< Zaburi 32 >

1 Zaburi ya Daudi. Funzo. Heri mtu yule ambaye amesamehewa makosa yake, ambaye dhambi zake zimefunikwa.
Zaburi ya Daudi. Zaburi. Amebarikiwa mtu yule aliyesamehewa makosa yake, ambaye dhambi zake zimesitiriwa.
2 Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi, na ambaye rohoni mwake hamna udanganyifu.
Amebarikiwa mtu yule ambaye Yahwe hamuhesabii hatia na ambaye rohoni mwake hamna udanganyifu.
3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.
Nilipokaa kimya, mifupa yangu ilidhohofika huku nikiugua muda wote.
4 Usiku na mchana mkono wako ulinilemea, nguvu zangu zilinyonywa kama vile katika joto la kiangazi.
Mchana na usiku mkono wako ulinielemea. nguvu zangu zilikauka wakati wa kiangazi. (Selah)
5 Kisha nilikujulisha dhambi yangu wala sikuficha uovu wangu. Nilisema, “Nitaungama makosa yangu kwa Bwana.” Ndipo uliponisamehe hatia ya dhambi yangu.
Ndipo nilipotambua makosa yangu kwako, nami sifichi tena uovu wangu. Nilisema, “Nitakiri makosa yangu kwa Yahwe,” nawe ulinisamehe hatia ya dhambi zangu. (Selah)
6 Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe wakati unapopatikana, hakika maji makuu yatakapofurika hayatamfikia yeye.
Kwa sababu ya haya, wale wote ambao ni wa kimungu wanapaswa kukuomba wakati wa shida kubwa. Nayo mafuriko yajapo, hayatawapata watu hao.
7 Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha, utaniepusha na taabu na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.
Wewe u mahali pangu pa kujifichia, nawe utanilinda matatizoni. Wewe utanizunguka pamoja na nyimbo zaushindi. (Selah)
8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; nitakushauri na kukuangalia.
Nitakuelekeza na kukufundisha katika njia upasayo kuiendea. Nitakuelekeza huku macho yangu yakikutazama.
9 Usiwe kama farasi au nyumbu wasio na akili, ambao ni lazima waongozwe kwa lijamu na hatamu la sivyo hawatakukaribia.
Msiwe kama farasi au kama nyumbu, ambao hawana uelewa; ni kwa hatamu na lijamu tu unaweza kuwapeleka popote utakapo wao waende.
10 Mtu mwovu ana taabu nyingi, bali upendo usio na kikomo wa Bwana unamzunguka mtu anayemtumaini.
Waovu wanahuzuni nyingi, bali uaminifu wa agano la Yahwe utamzunguka yule anaye mwamini yeye.
11 Shangilieni katika Bwana na mfurahi, enyi wenye haki! Imbeni, nyote mlio wanyofu wa moyo!
Furahini katika Yahwe, na mshangilie, ninyi wenye haki; pigeni kelele za shangwe, ninyi nyote wenye haki mioyoni mwenu.

< Zaburi 32 >