< Zaburi 119 >
1 Heri wale walio waadilifu katika njia zao, wanaoenenda katika sheria ya Bwana.
Wamebarikiwa wale ambao njia zao hazina lawama, waenendao katika sheria ya Yahwe.
2 Heri wale wanaozishika shuhuda zake, wamtafutao kwa moyo wao wote.
Wamebarikiwa wale wazishikao amri zake thabiti, wamtafutao kwa moyo wao wote.
3 Wasiofanya lolote lililo baya, wanaoenenda katika njia zake.
Hawatendi makosa; wanaenenda katika njia zake.
4 Umetoa maagizo yako ili tuyatii kwa ukamilifu.
Wewe umetuamuru kuyashika maagizo yako ili tuyachunguze kwa umakini.
5 Laiti mwenendo wangu ungekuwa imara katika kuyatii maagizo yako!
Oh, ningependa njia zangu ziwe thabiti nizitii amri zako!
6 Hivyo mimi sitaaibishwa ninapozingatia amri zako zote.
Ndipo sitaaibika nizifikiripo amri zako zote.
7 Nitakusifu kwa moyo mnyofu ninapojifunza sheria zako za haki.
Nitakushukuru wewe kwa unyofu wangu wa moyo nijifunzapo amri za haki yako.
8 Nitayatii maagizo yako; usiniache kabisa.
Nitazitii amri zako; usiniache peke yangu. BETH.
9 Kijana aifanye njia yake kuwa safi jinsi gani? Ni kwa kutii, akilifuata neno lako.
Ni jinsi gani kijana aweza kuendelea kuishi katika njia yake ya utakatifu? Ni kwa kulitii neno lako.
10 Ninakutafuta kwa moyo wangu wote, usiniache niende mbali na amri zako.
Kwa moyo wangu wote ninakutafuta wewe; Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
11 Nimelificha neno lako moyoni mwangu ili nisikutende dhambi.
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako ili nisije nikakutenda dhambi.
12 Sifa ni zako, Ee Bwana, nifundishe maagizo yako.
Umetukuka, Yahwe; unifundishe amri zako.
13 Kwa midomo yangu nitasimulia sheria zote zinazotoka katika kinywa chako.
Kwa kinywa changu nimetangaza amri ya haki yako yote ambayo umeifunua.
14 Ninafurahia kufuata sheria zako kama mtu afurahiaye mali nyingi.
Ninafurahi katika njia ya amri za agano lako zaidi kuliko katika utajiri.
15 Ninatafakari maagizo yako na kuziangalia njia zako.
Nitayatafakari maagizo yako na kuzitilia maanani njia zako.
16 Ninafurahia maagizo yako, wala sitalipuuza neno lako.
Ninafurahia katika amri zako; sitalisahau neno lako. GIMEL.
17 Mtendee mema mtumishi wako, nami nitaishi; nitalitii neno lako.
Uwe mwema kwa mtumishi wako ili niweze kuishi na kulishika neno lako.
18 Yafungue macho yangu nipate kuona mambo ya ajabu katika sheria yako.
Ufungue macho yangu ili niweze kuona mambo ya ajabu katika sheria yako.
19 Mimi ni mgeni duniani, usinifiche amri zako.
Mimi ni mgeni katika nchi; usizifiche amri zako mbali nami.
20 Nafsi yangu inataabika kwa shauku kubwa juu ya sheria zako wakati wote.
Moyo wangu unauma kwa kutamani sana kuzijua amri zako za haki wakati wote.
21 Unawakemea wenye majivuno, waliolaaniwa waendao mbali na amri zako.
Wewe huwakemea wenye kiburi, waliolaaniwa, wanao tanga-tanga mbali na amri zako.
22 Niondolee dharau na dhihaka, kwa kuwa ninazishika sheria zako.
Uniokoe dhidi ya aibu na udhalilishaji, maana nimezitii amri za agano lako.
23 Ingawa watawala huketi pamoja na kunisingizia, mtumishi wako atatafakari juu ya maagizo yako.
Ingawa watawala wanapanga njama na kunikashfu, mtumishi wako huzitafakali amri zako.
24 Sheria zako ni furaha yangu, nazo ni washauri wangu.
Amri za agano lako ni furaha yangu, na washauri wangu. DALETH.
25 Nimelazwa chini mavumbini, yahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako.
Uhai wangu unashikamana na mavumbi! nipe uhai kwa neno lako.
26 Nilikueleza njia zangu ukanijibu, nifundishe sheria zako.
Nilikuambia mapito yangu, na ulinijibu; nifundishe sheria zako.
27 Nijulishe mafundisho ya mausia yako, nami nitatafakari maajabu yako.
Unifahamishe njia ya maagizo yako, ili niweze kutafakari juu ya mafundisho yako ya ajabu.
28 Nafsi yangu imechakazwa kwa huzuni, uniimarishe sawasawa na neno lako.
Nimelemewa na huzuni! Nitie nguvu kwa neno lako.
29 Niepushe na njia za udanganyifu, kwa neema unifundishe sheria zako.
Uiondoe kwangu njia ya udanganyifu; kwa wema wako unifundishe sheria yako.
30 Nimechagua njia ya kweli, nimekaza moyo wangu katika sheria zako.
Nimechagua njia ya uaminifu; siku zote nimeweka amri za haki yako mbele yangu.
31 Nimengʼangʼania sheria zako, Ee Bwana, usiniache niaibishwe.
Ninashikamana na amri za agano lako; Yahwe, usiniache niaibike.
32 Nakimbilia katika njia ya maagizo yako, kwa kuwa umeuweka moyo wangu huru.
Nitakimbia katika njia ya amri zako, kwa sababu wausukuma moyo wangu kufanya hivyo. HE
33 Ee Bwana, nifundishe kuyafuata maagizo yako, nami nitayashika mpaka mwisho.
Unifundishe, Yahwe, njia za sheria yako, nami nitazishika hadi mwisho.
34 Nipe ufahamu, nami nitaishika sheria yako na kuitii kwa moyo wangu wote.
Unipe uelewa, nami nitazishika sheria zako; nitazitii kwa moyo wangu wote.
35 Niongoze kwenye njia ya amri zako, kwa kuwa huko napata furaha.
Uniongoze katika njia ya amri zako, maana ninafurahi kuenenda katika hizo.
36 Ugeuze moyo wangu kuelekea sheria zako, na siyo kwenye mambo ya ubinafsi.
Uelekeze moyo wangu kuzielekea amari za agano lako na uniweke mbali na matendo yasiyo haki tena.
37 Geuza macho yangu kutoka kwenye mambo yasiyofaa, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako.
Uyageuze macho yangu dhidi ya kutazama mambo yasiyofaa; unihuishe katika njia zako.
38 Mtimizie mtumishi wako ahadi yako, ili upate kuogopwa.
Umtendee mtumishi wako ahadi ambayo uliifanya kwa wale wanaokuheshimu wewe.
39 Niondolee aibu ninayoiogopa, kwa kuwa sheria zako ni njema.
Uniondolee shutumu niiogopayo, maana hukumu zako za haki ni njema.
40 Tazama jinsi ninavyoonea shauku mausia yako! Hifadhi maisha yangu katika haki yako.
Tazama, nimeyatamani maagizo yako; unihuishe katika haki yako. VAV.
41 Ee Bwana, upendo wako usiokoma unijie, wokovu wako sawasawa na ahadi yako,
Ee Yahwe, unipe upendo wako usiokwisha na wokovu wako kulingana na ahadi yako;
42 ndipo nitakapomjibu anayenidhihaki, kwa kuwa ninalitumainia neno lako.
ndipo nitakuwa na jibu kwa ajili ya yule anayenidhihaki.
43 Usilinyakue neno la kweli kutoka kinywani mwangu, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika amri zako.
Usiliondoe neno la kweli mdomoni mwangu, maana nimesubiri kwa ajili ya amri zako za haki.
44 Nitaitii amri yako daima, naam, milele na milele.
Nitazitii sheria zako siku zote, milele na milele.
45 Nitatembea nikiwa huru, kwa kuwa nimejifunza mausia yako.
Nitaenenda salama, maana ninayatafuta maagizo yako.
46 Nitasema sheria zako mbele za wafalme wala sitaaibishwa,
Nitazinena amri zako thabiti mbele ya wafalme nami sitaaibika.
47 kwa kuwa ninazifurahia amri zako kwa sababu ninazipenda.
Ninafurahia katika amri zako, nizipendazo sana.
48 Ninaziinulia amri zako ambazo ninazipenda mikono yangu, nami ninatafakari juu ya maagizo yako.
Nitaziinulia mikono yangu amri zako, nizipendazo; nitazitafakari sheria zako. ZAYIN.
49 Kumbuka neno lako kwa mtumishi wako, kwa sababu umenipa tumaini.
Kumbuka ahadi yako kwa mtumishi wako kwa sababu umenipa tumaini.
50 Faraja yangu katika mateso yangu ni hii: Ahadi yako inahifadhi maisha yangu.
Hii ni faraja yangu katika mateso: kuwa ahadi yako imeniweka hai.
51 Wenye majivuno wamenisimanga bila kuchoka, hata hivyo sitaiacha sheria yako.
Wenye kiburi wamenicheka, lakini sijaiacha sheria yako.
52 Ee Bwana, ninazikumbuka sheria zako za zamani, nazo zinanifariji.
Nimezitafakari amri zako za haki tangu zamani, Yahwe, nami ninajifariji mwenyewe.
53 Nimeshikwa sana na ghadhabu kwa ajili ya waovu, ambao wameacha sheria yako.
Hasira kali imenishikilia kwa sababu ya waovu wanaoikataa sheria yako.
54 Maagizo yako ni kiini cha nyimbo zangu popote ninapoishi.
Sheria zako zimekuwa nyimbo zangu katika nyumba ninayoishi kwa muda.
55 Ee Bwana, wakati wa usiku ninalikumbuka jina lako, nami nitatii sheria yako.
Ninalifikiria jina lako wakati wa usiku, Yahwe, na kuzishika sheria zako.
56 Hili limekuwa zoezi langu: nami ninayatii mausia yako.
Hili limekuwa zoezi langu kwa sababu nimeyatii maagizo yako. HETH.
57 Ee Bwana, wewe ni fungu langu, nimeahidi kuyatii maneno yako.
Yahwe ni sehemu yangu; nimeamua kuyatii maneno yake.
58 Nimetafuta uso wako kwa moyo wangu wote, nihurumie sawasawa na ahadi yako.
Kwa bidii ninaomba neema yako kwa moyo wangu wote; unihurumie, kama neno lako lilivyo ahidi.
59 Nimezifikiri njia zangu na nimeelekeza hatua zangu katika mausia yako.
Nilizichunguza njia zangu na kugeuzia miguu yangu kwenye amri za agano lako.
60 Nitafanya haraka bila kuchelewa kuzitii amri zako.
Naharakisha na sichelewi kuzishika amri zako.
61 Hata waovu wanifunge kwa kamba, sitasahau sheria yako.
Kamba za waovu zimenifunga; nami sijaisahau sheria yako.
62 Usiku wa manane ninaamka kukushukuru kwa sababu ya sheria zako za haki.
Katikati ya usiku ninaamka kukushukuru wewe kwa sababu ya amri za haki yako.
63 Mimi ni rafiki kwa wale wote wakuchao, kwa wote wanaofuata mausia yako.
Ninaurafiki na wale wanao kuabudu wewe, wale wote watiio maagizo yako.
64 Ee Bwana, dunia imejaa upendo wako, nifundishe maagizo yako.
Yahwe, nchi, imejaa uaminifu wa agano lako; unifundishe sheria zako. TETH.
65 Mtendee wema mtumishi wako Ee Bwana, sawasawa na neno lako.
Wewe umemtendea mema mtumishi wako, Yahwe, sawasawa na neno lako.
66 Nifundishe maarifa na uamuzi mzuri, kwa kuwa ninaamini amri zako.
Unifundishe utambuzi sahihi na uelewa, kwa kuwa nimeamini katika amri zako.
67 Kabla sijapata shida nilipotea njia, lakini sasa ninalitii neno lako.
Kabla sijateswa nilipotea, lakini sasa nimelitii neno lako.
68 Wewe ni mwema, unalotenda ni jema, nifundishe maagizo yako.
Wewe ni mwema, na ndiye yule utendaye mema; unifundishe sheria zako.
69 Ingawa wenye majivuno wamenisingizia uongo, nitafuata mausia yako kwa moyo wangu wote.
Wenye kiburi wamenichafua kwa uongo, lakini niliyashika maagizo yako kwa moyo wangu wote.
70 Mioyo yao ni katili na migumu, bali mimi napendezwa na sheria yako.
Mioyo yao ni migumu, lakini ninafurahia katika sheria yako.
71 Ilikuwa vyema mimi kupata shida ili nipate kujifunza maagizo yako.
Ni vizuri kwangu kuwa nimeteseka ili niweze kujifunza sheria zako.
72 Sheria inayotoka kinywani mwako ina thamani kubwa kwangu kuliko maelfu ya vipande vya fedha na dhahabu.
Maagizo yatokayo kinywani mwako ni ya thamani zaidi kwangu kuliko maelfu ya vipande vya dhahabu na fedha. YOD.
73 Mikono yako ilinifanya na kuniumba, nipe ufahamu niweze kujifunza amri zako.
Mikono yako imeniumba na kunitengeneza; unipe uelewa ili niweze kujifunza amri zako.
74 Wakuchao wafurahie wanaponiona, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika neno lako.
Wale wanao kucha wewe watafurahi wanionapo kwa sababu ninapata tumaini katika neno lako.
75 Ee Bwana, ninajua kwamba sheria zako ni za haki, katika uaminifu wako umeniadhibu.
Ninajua, Yahwe, kuwa amri zako ni za haki, na kuwa katika uaminifu ulinitesa.
76 Upendo wako usiokoma uwe faraja yangu, sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako.
Agano lako aminifu na linifariji, kama ulivyomwahidi mtumishi wako.
77 Huruma yako na inijie ili nipate kuishi, kwa kuwa naifurahia sheria yako.
Unihurumie ili niweze kuishi, kwa maana sheria yako ni furaha yangu.
78 Wenye majivuno na waaibishwe kwa kunikosea mimi bila sababu, lakini mimi nitatafakari juu ya mausia yako.
Wenye kiburi na waaibishwe, maana wamenitukana; bali mimi nitayatafakari maagizo yako.
79 Wale wakuchao na wanigeukie mimi, hao ambao wanazielewa sheria zako.
Wale wote wanao kucha wewe na wanigeukie, wale wazijuao amri za agano lako.
80 Moyo wangu usiwe na lawama katika kutii maagizo yako, ili nisiaibishwe.
Moyo wangu uwe mkamilifu pamoja na heshima kwa sheria zako ili nisiaibike. KAPH.
81 Nafsi yangu inazimia kwa kutamani wokovu wako, lakini nimeweka tumaini langu katika neno lako.
Ninazimia kwa kutamani sana kuwa wewe unaweza kuniokoa! Ninamatumaini katika neno lako.
82 Macho yangu yamefifia, nikingoja ahadi yako; ninasema, “Utanifajiri lini?”
Macho yangu yanatamani sana kuiona ahadi yako; ni lini utanifariji mimi?
83 Ingawa nimekuwa kama kiriba kwenye moshi, bado sijasahau maagizo yako.
Kwa maana nimekuwa kama kiriba katika moshi; sisahau sheria zako.
84 Mtumishi wako itampasa angoje mpaka lini? Ni lini utawaadhibu washtaki wangu?
Ni kwa muda gani gani mtumishi wako atalazimika kuyavumilia haya; ni lini utawahukumu wale wanaonitesa?
85 Wenye majivuno wananichimbia mashimo, kinyume na sheria yako.
Wenye kiburi wamenichimbia shimo, wasiotii sheria yako.
86 Amri zako zote ni za kuaminika; unisaidie, kwa sababu watu wananishtaki bila sababu.
Amri zako zote ni za kuaminika; wale watu walinitesa bila ya haki; unisaidie.
87 Walikaribia kabisa kunifuta kutoka uso wa dunia, lakini sijaacha mausia yako.
karibu kunifanya nifikie mwisho juu ya nchi hii, lakini siyakatai maagizo yako.
88 Yahifadhi maisha yangu sawasawa na upendo wako, nami nitatii sheria za kinywa chako.
Kwa upendo wako thabiti, uniweke hai, ili niweze kuzitii amri zako. LAMEDH.
89 Ee Bwana, neno lako ni la milele, linasimama imara mbinguni.
Yahwe, neno lako linasimama milele; neno lako limefanywa imara mbinguni.
90 Uaminifu wako unaendelea kwa vizazi vyote, umeiumba dunia, nayo inadumu.
Uaminifu wako wadumu kwa ajili ya vizazi vyote; umeiimarisha nchi, nayo inadumu.
91 Sheria zako zinadumu hadi leo, kwa kuwa vitu vyote vinakutumikia.
Vitu yote yaliendelea mpaka leo hii, kama vile ulivyosema katika amri zako za haki, maana vitu vyote ni watumishi wako.
92 Kama nisingefurahia sheria yako, ningeangamia katika taabu zangu.
Kama sheria yako isingekuwa furaha yangu, ningeangamia katika mateso yangu.
93 Sitasahau mausia yako kamwe, kwa maana kwayo umehifadhi maisha yangu.
Sitayasahau kamwe maagizo yako, maana kupitia hayo umeniweka hai.
94 Uniokoe, kwa maana mimi ni wako, kwa kuwa nimetafuta mausia yako.
Mimi ni wako, kwa maana ninayatafuta maagizo yao.
95 Waovu wanangojea kuniangamiza, bali mimi ninatafakari sheria zako.
Waovu hujiandaa kuniangamiza, lakini nitatafuta kuzielewa amri za agano lako.
96 Katika ukamilifu wote ninaona mna kikomo, lakini amri zako hazina mpaka.
Nimeona kuwa kila kitu kina mipaka, lakini amri zako ni pana, zaidi ya mipaka. MEM.
97 Aha! Tazama, sheria yako naipenda mno ajabu. Ninaitafakari mchana kutwa.
Oh ni jinsi gani naipenda sheria yako! Ni tafakari yangu mchana kutwa.
98 Amri zako zimenipa hekima zaidi kuliko adui zangu, kwa kuwa nimezishika daima.
Amri zako hunifanya mwenye hekima kuliko adui zangu, maana amri zako siku zote ziko pamoja nami.
99 Nina akili zaidi kuliko walimu wangu wote, kwa kuwa ninatafakari juu ya sheria zako.
Ninauelewa zaidi kuliko walimu wangu wote, kwa maana ninazitafakari amri za agano lako.
100 Nina ufahamu zaidi kuliko wazee, kwa kuwa ninayatii mausia yako.
Ninaelewa kuliko wale wanaonizidi umri; hii ni kwa sababu nimeyashika maagizo yako.
101 Nimezuia miguu yangu isiende kwenye kila njia mbaya, ili niweze kutii neno lako.
Nimeiepusha miguu yangu na kila njia ya uovu ili niweze kulitii neno lako.
102 Sijaziacha sheria zako, kwa kuwa umenifundisha wewe mwenyewe.
Sijaenda kinyume na amri zako za haki, kwa maana wewe umenifundisha.
103 Tazama jinsi maneno yako yalivyo matamu kwangu, matamu kuliko asali katika kinywa changu!
Ni jinsi gani maneno yako ni matamu kwenye majaribu yangu, naam, matamu kuliko asali kinywani mwangu!
104 Ninapata ufahamu kutoka mausia yako, kwa hiyo ninachukia kila njia ya upotovu.
Kupitia maagizo yako ninapata utambuzi; kwa hiyo kila njia isiyo ya kweli.
105 Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga katika njia yangu.
Neno lako ni taa ya mguu miguu yangu na mwanga wa njia yangu.
106 Nimeapa na nimethibitisha, kwamba nitafuata sheria zako za haki.
Nimeapa na nimethibitisha, kuwa nitazitii amri za haki yako.
107 Nimeteseka sana, uhifadhi maisha yangu, Ee Bwana, sawasawa na neno lako.
Nimeteswa sana; uniweke hai, Yahwe, kama ulivyoahidi katika neno lako.
108 Ee Bwana, pokea sifa za hiari za kinywa changu, nifundishe sheria zako.
Yahwe, tafadhali pokea dhabihu yangu ya hiari ya kinywa changu, na unifundishe amri zako za haki.
109 Ingawa maisha yangu yako hatarini siku zote, sitasahau sheria yako.
Uhai wangu ziku zote uko mkononi mwangu, lakini bado sisahau sheria yako.
110 Waovu wamenitegea mtego, lakini sijayakiuka maagizo yako.
Waovu wamenitegea mtego, lakini sijapotea mbali na maagizo yako.
111 Sheria zako ni urithi wangu milele, naam ni furaha ya moyo wangu.
Nimezifanya amri za agano lako kama urithi wangu milele, maana hizo ni furaha ya moyo wangu.
112 Nimekusudia moyoni mwangu kuyafuata maagizo yako mpaka mwisho.
Moyo wangu umewekwa kuzitii sheria zako milele mpaka mwisho kabisa. SAMEKH.
113 Ninachukia watu wa nia mbili, lakini ninapenda sheria yako.
Ninawachukia watu wa kusita-sita, lakini naipenda sheria yako.
114 Wewe ni kimbilio langu na ngao yangu, nimeweka tumaini langu katika neno lako.
Wewe ni ficho langu na ngao yangu; nalingoja neno lako.
115 Ondokeni kwangu, ninyi mtendao mabaya, ili niweze kushika amri za Mungu wangu!
Ondokeni kwangu, ninyi mtendao uovu, ili niweze kuzitii amri za Mungu wangu.
116 Nihifadhi sawasawa na ahadi yako, nami nitaishi; usiache matumaini yangu yakavunjwa.
Uniwezeshe kwa neno lako ili niweze kuishi na nisiaibike na matumaini yangu.
117 Nitegemeze, nami nitaokolewa, nami daima nitayaheshimu maagizo yako.
Unisaidie, nami nitakuwa salama; siki zote nitazitafakari sheria zako.
118 Unawakataa wote wanaoyaasi maagizo yako, kwa maana udanganyifu wao ni bure.
Wewe huwakataa wale wote wapoteao mbali na sheria zako, maana watu hao ni wadanganyifu na si wakuaminika.
119 Waovu wa nchi unawatupa kama takataka, kwa hivyo nazipenda sheria zako.
Wewe huwaondoa waovu wa nchi kama takataka; kwa hiyo ninazipenda amri zako thabiti.
120 Mwili wangu unatetemeka kwa kukuogopa wewe, ninaziogopa sheria zako.
Mwili wangu hutetemeka kwa hofu yako, na ninaziogopa amri za haki yako. AYIN.
121 Nimetenda yaliyo haki na sawa, usiniache mikononi mwa watesi wangu.
Ninafanya kilicho sahihi na haki; usiniache kwa watesi wangu.
122 Mhakikishie mtumishi wako usalama, usiache wenye kiburi wanionee.
Uwe mdhamini wa ustawi wa mtumishi wako; usiwaache wenye kiburi wanionee.
123 Macho yangu yamefifia, yakitazamia wokovu wako, na kuitazamia ahadi yako ya kweli.
Macho yangu yanachoka kwa kuusubiri wokovu wako na neno lako la haki.
124 Mfanyie mtumishi wako kulingana na upendo wako na unifundishe maagizo yako.
Mwoneshe mtumishi wako uaminifu wa agano lako, na unifundishe sheria zako.
125 Mimi ni mtumishi wako; nipe ufahamu ili niweze kuelewa sheria zako.
Mimi ni mtumishi wako; unipe uelewa ili niweze kuzijua amri za agano lako.
126 Ee Bwana, wakati wako wa kutenda umewadia, kwa kuwa sheria yako inavunjwa.
Ni wakati wa Yahwe kutenda, kwa maana watu wamevunja sheria yako.
127 Kwa sababu nazipenda amri zako zaidi ya dhahabu, naam, zaidi ya dhahabu safi,
Hakika ninazipenda amri zako kuliko dhahabu, naam, kuliko dhahabu safi.
128 na kwa sababu naona maagizo yako yote ni adili, nachukia kila njia potovu.
Hivyo ninayafuata maagizo yako yote kwa makini, na ninachukia kila njia ya uongo. PE.
129 Sheria zako ni za ajabu, hivyo ninazitii.
Sheria zako ni za ajabu, ndiyo sababu ninazitii.
130 Kuingia kwa maneno yako kunaleta nuru, kunampa mjinga ufahamu.
Ufafanuzi wa maneno yako huleta nuru; na kumpa ufahamu mjinga.
131 Nimefungua kinywa changu na kuhema, nikitamani amri zako.
Ninafungua kinywa changu na kutweta, maana ninazitamani amri zako.
132 Nigeukie na unihurumie, kama uwafanyiavyo siku zote wale wanaolipenda jina lako.
Unigeukie na unihurumie, kama ufanyavyo siku zote kwa wale walipendao jina lako.
133 Ongoza hatua zangu kulingana na neno lako, usiache dhambi yoyote initawale.
Uziongoze hatua zangu kwa neno lako; usiruhusu dhambi yeyote initawale.
134 Niokoe na uonevu wa wanadamu, ili niweze kutii mausia yako.
Unikomboe dhidi ya wanadamu waonevu ili niyatii maagizo yako.
135 Mwangazie mtumishi wako uso wako na unifundishe amri zako.
Uso wako umwangazie mtumishi wako, na unifundishe sheria zako.
136 Chemchemi za machozi zinatiririka kutoka machoni yangu, kwa kuwa sheria yako haifuatwi.
Mito ya machozi yatiririka kutoka machoni pangu kwa sababu watu hawaitii sheria yako. TSADHE.
137 Ee Bwana, wewe ni mwenye haki, sheria zako ni sahihi.
Wewe ni mwenye haki, Yahwe, na amri zako ni haki.
138 Sheria ulizoziweka ni za haki, ni za kuaminika kikamilifu.
Umezipa amri za agano lako haki na uaminifu.
139 Jitihada yangu imenidhoofisha, kwa kuwa adui zangu wanayapuuza maneno yako.
Hasira imeniangamiza kwa sababu adui zangu husahau maneno yako.
140 Ahadi zako zimejaribiwa kikamilifu, mtumishi wako anazipenda.
Neno lako limepimwa sana, naye mtumishi wako analipenda.
141 Ingawa ni mdogo na ninadharauliwa, sisahau mausia yako.
Sina umuhimu na ninadharauliwa, lakini bado siyasahau maagizo yako.
142 Haki yako ni ya milele, na sheria yako ni kweli.
Hukumu yako ni ya haki milele, na sheria yako ni ya kuaminika.
143 Shida na dhiki zimenipata, lakini amri zako ni furaha yangu.
Japo dhiki na taabu vimenipata, amri zako bado ni furaha yangu.
144 Sheria zako ni sahihi milele, hunipa ufahamu ili nipate kuishi.
Amri za agano lako ni za haki milele; unipe uelewa ili niweze kuishi. QOPH.
145 Ee Bwana, ninakuita kwa moyo wangu wote, nami nitayatii maagizo yako.
Nililia kwa moyo wangu wote, “Unijibu, Yahwe, nitazishika sheria zako.
146 Ninakuita; niokoe nami nitazishika sheria zako.
Ninakuita wewe; uniokoe, nami nitazitii amri za agano lako.”
147 Ninaamka asubuhi na mapema na kukuomba msaada; nimeweka tumaini langu katika neno lako.
NInaamka asubuhi kabla jua halijachomoza na kulia kwa ajili ya msaada.
148 Sikufumba macho yangu usiku kucha, ili niweze kutafakari juu ya ahadi zako.
Ninatumaini katika maneno yako. Macho yangu yako wazi usiku kucha ili niweze kutafakari juu ya neno lako.
149 Usikie sauti yangu sawasawa na upendo wako, Ee Bwana, uyahifadhi maisha yangu, sawasawa na sheria zako.
Sikia sauti yangu katika uaminifu wa agano lako; uniweke hai, Yahwe, kama ulivyoahidi katika amri zako za haki.
150 Wale wanaopanga mipango miovu wako karibu nami, lakini wako mbali na sheria yako.
Wale wanaonitesa wananikaribia, lakini wako mbali na sheria yako.
151 Ee Bwana, hata hivyo wewe u karibu, na amri zako zote ni za kweli.
Wewe uko karibu, Yahwe, na amri zako ni za kuaminika.
152 Tangu zamani nimejifunza kutoka shuhuda zako kwamba umezithibitisha ili zidumu milele.
Muda mrefu uliopita nilijifunza kutoka katika amri za agano lako ulizoziweka katika mahali pa milele. RESH.
153 Yaangalie mateso yangu, uniokoe, kwa kuwa sijasahau sheria yako.
Uyatazame mateso yangu na unisaidie, maana siisahau sheria yako.
154 Nitetee katika hali hii yangu na unikomboe, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na ahadi yako.
Unitetee na kunikomboa; unihifadhi, kama ulivyo ahidi katika neno lako.
155 Wokovu uko mbali na waovu, kwa kuwa hawatafuti maagizo yako.
Wokovu uko mbali na waovu, maana hawazipendi amri zako.
156 Ee Bwana, huruma zako ni kuu, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na sheria zako.
Matendo yako ya huruma ni makuu, Yahwe; uniweke hai; kama ufanyavyo siku zote.
157 Adui wanaonitesa ni wengi, lakini mimi sitaziacha sheria zako.
Watesi wangu na adui zangu ni wengi, lakini bado sijaenda mbali na amri za agano lako.
158 Ninawatazama wasioamini kwa chuki, kwa kuwa hawalitii neno lako.
Nimewaona wasaliti wakitia kinyaa kwa sababu hawalishiki neno lako.
159 Tazama jinsi ninavyopenda mausia yako; Ee Bwana, uyahifadhi maisha yangu, sawasawa na upendo wako.
Tazama jinsi niyapendavyo maagizo yako; uniweke hai, Yahwe, kama ulivyoahidi katika uaminifu wa agano lako.
160 Maneno yako yote ni kweli, sheria zako zote za haki ni za milele.
Kiini cha neno lako ni kweli; kila mmoja mwenye amri za haki hudumu milele. SHIN.
161 Watawala wamenitesa bila sababu, lakini moyo wangu unatetemeka kwa neno lako.
Wakuu hunitesa bila sababu; moyo wangu hutetemeka, ukiogopa kutolitii neno lako.
162 Nafurahia ahadi zako kama mtu aliyepata mateka mengi.
Ninalifurahia neno lako kama apataye nyara nyingi.
163 Ninachukia na kuchukizwa sana na uongo, lakini napenda sheria yako.
Ninachukia na kudharau uongo, lakini naipenda sheria yako.
164 Ninakusifu mara saba kwa siku, kwa ajili ya sheria zako za haki.
Mara saba kwa siku ninakusifu wewe kwa sababu ya amri zako za haki.
165 Wanaopenda sheria yako wana amani tele, wala hakuna kitu kinachoweza kuwakwaza.
Wana amani nyingi, waipendao sheria yako; hakuna cha kuwatia mashakani.
166 Ee Bwana, ninangojea wokovu wako, nami ninafuata amri zako,
Naungoja wokovu wako, Yahwe, na ninatii amri zako.
167 Ninazitii sheria zako, kwa sababu ninazipenda mno.
Ninazishika amri zako thabiti, na ninazipenda sana.
168 Nimetii mausia yako na sheria zako, kwa kuwa njia zangu zote zinajulikana kwako.
Ninayashika maagizo yako na amri zako thabiti, kwa maana unajua kila kitu nifanyacho. TAV.
169 Ee Bwana, kilio changu na kifike mbele zako, nipe ufahamu sawasawa na neno lako.
Sikia kilio changu, Yahwe; unipe uelewa wa neno lako.
170 Maombi yangu na yafike mbele zako, niokoe sawasawa na ahadi yako.
Maombi yangu yaje mbele zako; unisaidie, kama ulivyoahidi katika neno lako.
171 Midomo yangu na ibubujike sifa, kwa kuwa unanifundisha maagizo yako.
Midomo yangu na imwage sifa, maana wewe unanifundisha sheria zako.
172 Ulimi wangu na uimbe kuhusu neno lako, kwa kuwa amri zako zote ni za haki.
Ulimi wangu na uimbe kuhusu neno lako, maana amri zako zote ni za haki.
173 Mkono wako uwe tayari kunisaidia, kwa kuwa nimechagua mausia yako.
Mkono wako unisaidie, maana nimechagua maagizo yako.
174 Ee Bwana, ninatamani wokovu wako, na sheria yako ni furaha yangu.
Ninautamani wokovu wako, Yahwe, na sheria yako ni furaha yangu.
175 Nijalie kuishi ili nipate kukusifu, na sheria zako zinitegemeze.
Naomba niishi na nikusifu wewe, na amri zako za haki zinisaidie.
176 Nimetangatanga kama kondoo aliyepotea. Mtafute mtumishi wako, kwa kuwa sijasahau amri zako.
Nimetanga-tanga kama kondoo aliyepotea; mtafute mtumishi wako, kwa maana sijazisahau amri zako.