< Zaburi 148 >

1 Msifuni Bwana. Msifuni Bwana kutoka mbinguni, msifuni juu vileleni.
Msifuni Yahwe. Msifuni Yahwe, ninyi mlio katika mbingu; msifuni yeye, ninyi mlio juu.
2 Msifuni, enyi malaika wake wote, msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni.
Msifuni yeye, enyi malaika wake wote; msifuni yeye, majeshi ya malaika wake wote.
3 Msifuni yeye, enyi jua na mwezi, msifuni yeye, enyi nyota zote zingʼaazo.
Msifuni yeye, enyi jua na mwezi; msifuni yeye, nyota zote zing'aazo.
4 Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana, na ninyi maji juu ya anga.
Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu zaidi na maji yaliyo juu ya anga.
5 Vilisifu jina la Bwana kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa.
Na vilisifu jina la Yahwe, maana aliamuru, navyo vikaumbwa.
6 Aliviweka mahali pake milele na milele, alitoa amri ambayo haibadiliki milele.
Pia ameviimrisha milele na milele; naye alitoa amri ambayo haitabadilika.
7 Mtukuzeni Bwana kutoka duniani, ninyi viumbe vikubwa vya baharini na vilindi vyote vya bahari,
Msifuni yeye kutoka nchi, ninyi viumbe wa baharini na viumbe vyote katika kina cha bahari,
8 umeme wa radi na mvua ya mawe, theluji na mawingu, pepo za dhoruba zinazofanya amri zake,
moto na mvua ya mawe, theluji na mawingu, upepo wa dhoruba ukitimiza neno lake.
9 ninyi milima na vilima vyote, miti ya matunda na mierezi yote,
Msifuni yeye, enyi milima na vilima, miti ya matunda na mierezi yote,
10 wanyama wa mwituni na mifugo yote, viumbe vidogo na ndege warukao,
wanyama pori na wanyama wafugwao, viumbe vitambaavyo na ndege.
11 wafalme wa dunia na mataifa yote, ninyi wakuu na watawala wote wa dunia,
Msifuni Yahwe, wafalme wa nchi na mataifa yote, wakuu na watawala wote wa nchi,
12 wanaume vijana na wanawali, wazee na watoto.
wote vijana wa kiume na vijana wa kike, wazee na watoto.
13 Wote na walisifu jina la Bwana, kwa maana jina lake pekee limetukuka, utukufu wake uko juu ya nchi na mbingu.
Na walisifu jina la Yahwe, kwa kuwa jina lake pekee limetukuka na utukufu wake umeongezwa juu ya nchi na mbingu.
14 Amewainulia watu wake pembe, sifa ya watakatifu wake wote, ya Israeli, watu walio karibu na moyo wake. Msifuni Bwana.
Naye ameyainua mapembe ya watu wake kwa ajili ya sifa kutoka kwa waaminifu wake wote, Waisraeli, watu wa karibu naye. Msifuni Yahwe.

< Zaburi 148 >