< Zaburi 139 >
1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, umenichunguza na kunijua.
Ee Yahwe, wewe umenichunguza, na unanijua.
2 Unajua ninapoketi na ninapoinuka; unatambua mawazo yangu tokea mbali.
Wewe unajua nikaapo na niinukapo; unayajua mawazo yangu tokea mbali sana.
3 Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu; unaelewa njia zangu zote.
Unachunguza wenendo wangu na kulala kwangu; unazijua njia zangu zote.
4 Kabla neno halijafika katika ulimi wangu, wewe walijua kikamilifu, Ee Bwana.
Kabla hakujawa na neno kwenye ulimi wangu, wewe unalijua kabisa, Yahwe.
5 Umenizunguka nyuma na mbele; umeweka mkono wako juu yangu.
Nyuma yangu na mbele yangu unanizunguka na kuniwekea mkono wako.
6 Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu, ni ya juu sana kwangu kuyafikia.
Maarifa hayo ni mengi yananizidi mimi; yako juu sana, nami siwezi kuyafikia.
7 Niende wapi nijiepushe na Roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako?
Niende wapi mbali na roho yako? Niende wapi niukimbie uwepo wako?
8 Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko; nikifanya vilindi kuwa kitanda changu, wewe uko huko. (Sheol )
Kama nikipaa mbinguni, uko huko; kama nikifanya kitanda changu Kuzimuni, tazama, uko huko. (Sheol )
9 Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko, kama nikikaa pande za mbali za bahari,
Kama nikipaa kwa mbawa za asubuhi na kwenda kuishi pande za mwisho wa bahari,
10 hata huko mkono wako utaniongoza, mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti.
hata huko mkono wako utaniongoza, mkono wako wa kuume utanishika.
11 Kama nikisema, “Hakika giza litanificha na nuru inayonizunguka iwe usiku,”
Kama nikisema, “Hakika giza litanifunika, na nuru inizungukayo itakuwa usiku,”
12 hata giza halitakuwa giza kwako, usiku utangʼaa kama mchana, kwa kuwa giza ni kama nuru kwako.
Hata giza lisingweza kuwa giza kwako. Usiku ungeng'aa kama mchana, maana giza na nuru kwako vinafanana.
13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani; uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.
Wewe uliumba sehemu zangu za ndani; uliniumba tumboni mwa mama yangu.
14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa kwa namna ya ajabu na ya kutisha; kazi zako ni za ajabu, ninajua hayo kikamilifu.
Nitakusifu, kwa maana nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu. Nafsi yangu yalijua hili vizuri sana.
15 Umbile langu halikufichika kwako, nilipoumbwa mahali pa siri. Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,
Mifupa yangu haikusitirika kwako nilipoumbwa kwa siri, nilipoumbwa kwa ustadi pande za chini za nchi.
16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika. Siku zangu zote ulizonipangia ziliandikwa katika kitabu chako kabla haijakuwepo hata moja.
Uliniona ndani ya tumbo; siku zote zilizo pangwa kwangu ziliandikwa kitabuni mwako hata kabla ya siku ya kwanza kutokea.
17 Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu! Jinsi jumla yake ilivyo kubwa!
Ni jinsi gani mawazo yako ni ya thamani kwangu, Mungu! Njinsi ilivyo kubwa jumla zake!
18 Kama ningezihesabu, zingekuwa nyingi kuliko mchanga. Niamkapo, bado niko pamoja nawe.
Kama nikijaribu kuyahesabu ni mengi kuliko mchanga. Niamkapo bado niko na wewe.
19 Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu! Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu!
Ee Mungu, kama ungewaua waovu; ondokeni kwangu enyi watu wenye vurugu.
20 Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya, adui zako wanatumia vibaya jina lako.
Wanakuasi wewe na kutenda udanganyifu; adui zako wananena uongo.
21 Ee Bwana, je, nisiwachukie wanaokuchukia? Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako?
Je, siwachukii hao, wale wakuchukiao Yahwe? Je, siwadharau wale wanao inuka dhidi yako?
22 Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao, ninawahesabu ni adui zangu.
Nawachukia kabisa; wamekuwa adui zangu.
23 Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu, nijaribu na ujue mawazo yangu.
Ee Mungu, unichunguze na kuujua moyo wangu; unijaribu na uyajue mawazo yangu.
24 Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu, uniongoze katika njia ya milele.
Uone kama kuna njia ya uovu ndani yangu, na uniongoze katika njia ya milele.