< Zaburi 109 >

1 Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, ambaye ninakusifu, usiwe kimya,
Zaburi ya Daudi. Mungu ninaye msifu, usinyamaze kimya.
2 kwa maana watu waovu na wadanganyifu wamefungua vinywa vyao dhidi yangu; wasema dhidi yangu kwa ndimi za udanganyifu.
Kwa maana waovu na wadanganyifu wananishambulia; wanazungumza uongo dhidi yangu.
3 Wamenizunguka kwa maneno ya chuki, wananishambulia bila sababu.
Wananizunguka na kusema mambo ya chuki, na wananishambulia bila sababu.
4 Wanachonilipa badala ya urafiki wangu ni kunishtaki, lakini mimi ninawaombea.
Wananilipa kashfa badala ya upendo, lakini mimi ninawaombea.
5 Wananilipiza mabaya kwa mema, chuki badala ya urafiki wangu.
Wananilipa uovu badala ya mema, na wanachukia upendo wangu.
6 Agiza mtu mwovu ampinge, mshtaki asimame mkono wake wa kuume.
Teua mtu mwovu aliye adui zaidi kama watu hawa; teua mshitaki asimame mkono wake wa kuume.
7 Anapohukumiwa, apatikane na hatia, nayo maombi yake yamhukumu.
Na atakapohukumiwa, aonekane na hatia; maombi yake yachukuliwe kuwa ni dhambi.
8 Siku zake za kuishi na ziwe chache, nafasi yake ya uongozi ichukuliwe na mtu mwingine.
Siku zake na ziwe chahe; mamlaka yake na yachukuliwe na mtu mwingine.
9 Watoto wake na waachwe yatima, mke wake na awe mjane.
Watoto wake wawe yatima, na mke wake awe mjane.
10 Watoto wake na watangetange wakiomba, na wafukuzwe kwenye magofu ya nyumba zao.
Watoto wake wenye kutanga tanga na kuombaomba, wakiondoka katika nyumba zao zilizo haribika na kuomba chakula au pesa kwa wapita njia.
11 Mtu anayemdai na ateke vyote alivyo navyo, matunda ya kazi yake yatekwe nyara na wageni.
Mdai na achukue vitu vyake vyote amilikivyo; wageni wateke mapato ya kazi yake.
12 Asiwepo mtu yeyote wa kumtendea mema wala wa kuwahurumia yatima wake.
Asiwepo mtu yeyote wa kumfanyia wema; mtu yeyote asiwahurumie yatima wake.
13 Uzao wake na ukatiliwe mbali, majina yao yafutike katika kizazi kifuatacho.
Watoto wake waangamizwe; majina yao na yafutwe katika kizazi kijacho.
14 Maovu ya baba zake na yakumbukwe mbele za Bwana, dhambi ya mama yake isifutwe kamwe.
Uovu wa baba zake utajwe kwa Yahwe; na dhambi ya mama yake isisahaulike.
15 Dhambi zao na zibaki daima mbele za Bwana, ili apate kukatilia mbali kumbukumbu lao duniani.
Hatia zao na ziwe mbele ya Yahwe siku zote; Yahwe na aiondoe kumbukumbu yao duniani.
16 Kwa maana kamwe hakuweza kutenda wema, bali alimfukuza mnyonge na mhitaji, aliwafanyia jeuri wahitaji na waliovunjika moyo.
Yahwe na afanye hivi kwa sababu mtu huyu kamwe hakusumbuka kuonesha uaminifu wa agano wowote, lakini badala yake aliwasumbua wanyonge, wahitaji, na kuwaua walio vunjika moyo.
17 Alipenda kulaani, nayo laana ikampata; hakupenda kubariki, kwa hiyo baraka na ikae mbali naye.
Alipenda kulaani; na imrudie juu yake. Alichukia kubariki; baraka zozote na zisije kwake.
18 Alivaa kulaani kama vazi lake, nayo laana ikamwingia mwilini mwake kama maji, kwenye mifupa yake kama mafuta.
Alijivika kulaani kana kwamba ni vazi lake, na laana yake iliingia ndani yake kama maji, na kama mafuta mifupani mwake.
19 Na iwe kama joho alilozungushiwa, kama mshipi aliofungiwa daima.
Laana zake na ziwe kwake kama vazi avaalo kujifunika mwenyewe, na kama mkanda avaao kila siku.
20 Haya na yawe malipo ya Bwana kwa washtaki wangu, kwa wale wanaoninenea mabaya.
Na haya yawe malipo ya mshitaki wangu kutoka kwa Yahwe, ya wale wasemao mambo maovu juu yangu.
21 Lakini wewe, Ee Bwana Mwenyezi, unitendee wema kwa ajili ya jina lako, uniokoe kwa wema wa pendo lako.
Yahwe Bwana wangu, unishughulikie kwa wema kwa ajili ya jina lako. Kwa sababu uaminifu wa agano lako ni mwema, uniokoe.
22 Maana mimi ni maskini na mhitaji, moyo wangu umejeruhiwa ndani yangu.
Kwa maana ni mnyonge na muhitaji, na moyo wangu umejeruhiwa ndani yangu.
23 Ninafifia kama kivuli cha jioni, nimerushwa-rushwa kama nzige.
Ninatoweka kama kivuli cha jioni; ninapeperushwa kama nzige.
24 Magoti yangu yamelegea kwa kufunga, mwili wangu umedhoofika na kukonda.
Magoti yangu ni dhaifu kutokana na kufunga; ninakuwa mwembamba na mifupa.
25 Nimekuwa kitu cha kudharauliwa kwa washtaki wangu, wanionapo, hutikisa vichwa vyao.
Nimedharauliwa na washitaki wangu; wanionapo; hutikisa vichwa vyao.
26 Ee Bwana, Mungu wangu nisaidie, niokoe sawasawa na upendo wako.
Nisaidie, Yahwe Mungu wangu; uniokoe kwa uaminifu wa agano lako.
27 Watu na wafahamu kuwa ni mkono wako, kwamba wewe, Ee Bwana, umetenda hili.
Nao wajue kuwa wewe umefanya haya, kwamba wewe, Yahwe, umetenda haya.
28 Wanaweza kulaani, lakini wewe utabariki, watakaposhambulia wataaibishwa, lakini mtumishi wako atashangilia.
Ingawa wananilaani, tafadhali unibariki; wanishambuliapo, waaibishwe, lakini mtumishi wako afurahi.
29 Washtaki wangu watavikwa fedheha, na kufunikwa na aibu kama joho.
Washitaki wangu na wavishwe kwa aibu; wavae aibu yao kama vazi.
30 Kwa kinywa changu nitamtukuza sana Bwana, katika umati mkubwa nitamsifu.
Kwa kinywa changu ninatoa shukrani kuu kwa Yahwe; nitamsifu yeye katikati ya kusanyiko.
31 Kwa maana husimama mkono wa kuume wa mhitaji, kuokoa maisha yake kutoka kwa wale wanaomhukumu.
Maana nitasimama mkono wa kuume wa mhitaji, ili nimuokoe dhidi ya wale wanao muhukumu.

< Zaburi 109 >