< Zaburi 143 >

1 Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, sikia sala yangu, sikiliza kilio changu unihurumie; katika uaminifu na haki yako njoo unisaidie.
Ee Yahwe, usikie maombi yangu; sikia kuomba kwangu. Kwa sababu ya uaminifu wa agano lako na haki yako, unijibu!
2 Usimhukumu mtumishi wako, kwa kuwa hakuna mtu anayeishi aliye mwenye haki mbele zako.
Usimuhukumu mtumishi wako, kwa kuwa machoni pako hamna aliye haki.
3 Adui hunifuatilia, hunipondaponda chini; hunifanya niishi gizani kama wale waliokufa zamani.
Adui ameifuatia nafsi yangu; amenisukuma hadi chini; amenifanya niishi gizani kama wale ambao wamekwisha kufa siku nyingi zilizopita.
4 Kwa hiyo roho yangu inazimia ndani yangu, moyo wangu ndani yangu unakata tamaa.
Na roho yangu inazidiwa ndani yangu; moyo wangu unakata tamaa.
5 Nakumbuka siku za zamani; natafakari juu ya kazi zako zote, naangalia juu ya kazi ambazo mikono yako imezifanya.
Nakumbuka siku za zamani zilizopita; nayatafakari matendo yako yote; nawaza juu ya utimilifu wako.
6 Nanyoosha mikono yangu kwako, nafsi yangu inakuonea kiu kama ardhi kame.
Nakunyoshea mikono yangu katika maombi; nafsi yangu inakuonea kiu katika nchi kavu. (Selah)
7 Ee Bwana, unijibu haraka, roho yangu inazimia. Usinifiche uso wako, ama sivyo nitafanana na wale washukao shimoni.
Unijibu upesi, Yahwe, kwa sababu roho yangu inazimia. Usinifiche uso wako, vinginevyo nitakuwa kama wale waendao chini shimoni.
8 Asubuhi uniletee neno la upendo wako usiokoma, kwa kuwa nimeweka tumaini langu kwako. Nionyeshe njia nitakayoiendea, kwa kuwa kwako nainua nafsi yangu.
Unifanye kusikia uaminifu wa agano lako wakati wa asubuhi, maana ninakuamini wewe. Unionyeshe njia niipasayo kutembea kwayo, kwa maana nakuinulia wewe nafsi yangu.
9 Ee Bwana, uniokoe na adui zangu, kwa kuwa nimejificha kwako.
Uniokoe dhidi ya adui zangu, Yahwe; nakimbilia kwako ili nijifiche.
10 Nifundishe kufanya mapenzi yako, kwa maana wewe ndiwe Mungu wangu, Roho wako mwema na aniongoze katika nchi tambarare.
Unifundishe kufanya mapenzi yako, maana wewe ni Mungu wangu. Roho wako mwema na aniongoze mimi katika nchi ya unyoofu.
11 Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako, hifadhi maisha yangu, kwa haki yako nitoe katika taabu.
Ee Yahwe, kwa ajili ya jina lako, unihifadhi hai; katika haki yako uitoe nafsi yangu taabuni.
12 Kwa upendo wako usiokoma, nyamazisha adui zangu; waangamize watesi wangu wote, kwa kuwa mimi ni mtumishi wako.
Katika uaminifu wa agano lako uwaondoshe maadui zangu na uwaangamize maadui wa uhai wangu, maana mimi ni mtumishi wako.

< Zaburi 143 >