< Zaburi 116 >

1 Ninampenda Bwana kwa maana amesikia sauti yangu; amesikia kilio changu ili anihurumie.
Nampenda Yahwe kwa kuwa anasikia sauti yangu na kuomba kwangu kwa ajili ya huruma.
2 Kwa sababu amenitegea sikio lake, nitamwita siku zote za maisha yangu.
Kwa sababu alinisikiliza, nitamuita yeye ningali ninaishi.
3 Kamba za mauti zilinizunguka, maumivu makuu ya kuzimu yalinipata, nikalemewa na taabu na huzuni. (Sheol h7585)
Kamba za mauti zilinizunguka, na mitego ya kuzimu ilinikabili; niliona dhiki na huzuni. (Sheol h7585)
4 Ndipo nikaliitia jina la Bwana: “Ee Bwana, niokoe!”
Kisha niliita kwa jina la Yahwe: “Tafadhali Yahwe, uiokoe nafsi yangu.”
5 Bwana ni mwenye neema na haki, Mungu wetu ni mwingi wa huruma.
Yahwe ni mwenye neema na haki; Mungu wetu ni mwenye huruma.
6 Bwana huwalinda wanyenyekevu, nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa.
Yahwe huwalinda wasio na hila; nilishushwa chini akaniokoa.
7 Ee nafsi yangu, tulia tena, kwa kuwa Bwana amekuwa mwema kwako.
Nafsi yangu inaweza kurudi mahali pake pa kupumzika, kwa kuwa Yahwe amekuwa mwema kwangu.
8 Kwa kuwa wewe, Ee Bwana, umeniokoa nafsi yangu na mauti, macho yangu kutokana na machozi, miguu yangu kutokana na kujikwaa,
Kwa maana uliokoa uhai wangu dhidi ya kifo, mcho yangu dhidi ya machozi, na miguu yangu dhidi ya kujikwaa.
9 ili niweze kutembea mbele za Bwana, katika nchi ya walio hai.
Nitamtumikia Yahwe katika nchi ya walio hai.
10 Niliamini, kwa hiyo nilisema, “Mimi nimeteseka sana.”
Nilimwamini yeye, hata niliposema, “nimeteswa sana.”
11 Katika taabu yangu nilisema, “Wanadamu wote ni waongo.”
Kwa haraka nilisema, “Watu wote ni waongo.”
12 Nimrudishie Bwana nini kwa wema wake wote alionitendea?
Nimlipeje Yahwe kwa wema wake wote kwangu?
13 Nitakiinua kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Bwana.
Nitakiinua kikombe cha wokovu, na kuliitia jina la Yahwe.
14 Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Bwana mbele za watu wake wote.
Nitatimiza viapo vyangu kwa Yahwe katika uwepo wa watu wake wote.
15 Kifo cha watakatifu kina thamani machoni pa Bwana.
Mauti ya wacha Mungu ina thamani machoni pa Mungu.
16 Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako, mimi ni mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako; umeniweka huru toka katika minyororo yangu.
Ee Yahwe, hakika, mimi ni mtumishi wako; mimi ni mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako; umefungua vifungo vyangu.
17 Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru na kuliita jina la Bwana.
Nitakutolea dhabihu ya shukrani na nitaliitia jina la Yahwe.
18 Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Bwana mbele za watu wake wote,
Nitatimiza viapo vyangu kwa Yahwe katika uwepo wa watu wake wote,
19 katika nyua za nyumba ya Bwana, katikati yako, ee Yerusalemu. Msifuni Bwana.
katika nyua za nyumba ya Yahwe, katikati yako, Yerusalemu. Msifuni Yahwe.

< Zaburi 116 >