< Zaburi 144 >
1 Zaburi ya Daudi. Sifa ni kwa Bwana Mwamba wangu, aifundishaye mikono yangu vita, na vidole vyangu kupigana.
2 Yeye ni Mungu wangu wa upendo na boma langu, ngome yangu na mwokozi wangu, ngao yangu ninayemkimbilia, ambaye huwatiisha mataifa chini yangu.
3 Ee Bwana, mwanadamu ni nini hata umjali, Binadamu ni nini hata umfikirie?
4 Mwanadamu ni kama pumzi, siku zake ni kama kivuli kinachopita.
5 Ee Bwana, pasua mbingu zako, ushuke, gusa milima ili itoe moshi.
6 Peleka umeme uwatawanye adui, lenga mishale yako uwashinde.
7 Nyoosha mkono wako kutoka juu, nikomboe na kuniokoa kutoka maji makuu, kutoka mikononi mwa wageni
8 ambao vinywa vyao vimejaa uongo, na mikono yao ya kuume ni midanganyifu.
9 Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, kwa zeze yenye nyuzi kumi nitakuimbia,
10 kwa Yule awapaye wafalme ushindi, ambaye humwokoa Daudi, mtumishi wake kutokana na upanga hatari.
11 Nikomboe na uniokoe kutoka mikononi mwa wageni ambao vinywa vyao vimejaa uongo, na mikono yao ya kuume ni midanganyifu.
12 Kisha wana wetu wakati wa ujana wao watakuwa kama mimea iliyotunzwa vizuri, binti zetu watakuwa kama nguzo zilizoviringwa kurembesha jumba la kifalme.
13 Ghala zetu zitajazwa aina zote za mahitaji. Kondoo zetu watazaa kwa maelfu, kwa makumi ya maelfu katika mashamba yetu;
14 maksai wetu watakokota mizigo mizito. Hakutakuwa na kubomoka kuta, hakuna kuchukuliwa mateka, wala kilio cha taabu katika barabara zetu.
15 Heri watu ambao hili ni kweli; heri wale ambao Bwana ni Mungu wao.