< Zaburi 3 >
1 Zaburi ya Daudi. Alipomkimbia mwanawe Absalomu. Ee Bwana, tazama adui zangu walivyo wengi! Ni wengi kiasi gani wanaoinuka dhidi yangu!
Yahewh, maadui zangu wako wangapi! Ni wengi wamekuja kinyume na mimi.
2 Wengi wanasema juu yangu, “Mungu hatamwokoa.”
Ni wengi wanaonisema, “Hakuna msaada wowote kutoka kwa Mungu kwa ajili yake.” (Selah)
3 Lakini wewe, Ee Bwana, ni ngao pande zote; umeniwekea utukufu na kuinua kichwa changu.
Bali wewe, Yahweh, u ngao yangu pande zote, utukufu wangu, na uniinuaye kichwa changu.
4 Ninamlilia Bwana kwa sauti kuu, naye ananijibu kutoka mlima wake mtakatifu.
Nampazia Yahweh sauti yangu, na yeye ananijibu kutoka katika mlima wake mtakatifu.
5 Ninajilaza na kupata usingizi; naamka tena, kwa maana Bwana hunitegemeza.
Nilijilaza chini na kusinzia; na niliamka, kwa kuwa Yahweh alinilinda.
6 Sitaogopa makumi elfu ya adui, wanaojipanga dhidi yangu kila upande.
Sitaogopa kusanyiko la watu ambao wamejipanga kinyume na mimi pande zote.
7 Ee Bwana, amka! Niokoe, Ee Mungu wangu! Wapige adui zangu wote kwenye taya, vunja meno ya waovu.
Inuka, Yahweh! Uniokoe, Mungu wangu! Kwa kuwa utawapiga maadui zangu wote kwenye taya zao; utayavunja meno ya waovu.
8 Kwa maana wokovu watoka kwa Bwana. Baraka yako na iwe juu ya watu wako.
Wokovu unatoka kwa Yahweh. Baraka zako ziwe juu ya watu wako.