< Zaburi 37 >

1 Zaburi ya Daudi. Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu, wala usiwaonee wivu watendao mabaya,
Usikereshwe na wafanyao maovu; usiwaonee wivu wale watendao yasiyo haki.
2 kwa maana kama majani watanyauka mara, kama mimea ya kijani watakufa mara.
Kwa kuwa muda mfupi watakauka kama nyasi na kukauka kama vile mimea ya kijani ikaukavyo wakati wa kiangazi.
3 Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema; Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.
Uwamini Mungu na kufanya yaliyo mema; uishi katika nchi na uongezeke katika imani.
4 Jifurahishe katika Bwana naye atakupa haja za moyo wako.
Kisha ufurahi mwenyewe katika Yahwe, naye atakupa matamanio ya moyo wako.
5 Mkabidhi Bwana njia yako, mtumaini yeye, naye atatenda hili:
Umkabidhi njia zako Yahwe; uamini katika yeye, naye atatenda kwa niaba yako.
6 Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko, na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri.
Yeye ataidhihilisha haki yako kama mchana na usafi wako kama mwangaza wa mchana.
7 Tulia mbele za Bwana na umngojee kwa uvumilivu; usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao, wanapotekeleza mipango yao miovu.
Uwe kumya mbele za Yahwe na umsubiri yeye kwa uvumilivu. Usikasirike ikiwa kuna mtu anafanikiwa kwa kile afanyacho, au afanyapo njama za uovu.
8 Epuka hasira na uache ghadhabu, usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu.
Usikasilile na kugadhabika. Usiogope. Hii huleta matatizo tu.
9 Kwa maana waovu watakatiliwa mbali, bali wale wanaomtumaini Bwana watairithi nchi.
Watendao maovu watafutiliwa mbali, bali wale wamngojao Yahwe watairithi nchi.
10 Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana, ingawa utawatafuta, hawataonekana.
Katika muda mfupi mtu mwovu atatoweka; wewe utatazama mahali pake, wala hautamuona.
11 Bali wanyenyekevu watairithi nchi na wafurahie amani tele.
Lakini wapole watairithi nchi nao watafurahia katika mafanikio makubwa.
12 Waovu hula njama dhidi ya wenye haki na kuwasagia meno,
Mtu mwovu hupanga njama kinyume na mwenye haki na kumsagia meno.
13 bali Bwana huwacheka waovu, kwa sababu anajua siku yao inakuja.
Bwana humcheka, kwa maana anaona siku yake inakuja.
14 Waovu huchomoa upanga na kupinda upinde, ili wawaangushe maskini na wahitaji, kuwachinja wale ambao njia zao ni nyofu.
Waovu wametoa nje panga zao na wametayarisha pinde zao ili kuwaangamiza wanyonge na wahitaji, na kuwaua wenye haki.
15 Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe, na pinde zao zitavunjwa.
Panga zao zitawaua wenyewe, na pinde zao zitavunjika.
16 Bora kidogo walicho nacho wenye haki kuliko wingi wa mali wa waovu wengi;
Ni bora kuwa mwenye haki maskini kuliko tajiri mwenye mali nyingi.
17 kwa maana nguvu za waovu zitavunjwa, lakini Bwana humtegemeza mwenye haki.
Kwa maana mikono ya watu waovu itavunjika, bali Yahwe huwasaidia watu wenye haki.
18 Bwana anazifahamu siku za wanyofu, na urithi wao utadumu milele.
Yahwe huwalinda watu wasio na lawama siku hadi siku, na urithi wao utakuwa wa milele.
19 Siku za maafa hawatanyauka, siku za njaa watafurahia wingi wa vitu.
Hawata aibika siku mbaya zijapo. Wakati wa njaa ufikapo wao watakuwa na chakula cha kutosha.
20 Lakini waovu wataangamia: Adui za Bwana watakuwa kama uzuri wa mashamba, watatoweka, watatoweka kama moshi.
Bali waovu wataangamia. Maadui wa Yahwe watakuwa kama vile utukufu wa malisho; watamalizwa na kupotezwa katika moshi.
21 Waovu hukopa na hawalipi, bali wenye haki hutoa kwa ukarimu.
Mtu mwovu hukopa lakini halipi, bali mtu mwenye haki ni mkarimu na hutoa.
22 Wale wanaobarikiwa na Bwana watairithi nchi, bali wale anaowalaani watakatiliwa mbali.
Wale walio barikiwa na Mungu watairithi nchi; wale aliowalaani watafutiliwa mbali.
23 Kama Bwana akipendezwa na njia ya mtu, yeye huimarisha hatua zake,
Hatua za mwanadamu zinaimarishwa na Yahwe, mtu ambaye njia zake zinakubalika machoni pa Mungu.
24 ajapojikwaa, hataanguka, kwa maana Bwana humtegemeza kwa mkono wake.
Ajapojikwaa, hataanguka chini, kwa kuwa Yahwe anamshikilia kwa mkono wake.
25 Nilikuwa kijana na sasa ni mzee, lakini sijaona kamwe wenye haki wameachwa au watoto wao wakiombaomba chakula.
Nilikuwa kijana na sasa ni mzee; sijawahi kumuona mtu mwenye haki ametelekezwa wala watoto wake kuombaomba mkate.
26 Wakati wote ni wakarimu na hukopesha bila masharti. Watoto wao watabarikiwa.
Wakati wote yeye ni mkarimu na hukopesha, nao watoto wake hufanyika baraka.
27 Acha ubaya na utende wema, nawe utaishi katika nchi milele.
Acha uovu na ufanye yaliyo mema; ndipo utakapokuwa salama milele.
28 Kwa kuwa Bwana huwapenda wenye haki naye hatawaacha waaminifu wake. Watalindwa milele, lakini uzao wa waovu utakatiliwa mbali.
Kwa maana Yahwe hupenda haki naye hawaachi wafuasi waaminifu. Wao hutunzwa milele, lakini uzao wa waovu utafutiliwa mabli.
29 Wenye haki watairithi nchi, na kuishi humo milele.
Wenye haki watairithi nchi na kuaa huko milele.
30 Kinywa cha mwenye haki hutamka hekima, nao ulimi wake huzungumza lililo haki.
Mdomo wa mwenye haki huongea hekima na huongeza haki.
31 Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake; nyayo zake hazitelezi.
Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake; miguu yake haitelezi.
32 Watu waovu huvizia wenye haki, wakitafuta kuwaua;
Mtu mwovu humvizia mwenye haki na kutafuta kumuua.
33 lakini Bwana hatawaacha mikononi mwao wala hatawaacha wahukumiwe kuwa wakosa wanaposhtakiwa.
Yahwe hatamuacha yeye kwenye mkono wa mtu mwovu wala kumlaumu atakapohukumiwa.
34 Mngojee Bwana, na uishike njia yake. Naye atakutukuza uirithi nchi, waovu watakapokatiliwa mbali, utaliona hilo.
Umngoje Yahwe na uishike njia yake, naye atakuinua uimiliki nchi. Atakapo waondosha waovu wewe utaona.
35 Nimemwona mtu mwovu na mkatili akistawi kama mwerezi wa Lebanoni,
Nimewaona waovu na mtu wa kutisha akienea kama mti wa kijani katika udongo wa asili.
36 lakini alitoweka mara na hakuonekana, ingawa nilimtafuta, hakupatikana.
Lakini nilipopita tana mara nyingine, hakuwepo pale. nilimtafuta, lakini sikumpata.
37 Watafakari watu wasio na hatia, wachunguze watu wakamilifu, kuna mafanikio kwa mtu apendaye amani.
Uwachunguze watu waadilifu, na uwatambue wenye haki; kuna hatima nzuri kwa ajili ya mtu wa amani.
38 Lakini watenda dhambi wote wataangamizwa, mafanikio yao yatakatiliwa mbali.
Mwenye dhambi wataharibiwa kabisa; hatima ya mtu mwovu ni kuondoshwa.
39 Wokovu wa wenye haki hutoka kwa Bwana, yeye ni ngome yao wakati wa shida.
Wokovu wa haki unatoka kwa Yahwe; yeye huwalinda wao nyakati za shida.
40 Bwana huwasaidia na kuwaokoa, huwaokoa kutoka kwa waovu na kuwahifadhi, kwa maana wanamkimbilia.
Yahwe huwasaidia na kuwaokoa. Yeye huwaokoa dhidi ya watu waovu na kuwanusuru wao kwa sababu wao wamemkimbilia yeye kwa ajili ya usalama.

< Zaburi 37 >