< Zaburi 105 >
1 Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake, wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.
2 Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa, waambieni matendo yake yote ya ajabu.
3 Lishangilieni jina lake takatifu, mioyo ya wale wamtafutao Bwana na ifurahi.
4 Mtafuteni Bwana na nguvu zake, utafuteni uso wake siku zote.
5 Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya, miujiza yake na hukumu alizozitamka,
6 enyi wazao wa Abrahamu mtumishi wake, enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
7 Yeye ndiye Bwana Mungu wetu, hukumu zake zimo duniani pote.
8 Hulikumbuka agano lake milele, neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,
9 agano alilolifanya na Abrahamu, kiapo alichomwapia Isaki.
10 Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri, kwa Israeli liwe agano la milele:
11 “Nitakupa wewe nchi ya Kanaani kuwa sehemu utakayoirithi.”
12 Walipokuwa wachache kwa idadi, wachache sana na wageni ndani yake,
13 walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine, kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.
14 Hakuruhusu mtu yeyote awaonee; kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema:
15 “Msiwaguse niliowatia mafuta; msiwadhuru manabii wangu.”
16 Akaiita njaa juu ya nchi na kuharibu chakula chao chote,
17 naye akatuma mtu mbele yao, Yosefu, aliyeuzwa kama mtumwa.
18 Walichubua miguu yake kwa minyororo, shingo yake ilifungwa kwa chuma,
19 hadi yale aliyotangulia kusema yalipotimia, hadi neno la Bwana lilipomthibitisha.
20 Mfalme alituma watu wakamfungua, mtawala wa watu alimwachia huru.
21 Alimfanya mkuu wa nyumba yake, mtawala juu ya vyote alivyokuwa navyo,
22 kuwaelekeza wakuu wa mfalme apendavyo na kuwafundisha wazee wake hekima.
23 Kisha Israeli akaingia Misri, Yakobo akaishi kama mgeni katika nchi ya Hamu.
24 Bwana aliwafanya watu wake kuzaana sana, akawafanya kuwa wengi sana kuliko adui zao,
25 ndiye aliigeuza mioyo yao iwachukie watu wake, wakatenda hila dhidi ya watumishi wake.
26 Akamtuma Mose mtumishi wake, pamoja na Aroni, aliyemchagua.
27 Walifanya ishara zake za ajabu miongoni mwao, miujiza yake katika nchi ya Hamu.
28 Alituma giza na nchi ikajaa giza, kwani si walikuwa wameyaasi maneno yake?
29 Aligeuza maji yao kuwa damu, ikasababisha samaki wao kufa.
30 Nchi yao ilijaa vyura tele, ambao waliingia hadi kwenye vyumba vya kulala vya watawala wao.
31 Alisema, yakaja makundi ya mainzi, na viroboto katika nchi yao yote.
32 Alibadilisha mvua yao ikawa mvua ya mawe, yenye umeme wa radi nchini yao yote,
33 akaharibu mizabibu yao na miti ya tini, na akaangamiza miti ya nchi yao.
34 Alisema, nzige wakaja, tunutu wasio na idadi,
35 wakala kila jani katika nchi yao, wakala mazao ya ardhi yao.
36 Kisha akawaua wazaliwa wote wa kwanza katika nchi yao, matunda ya kwanza ya ujana wao wote.
37 Akawatoa Israeli katika nchi wakiwa na fedha na dhahabu nyingi, wala hakuna hata mmoja kutoka kabila zao aliyejikwaa.
38 Misri ilifurahi walipoondoka, kwa sababu hofu ya Israeli ilikuwa imewaangukia.
39 Alitandaza wingu kama kifuniko, na moto kuwamulikia usiku.
40 Waliomba, naye akawaletea kware, akawashibisha kwa mkate wa mbinguni.
41 Alipasua mwamba, maji yakabubujika, yakatiririka jangwani kama mto.
42 Kwa maana alikumbuka ahadi yake takatifu, aliyompa Abrahamu mtumishi wake.
43 Aliwatoa watu wake kwa furaha, wateule wake kwa kelele za shangwe,
44 akawapa nchi za mataifa, wakawa warithi wa mali wengine walikuwa wameitaabikia:
45 alifanya haya ili wayashike mausia yake na kuzitii sheria zake. Msifuni Bwana.