< Zaburi 108 >
1 Wimbo. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti; nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote.
Ee Mungu, moyo wangu u thabiti; nitaimba, naam, nitaimba sifa pia kwa moyo mkuu.
2 Amka, kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko.
Amka, kinanda na kinubi; nitaamka alfajiri.
3 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, katikati ya mataifa; nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu.
Nitakushukuru wewe, Yahwe, kati ya watu; nitakuimbia sifa kati ya mataifa.
4 Kwa maana upendo wako ni mkuu, ni juu kuliko mbingu; uaminifu wako unazifikia anga.
Kwa maana uaminifu wa agano lako ni mkuu juu ya mbingu; na uaminifu wako wafika mawinguni.
5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, utukufu wako na uenee duniani kote.
Ee Mungu, uinuliwe, juu ya mbingu, na utukufu wako utukuke juu ya nchi.
6 Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume, ili wale uwapendao wapate kuokolewa.
Ili kwamba wale uwapendao waokolewe, utuokoe sisi kwa mkono wako wa kuume na unijibu.
7 Mungu amenena kutoka patakatifu pake: “Nitaigawa Shekemu kwa ushindi na kulipima Bonde la Sukothi.
Mungu ameongea katika utakatifu wake; “Nitashangilia; nitaigawanya Shekemu na nitalipima bonde la Sukothi.
8 Gileadi ni yangu, Manase ni yangu, Efraimu ni kofia yangu ya chuma, nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala.
Gileadi ni yangu, na manase ni yangu; Ephraimu ni nguvu ya kichwa changu; Yuda ni fimbo yangu ya kifalme.
9 Moabu ni sinia langu la kunawia, juu ya Edomu natupa kiatu changu; nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”
Moabu ni bakuli langu la kunawia; nitatupa kiatu changu juu ya Edomu; nitapaza sauti katika ushindi kwa ajili ya Filisti.
10 Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome? Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?
Ni nani atakaye nipeleka kwenye mji imara? Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu?”
11 Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi, na hutoki tena na majeshi yetu?
Ee Mungu, sio wewe uliyetukataa? Hauendi vitani na jeshi letu.
12 Tuletee msaada dhidi ya adui, kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.
Utupe msaada dhidi ya adui yetu, maana msaada wa wanadamu ni bure.
13 Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi, naye atawaponda adui zetu.
Tutashinda kwa msaada wa Mungu; atawakanyaga kwa adui zetu.