< Zaburi 135 >
1 Msifuni Bwana. Lisifuni jina la Bwana, msifuni, enyi watumishi wa Bwana,
Msifuni Yahwe. Lisifuni jina la Yahwe. Msifuni yeye, enyi watumishi wa Yahwe,
2 ninyi ambao mnatumika ndani ya nyumba ya Bwana, katika nyua za nyumba ya Mungu wetu.
ninyi msimamao katika nyumba ya Yahwe, katika nyua za nyumba ya Mungu wetu.
3 Msifuni Bwana, kwa kuwa Bwana ni mwema, liimbieni sifa jina lake, kwa maana hilo lapendeza.
Msifuni Yahwe, kwa kuwa ni mwema; liimbieni sifa jina lake, maana ni vizuri kufanya hivyo.
4 Kwa maana Bwana amemchagua Yakobo kuwa wake mwenyewe, Israeli kuwa mali yake ya thamani.
Kwa kuwa Yahwe amemchagua Yakobo kwa ajili yake mwenyewe, Israeli kama urithi wake.
5 Ninajua ya kuwa Bwana ni mkuu, kwamba Bwana wetu ni mkuu kuliko miungu yote.
Najua ya kuwa Yahwe ni mkuu, na kwamba Bwana wetu yuko juu ya miungu yote.
6 Bwana hufanya lolote apendalo, mbinguni na duniani, katika bahari na vilindi vyake vyote.
Chochote Yahwe apendacho, hufanya mbinguni, duniani, katika bahari na katika vilindi vyote.
7 Hufanya mawingu kupanda kutoka miisho ya dunia; hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua na huleta upepo kutoka ghala zake.
Hushusha mawingu kutoka mbali, akifanya mianga ya radi kuongozana na mvua na kuleta upepo toka katika ghala yake.
8 Alimuua mzaliwa wa kwanza wa Misri, mzaliwa wa kwanza wa wanadamu na wanyama.
Aliua mzaliwa wa kwanza wa Misri, wote wanadamu na wanyama.
9 Alipeleka ishara zake na maajabu katikati yako, ee Misri, dhidi ya Farao na watumishi wake wote.
Alituma ishara na maajabu kati yako Misri, dhidi ya Farao na watumishi wake wote.
10 Aliyapiga mataifa mengi, na akaua wafalme wenye nguvu:
Aliwashambulia mataifa mengi na aliua wafalme wenye nguvu,
11 Mfalme Sihoni na Waamori, Ogu mfalme wa Bashani na wafalme wote wa Kanaani:
Sihoni mfalme wa Waamori na Ogu mfalme wa Bashani na falme zote za Kanaani.
12 akatoa nchi yao kuwa urithi, urithi kwa watu wake Israeli.
Alitupatia sisi nchi yao kama urithi, urithi wa Israeli watu wake.
13 Ee Bwana, jina lako ladumu milele, kumbukumbu za fahari zako, Ee Bwana, kwa vizazi vyote.
Jina lako, Yahwe, inadumu milele; Yahwe, kumbukumbu lako vizazi hata vizazi.
14 Maana Bwana atawathibitisha watu wake, na kuwahurumia watumishi wake.
Kwa kuwa Bwana huwatetea watu wake na anahuruma juu ya watumishi wake.
15 Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu, zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu, kazi ya mikono ya wanadamu.
16 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema, zina macho, lakini haziwezi kuona;
Sanamu hizo zina vinywa, lakini haziongei; zina macho, lakini hazioni;
17 zina masikio, lakini haziwezi kusikia, wala hakuna pumzi katika vinywa vyao.
zina masikio, lakini hazisikii, wala vinywani mwao hamna pumzi.
18 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo, vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.
Wale wazitengenezao wanafanana nazo, vilevile kila anaye zitumainia.
19 Ee nyumba ya Israeli, msifuni Bwana; ee nyumba ya Aroni, msifuni Bwana;
Enyi kizazi cha Israeli, mtukuzeni Yahwe; kizazi cha Haruni, mtukuzeni Yahwe.
20 ee nyumba ya Lawi, msifuni Bwana; ninyi mnaomcha, msifuni Bwana.
Kizazi cha Lawi, mtukuzeni Yahwe.
21 Msifuni Bwana kutoka Sayuni, msifuni yeye aishiye Yerusalemu. Msifuni Bwana.
Atukuzwe Yahwe katika Sayuni, yeye aishiye Yerusalemu. Msifuni Yahwe.