kwako.
10 Moyo wangu unapigapiga, nguvu zangu zimeniishia; hata macho yangu yametiwa giza.
Moyo wangu unapwita pwita, nguvu zangu zinaniisha, macho yangu yanafifia.
11 Rafiki na wenzangu wananikwepa kwa sababu ya majeraha yangu; majirani zangu wanakaa mbali nami.
Marafiki na ndugu zangu wamenitenga kwa sababu ya hali; majirani zangu hukaa mbali nami.
12 Wale wanaotafuta uhai wangu wanatega mitego yao, wale ambao wangetaka kunidhuru huongea juu ya maangamizi yangu; hufanya shauri la hila mchana kutwa.
Wale wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego kwa ajili yangu. Wao ambao hutafuta kunidhuru huongea maneno ya uharibifu na husema maneno ya uongo siku nzima.
13 Mimi ni kama mtu kiziwi, asiyeweza kusikia, ni kama bubu, asiyeweza kufungua kinywa chake,
Lakini, niko kama mtu kiziwi na sisikii lolote; niko kama mtu bubu ambaye hasemi lolote.
14 nimekuwa kama mtu asiyesikia, ambaye kinywa chake hakiwezi kutoa jibu.
Niko kama mtu asiye sikia na mbaye hawezi kujibu.
15 Ee Bwana, ninakungojea wewe, Ee Bwana Mungu wangu, utajibu.
Hakika ninakungoja wewe, Yahwe; wewe utanijibu, Bwana Mungu wangu.
16 Kwa kuwa nilisema, “Usiwaache wafurahie, wala wasijitukuze juu yangu mguu wangu unapoteleza.”
Ninasema hivi ili kwamba maadui zangu wasije wakafurahia juu yangu. Ikiwa mguu wangu utateleza, watanifanyia mambo mabaya.
17 Kwa maana ninakaribia kuanguka, na maumivu yangu yananiandama siku zote.
Kwa kuwa niko karibu mashakani, na niko katika maumivu ya mara kwa mara.
18 Naungama uovu wangu, ninataabishwa na dhambi yangu.
Ninatubu makosa yangu; ninahuzunika kwa dhambi zangu.
19 Wengi ni wale ambao ni adui zangu hodari, wale wanaonichukia bila sababu ni wengi.
Lakini maadui zangu ni wengi; wale wanichukiao ni wengi.
20 Wanaolipa maovu kwa wema wangu hunisingizia ninapofuata lililo jema.
Wao wananilipa mabaya kwa mema; wanavurumiza shutuma kwangu ingawa nimefuata lililo jema.
21 Ee Bwana, usiniache, usiwe mbali nami, Ee Mungu wangu.
Usinitelekeze, Yahwe, Mungu wangu, usikae mbali nami.
22 Ee Bwana Mwokozi wangu, uje upesi kunisaidia.
Njoo haraka unisaidie, Bwana, wokovu wangu.