< Zaburi 33 >
1 Mwimbieni Bwana kwa furaha, enyi wenye haki; kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
Furahini katika Yahwe, ninyi wenye haki; kusifu kwa wenye haki kwa faa sana.
2 Msifuni Bwana kwa kinubi, mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi.
Mshukuruni Bwana kwa kinubi; mwimbieni sifa kwa kinubi chenye nyuzi kumi.
3 Mwimbieni wimbo mpya; pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe.
Mwimbieni yeye wimbo mpaya; pigeni kwa ustadi na muimbe kwa furaha.
4 Maana neno la Bwana ni haki na kweli, ni mwaminifu kwa yote atendayo.
Kwa kuwa maneno ya Mungu ni ya hakika, na kila afanyacho ni haki.
5 Bwana hupenda uadilifu na haki; dunia imejaa upendo wake usiokoma.
Yeye hupenda haki na kutenda kwa haki. Dunia imejaa uaminifu wa agano la Yahwe.
6 Kwa neno la Bwana mbingu ziliumbwa, jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake.
Kwa neno la Yahwe mbingu ziliumbwa, na nyota zote ziliumbwa kwa pumzi ya mdomo wake.
7 Ameyakusanya maji ya bahari kama kwenye chungu; vilindi vya bahari ameviweka katika ghala.
Yeye huyakusanya maji ya baharini kama rundo; naye huiweka bahari katika ghala.
8 Dunia yote na imwogope Bwana, watu wote wa dunia wamche.
Basi ulimwengu wote umwogope Yahwe; wenyeji wote wa ulimwengu wamuhofu yeye.
9 Kwa maana Mungu alisema, na ikawa, aliamuru na ikasimama imara.
Kwa maana yeye alisema, na ikafanyika; aliamuru, na ikasimama mahali pake.
10 Bwana huzuia mipango ya mataifa, hupinga makusudi ya mataifa.
Yahwe huvunja muungano wa mataifa; naye huishinda mipango ya wanadamu.
11 Lakini mipango ya Bwana inasimama imara milele, makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote.
Mipango ya Yahwe husimama milele, mipango ya moyo wake ni kwa ajili ya vizazi vyote.
12 Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, watu ambao aliwachagua kuwa urithi wake.
Limebarikiwa taifa ambalo Mungu wao ni Yahwe, watu ambao yeye amewachagua kama warithi wake.
13 Kutoka mbinguni Bwana hutazama chini na kuwaona wanadamu wote;
Yahwe anatazama kutoka mbinguni; yeye huona watu wote.
14 kutoka maskani mwake huwaangalia wote wakaao duniani:
Kutokea mahali ambapo yeye anaishi, huwatazama wote waishio juu ya nchi.
15 yeye ambaye huumba mioyo yao wote, ambaye huangalia kila kitu wanachokitenda.
Yeye anaye iumba mioyo yao na kuyaona matendo yao yote.
16 Hakuna mfalme aokokaye kwa ukubwa wa jeshi lake; hakuna shujaa aokokaye kwa wingi wa nguvu zake.
Hakuna mfalme anayeokolewa na jeshi kubwa; shujaa haokolewi na nguvu zake nyingi.
17 Farasi ni tumaini la bure kwa wokovu, licha ya nguvu zake nyingi, hawezi kuokoa.
Farasi sio salama kwa ajili ya ushindi; ijapokuwa nguvu zake ni nyingi, hawezi kuokoa.
18 Lakini macho ya Bwana yako kwa wale wamchao, kwa wale tumaini lao liko katika upendo wake usio na kikomo,
Tazama, macho ya Yahwe yako kwa wale wanao mhofu yeye, wale wanao litumainia agano lake takatifu
19 ili awaokoe na mauti, na kuwahifadhi wakati wa njaa.
kuwaokoa maisha yao na mauti na kuwaweka hai wakati wa jaa.
20 Sisi tunamngojea Bwana kwa matumaini, yeye ni msaada wetu na ngao yetu.
Sisi tunamngoja Yahwe, yeye ni msaada wetu na ngao yetu.
21 Mioyo yetu humshangilia, kwa maana tunalitumainia jina lake takatifu.
Mioyo yetu hufurahia ndani yake, kwa kuwa tunaamini katika jina lake takatifu.
22 Upendo wako usio na mwisho ukae juu yetu, Ee Bwana, tunapoliweka tumaini letu kwako.
Yahwe, agano lako takatifu, liwe pamoja nasi tuwekapo tumaini letu katika wewe.