< Zaburi 141 >
1 Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, ninakuita wewe, uje kwangu hima. Sikia sauti yangu ninapokuita.
Ee Yahwe, ninakulilia wewe; uje upesi kwangu. Unisikilize nikuitapo.
2 Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba; kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni.
Maombi yangu na yawe kama uvumba mbele zako; mikono yangu iliyoinuliwa na iwe kama dhabihu ya jioni.
3 Ee Bwana, weka mlinzi kinywani mwangu, weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.
Ee Yahwe, uweke mlinzi kinywani mwangu; mngojezi malangoni pa midomo yangu.
4 Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya, nisije nikashiriki katika matendo maovu pamoja na watu watendao mabaya, wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.
Usiruhusu tamaa ya moyo wangu kutamani uovu wowote wala kushiriki katika matendo ya dhambi na watu waishio maovuni. Nisile vyakula vyao vya anasa.
5 Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma; na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu. Kichwa changu hakitalikataa. Hata hivyo, maombi yangu daima ni kinyume cha watenda mabaya,
Mwenye haki na anipige; nao utakuwa ni wema kwangu. Anirudi; itakuwa kama mafuta kichwani pangu; kichwa changu na kisikatae kupokea. Lakini maombi yangu siku zote yatakuwa dhidi ya matendo yao mauvu.
6 watawala wao watatupwa chini kutoka kwenye majabali, waovu watajifunza kwamba maneno yangu yalikuwa kweli.
Viongozi wao watatupwa chini toka juu mlimani; watayasikia maneno yangu kuwa ni matamu.
7 Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi, ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.” (Sheol )
Watalazimika kusema, “Kama vile jembe moja livunjapo ardhi, hivyo mifupa yetu imesambaratishwa kinywani pa kuzimu.” (Sheol )
8 Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mwenyezi, ndani yako nimekimbilia, usiniache nife.
Hakika macho yangu yanakutazama wewe, Yahwe, Bwana; katika wewe napata kimbilio; usiiache nafsi yangu.
9 Niepushe na mitego waliyonitegea, kutokana na mitego iliyotegwa na watenda mabaya.
Unilinde dhidi ya mitego waliyoiweka kwa ajili yangu, na matanzi yao watendao maovu.
10 Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe, wakati mimi ninapita salama.
Waovu na waangukie kwenye nyavu zao wenywe pindi mimi nitorokapo.