< Zaburi 138 >

1 Zaburi ya Daudi. Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kwa moyo wangu wote, mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako. 2 Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu, nami nitalisifu jina lako kwa ajili ya upendo wako na uaminifu, kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako juu ya vitu vyote. 3 Nilipoita, ulinijibu; ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari. 4 Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Bwana, wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako. 5 Wao na waimbe kuhusu njia za Bwana, kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu. 6 Ingawa Bwana yuko juu, humwangalia mnyonge, bali mwenye kiburi yeye anamjua kutokea mbali. 7 Nijapopita katikati ya shida, wewe unayahifadhi maisha yangu, unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu, kwa mkono wako wa kuume unaniokoa. 8 Bwana atatimiza kusudi lake kwangu, Ee Bwana, upendo wako wadumu milele: usiziache kazi za mikono yako.

< Zaburi 138 >