< Zaburi 111 >

1 Msifuni Bwana. Nitamtukuza Bwana kwa moyo wangu wote, katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko. 2 Kazi za Bwana ni kuu, wote wanaopendezwa nazo huzitafakari. 3 Kazi zake zimejaa fahari na utukufu, haki yake hudumu daima. 4 Amefanya maajabu yake yakumbukwe, Bwana ni mwenye neema na huruma. 5 Huwapa chakula wale wanaomcha, hulikumbuka agano lake milele. 6 Amewaonyesha watu wake uwezo wa kazi zake, akiwapa nchi za mataifa mengine. 7 Kazi za mikono yake ni za uaminifu na haki, mausia yake yote ni ya kuaminika. 8 Zinadumu milele na milele, zikifanyika kwa uaminifu na unyofu. 9 Aliwapa watu wake ukombozi, aliamuru agano lake milele: jina lake ni takatifu na la kuogopwa. 10 Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima, wote wanaozifuata amri zake wana busara. Sifa zake zadumu milele.

< Zaburi 111 >