< Zaburi 132 >

1 Wimbo wa kwenda juu. Ee Bwana, mkumbuke Daudi na taabu zote alizozistahimili.
Yahwe, kwa ajili ya Daudi kumbuka mateso yake yote.
2 Aliapa kiapo kwa Bwana na akaweka nadhiri kwa Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo:
Kumbuka ndiye aliye mwapia Yahwe, aliweka nadhiri kwa Shujaa wa Yakobo.
3 “Sitaingia nyumbani mwangu au kwenda kitandani mwangu:
Alisema, sitaingia nyumbani mwangu wala sitaenda kitandani mwangu,
4 sitaruhusu usingizi katika macho yangu, wala kope zangu kusinzia,
sitayapa macho yangu usingizi wala kope zangu kupumzika
5 mpaka nitakapompatia Bwana mahali, makao kwa ajili ya Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo.”
mpaka nitakapopata mahali kwa ajili ya Yahwe, na maskani kwa ajili ya Shujaa wa Yakobo.”
6 Tulisikia habari hii huko Efrathi, tulikutana nayo katika mashamba ya Yaara:
Tazama tulisikia kuhusu hilo katika Efrata; tuliipata katika konde la Yearimu.
7 “Twendeni kwenye makao yake, na tuabudu kwenye kiti cha kuwekea miguu yake;
Tutaingia katika maskani ya Mungu; tutasujudu miguuni pake.
8 inuka, Ee Bwana, uje mahali pako pa kupumzikia, wewe na Sanduku la nguvu zako.
Inuka, Ee Yahwe, uje mahali pako pa kupumzika, wewe na sanduku la nguvu zako!
9 Makuhani wako na wavikwe haki, watakatifu wako na waimbe kwa furaha.”
Makuhani wako na wavikwe uadilifu; waaminifu wako washangilie.
10 Kwa ajili ya Daudi mtumishi wako, usimkatae mpakwa mafuta wako.
Kwa ajili ya mtumishi wako Daudi, usimuache mfalme wako uliye mpaka mafuta.
11 Bwana alimwapia Daudi kiapo, kiapo cha uhakika ambacho hatakitangua: “Nitamweka mmoja wa wazao wako mwenyewe katika kiti chako cha enzi,
Yahwe alimwapia Daudi kiapo cha uhakika, kiapo cha uhakika ambacho hatakivunja: “Nitamuweka mmoja wa wazawa wako kwenye kiti chako cha enzi.
12 kama wanao watashika Agano langu na sheria ninazowafundisha, ndipo wana wao watarithi kiti chako cha enzi milele na milele.”
Kama wana wako watalishika agano langu na sheria ambazo nitawafundisha, watoto wao pia watakaa kwenye kiti chako cha enzi milele.”
13 Kwa maana Bwana ameichagua Sayuni, amepaonea shauku pawe maskani yake:
Hakika Yahwe ameichagua Sayuni, ameitamani kwa ajili ya makao yake.
14 “Hapa ni mahali pangu pa kupumzika milele na milele; hapa ndipo nitakapoketi nikitawala, kwa sababu nimepaonea shauku:
“Hapa ni mahali pangu pa kupumzika milele. Nitaishi hapa, kwa kuwa ninapatamani.
15 Nitambariki kwa kumpa mahitaji tele: nitashibisha maskini wake kwa chakula.
Nitapabariki sana kwa mahitaji. Nitawatosheleza maskini wake kwa mkate.
16 Nitawavika makuhani wake wokovu, nao watakatifu wake watadumu wakiimba kwa furaha.
Nitawavisha makuhani wake kwa wokovu, waaminifu wake watashangilia kwa furaha.
17 “Hapa nitamchipushia Daudi pembe, na kuweka taa kwa ajili ya masiya wangu.
Hapo nitachipusha pembe kwa ajili ya Daudi na kuweka taa juu kwa ajili ya mpakwa mafuta wangu.
18 Adui zake nitawavika aibu, bali taji kichwani pake itangʼaa sana.”
Nitawavisha adui kwa aibu, bali juu yake taji yake itang'aa.”

< Zaburi 132 >