< Zaburi 107 >

1 Mshukuruni Bwana, kwa kuwa yeye ni mwema, upendo wake wadumu milele.
Mshukuruni Yahwe, maana ni mwema, na uaminifu wa agano lake wadumu milele.
2 Waliokombolewa wa Bwana na waseme hivi, wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui,
Waseme hivi waliokombolewa na Yahwe, wale aliowaokoa toka mkononi mwa adui.
3 wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali, kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini.
Yeye amewakusanya kutoka nchi za kigeni, kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini.
4 Baadhi yao walitangatanga jangwani, hawakuona njia ya kuwafikisha mji ambao wangeweza kuishi.
Walitanga-tanga janwani katika njia ya nyika hawakuona mji wa kuishi.
5 Walikuwa na njaa na kiu, nafsi zao zikadhoofika.
Kwa sababu walikuwa na njaa na kiu, walikata tamaa kutokana na uchovu.
6 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao.
Kisha walimuita Yahwe katika shida yao, naye aliwaokoa toka katika dhiki yao.
7 Akawaongoza kwa njia iliyo sawa hadi mji ambao wangeweza kuishi.
Aliwaongoza kupitia njia ya moja kwa moja waweze kwenda mjini kuishi humo.
8 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,
Oh ili watu wamsifu Yahwe kwa ajili ya uaminifu wa agano lake na kwa mambo ya ajabu aliowatendea wanadamu!
9 kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu, na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema.
Maana hutosheleza shauku za walio na kiu, na hamu ya wale wenye njaa yeye huwashibisha kwa mambo mema.
10 Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu, wafungwa wakiteseka katika minyororo,
Baadhi walikaa katika giza na uvuli wa mauti, walifungwa katika mateso na minyororo.
11 kwa sababu walikuwa wameasi dhidi ya maneno ya Mungu na kudharau shauri la Aliye Juu Sana.
Hii ni kwa sababu walikuwa wameliasi neno la Mungu na walikataa maelekezo ya Aliye Juu.
12 Aliwatumikisha kwa kazi ngumu; walijikwaa na hapakuwepo yeyote wa kuwasaidia.
Aliinyenyekesha mioyo yao kupitia magumu; walipata mashaka na hakukuwa na mmoja wa kuwasaidia.
13 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao.
Kisha wakamwita Yahwe katika shida yao, naye akawatoa katika dhiki yao.
14 Akawatoa katika giza na huzuni kuu na akavunja minyororo yao.
Aliwatoa gizani na kwenye uvuli wa mauti na kuvunja vifungo vyao.
15 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,
Oh ili watu wamsifu Yahwe kwa ajili ya uaminifu wa agano lake na kwa mambo ya ajabu aliyoyatenda kwa wanadamu!
16 kwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba na kukata mapingo ya chuma.
Kwa maana amevunja malango ya shaba na kukata mapingo ya chuma.
17 Wengine wakawa wapumbavu kutokana na uasi wao, wakapata mateso kwa sababu ya uovu wao.
Walikuwa wapumbavu katika njia zao za uasi na kuteswa kwa sababu ya dhambi zao.
18 Wakachukia kabisa vyakula vyote, wakakaribia malango ya mauti.
Walipoteza hamu yao ya kula chakula chochote, na waliyakaribia malango ya kifo.
19 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao.
Kisha walimlilia Yahwe katika shida yao, naye akawatoa katika dhiki yao.
20 Akalituma neno lake na kuwaponya, akawaokoa kutoka maangamizo yao.
Alituma neno lake na likawaponya, na akawaokoa kutoka katika uharibifu wao.
21 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.
Oh ili watu wamsifu Yahwe kwa ajili ya uaminifu wa agano lake na kwa mambo ya ajabu aliyoyatenda kwa wanadamu!
22 Na watoe dhabihu za kushukuru, na wasimulie matendo yake kwa nyimbo za furaha.
Na watoe dhabihu ya shukrani na kutangaza matendo yake kwa kuimba.
23 Wengine walisafiri baharini kwa meli, walikuwa wafanyabiashara kwenye maji makuu.
Baadhi husafiri baharini katika meli na kufanya biashara juu ya bahari.
24 Waliziona kazi za Bwana, matendo yake ya ajabu kilindini.
Hawa huona matendo ya Yahwe na maajabu yake baharini.
25 Kwa maana alisema na kuamsha tufani iliyoinua mawimbi juu.
Kwa maana aliamuru na alivumisha upepo wa dhoruba ambao uliyainua juu mawimbi ya baharini.
26 Yakainuka juu mbinguni, yakashuka chini hadi vilindini, katika hatari hii ujasiri wao uliyeyuka.
Walipanda juu mawinguni na kushuka vilindini. Nafsi zao ziliyeyuka katika dhiki.
27 Walipepesuka na kuyumbayumba kama walevi, ujanja wao ukafikia ukomo.
Waliyumba-yumba na kupepesuka kama walevi na hawakujua la kufanya.
28 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao, naye akawatoa kwenye taabu yao.
Kisha walimlilia Yahwe katika shida yao, naye akawatoa katika dhiki yao.
29 Akatuliza dhoruba kwa mnongʼono, mawimbi ya bahari yakatulia.
Aliituliza dhoruba, na mawimbi yakatulia.
30 Walifurahi ilipokuwa shwari, naye akawaongoza hadi bandari waliyoitamani.
Ndipo walifurahia kwa sababu bahari ilikuwa shwali, na aliwaleta kwenye bandari waliyoitamani.
31 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu.
Oh, ili watu wamsifu Yahwe kwa ajili ya uaminifu wa agano lake na kwa mambo ya ajabu aliyowatendea wanadamu!
32 Na wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu, na wamsifu katika baraza la wazee.
Wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu na wamsifu yeye katika baraza la viongozi.
33 Yeye aligeuza mito kuwa jangwa, chemchemi za maji zitiririkazo kuwa ardhi yenye kiu,
Aligeuza mito ikwa jangwa, chemchem ya maji ikawa nchi kame,
34 nchi izaayo ikawa ya chumvi isiyofaa, kwa sababu ya uovu wa wale walioishi humo.
na nchi ya matunda mengi ikawa nchi isiyozaa kwa sababu ya uovu wa watu wake.
35 Aligeuza jangwa likawa madimbwi ya maji, nayo ardhi kame kuwa chemchemi za maji zitiririkazo;
Aligeuza jangwa likawa ziwa la maji na nchi kame ikawa chemchem ya maji.
36 aliwaleta wenye njaa wakaishi humo, nao wakajenga mji wangeweza kuishi.
Aliwakalisha huko wenye njaa, nao walijenga mji na kuishi humo.
37 Walilima mashamba na kupanda mizabibu, nayo ikazaa matunda mengi,
Walijenga mji ili kupanda mimea shambani, kupanda mizabibu, na kuleta humo mazao tele.
38 Mungu aliwabariki, hesabu yao ikaongezeka sana, wala hakuruhusu mifugo yao kupungua.
Yeye huwabariki wameongezeka sana katika hesabu. Haachi mifugo yao ipungue katika hesabu.
39 Kisha hesabu yao ilipungua, na walinyenyekeshwa kwa kuonewa, maafa na huzuni.
Kisha wakapungua na kudhilika kwa dhiki na mateso.
40 Yeye ambaye huwamwagia dharau wakuu, aliwafanya watangetange nyikani isiyo na njia.
Akawamwagia viongozi dharau na akawafanya wazunguke katika jangwa, mahali pasipo na njia.
41 Lakini yeye aliwainua wahitaji katika taabu zao, na kuongeza jamaa zao kama makundi ya kondoo.
Lakini aliwalinda wahitaji dhidi ya mateso na kujali kwa ajili ya familia yake kama kundi la kondoo.
42 Wanyofu wataona na kufurahi, lakini waovu wote watafunga vinywa vyao.
Wenye haki wataona hili na kufurahi, na uovu wote utaona na kufunga kinya chake.
43 Yeyote aliye na hekima, ayasikie mambo haya, na atafakari upendo mkuu wa Bwana.
Yeyote mwenye hekima anapaswa kuyaangalia haya na kutafakari juu ya matendo ya uaminifu wa agano la Yahwe.

< Zaburi 107 >