< Zaburi 22 >
1 Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Kulungu wa Alfajiri.” Zaburi ya Daudi. Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa? Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu?
2 Ee Mungu wangu, ninalia mchana, lakini hunijibu, hata usiku, sinyamazi.
3 Hata hivyo umesimikwa katika kiti cha enzi kama Uliye Mtakatifu; wewe ni sifa ya Israeli.
4 Kwako wewe baba zetu waliweka tumaini lao, walikutumaini nawe ukawaokoa.
5 Walikulilia wewe na ukawaokoa, walikutegemea wewe nao hawakuaibika.
6 Mimi ni mnyoo wala si mwanadamu, wanaume wamenibeza, na watu wamenidharau.
7 Wote wanionao hunidhihaki, hunivurumishia matusi, wakitikisa vichwa vyao:
8 Husema, “Anamtegemea Bwana, basi Bwana na amwokoe. Amkomboe basi, kwa maana anapendezwa naye.”
9 Hata hivyo ulinitoa tumboni, ukanifanya nikutegemee, hata nilipokuwa ninanyonya matiti ya mama yangu.
10 Nimekabidhiwa kwako tangu kuzaliwa, toka tumboni mwa mama yangu umekuwa Mungu wangu.
11 Usiwe mbali nami, kwa maana shida iko karibu na hakuna wa kunisaidia.
12 Mafahali wengi wamenizunguka, mafahali wa Bashani wenye nguvu wamenizingira.
13 Simba wangurumao wanaorarua mawindo yao hupanua vinywa vyao dhidi yangu.
14 Nimemiminwa kama maji, mifupa yangu yote imetoka katika viungo vyake. Moyo wangu umegeuka kuwa nta, umeyeyuka ndani yangu.
15 Nguvu zangu zimekauka kama kigae, ulimi wangu umegandamana na kaakaa la kinywa changu, kwa sababu umenilaza katika mavumbi ya kifo.
16 Mbwa wamenizunguka, kundi la watu waovu limenizingira, wametoboa mikono yangu na miguu yangu.
17 Naweza kuhesabu mifupa yangu yote, watu wananikodolea macho na kunisimanga.
18 Wanagawana nguo zangu wao kwa wao, na vazi langu wanalipigia kura.
19 Lakini wewe, Ee Bwana, usiwe mbali. Ee Nguvu yangu, uje haraka unisaidie.
20 Okoa maisha yangu na upanga, uhai wangu wa thamani kutoka nguvu za mbwa.
21 Niokoe kutoka kinywani mwa simba, niokoe kutoka pembe za mafahali mwitu.
22 Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu, katika kusanyiko nitakusifu wewe.
23 Ninyi ambao mnamcha Bwana, msifuni! Ninyi nyote wazao wote wa Yakobo, mheshimuni yeye! Mcheni yeye, ninyi wazao wote wa Israeli!
24 Kwa maana hakupuuza wala kudharau mateso ya aliyeonewa; hakumficha uso wake bali alisikiliza kilio chake ili amsaidie.
25 Kwako wewe hutoka kiini cha sifa zangu katika kusanyiko kubwa, nitatimiza nadhiri zangu mbele ya wale wakuchao wewe.
26 Maskini watakula na kushiba, wale wamtafutao Bwana watamsifu: mioyo yenu na iishi milele!
27 Miisho yote ya dunia itakumbuka na kumgeukia Bwana, nazo jamaa zote za mataifa watasujudu mbele zake,
28 kwa maana ufalme ni wa Bwana naye hutawala juu ya mataifa.
29 Matajiri wote wa dunia watasherehekea na kuabudu. Wote waendao mavumbini watapiga magoti mbele yake, wote ambao hawawezi kudumisha uhai wao.
30 Wazao wa baadaye watamtumikia yeye; vizazi vijavyo vitajulishwa habari za Bwana.
31 Watatangaza haki yake kwa watu ambao hawajazaliwa bado, kwa maana yeye ametenda hili.