< Zaburi 103 >
1 Zaburi ya Daudi. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Vyote vilivyomo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu.
Nitamsifu Yahwe maisha yangu yote, na vyote vilivyomo ndani yangu, nitalisifu jina lake takatifu.
2 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usisahau wema wake wote,
Maishani mwangu mwote nitamsifu Yahwe, na kukumbuka matendo yake yote mazuri.
3 akusamehe dhambi zako zote, akuponya magonjwa yako yote,
Yeye husamehe dhambi zako zote; huponya magonjwa yako yote.
4 aukomboa uhai wako na kaburi, akuvika taji ya upendo na huruma,
Huukomboa uhai wako dhidi ya uharubifu; hukuvika taji kwa uaminifu wa agano lake na hutenda kwa rehema.
5 atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema, ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.
Huyatosheleza maisha yako kwa mambo mema ili kwamba ujana wako ufanywe upya kama tai.
6 Bwana hutenda haki, naye huwapa hukumu ya haki wote wanaoonewa.
Yahwe hutenda yaliyo haki naye hutenda hukumu ya haki kwa ajili ya wote walio onewa.
7 Alijulisha Mose njia zake, na wana wa Israeli matendo yake.
Alimjulisha Musa njia zake, matendo yake kwa uzao wa Israeli.
8 Bwana ni mwingi wa huruma na mwenye neema; si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo.
Yahwe ni wa huruma na neema; ni mvumilivu; ana agano kuu la uaminifu.
9 Yeye hatalaumu siku zote, wala haweki hasira yake milele,
Hataadhibu siku zote; hakasiriki siku zote.
10 yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu.
Hatushughulikii sisi kama dhambi zetu zinavyostahili au kutulipa kulingana na uhitaji wa dhambi zetu.
11 Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia sana, ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;
Kama mbingu zilivyo juu zaidi ya nchi, ndivyo ulivyo ukuu wa uaminifu wa agano lake kwao wale wanaomcha yeye.
12 kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi.
Kama vile mashariki ilivyo mbali na magharibi, hivi ndivyo ameondoa hatia zetu za dhambi zetu mbali nasi.
13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake, ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;
Kama vile baba alivyo na huruma kwa watoto wake, ndivyo Yahwe alivyo na huruma kwao wamchao.
14 kwa kuwa anajua tulivyoumbwa, anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.
Maana anajua tulivyo umbwa; anajua kuwa tu mavumbi.
15 Kuhusu mwanadamu, siku zake ni kama majani, anachanua kama ua la shambani;
Kama ilivyo kwa mwanadamu, siku zake ni kama majani; hustawi kama ua katika shamba.
16 upepo huvuma juu yake nalo hutoweka, mahali pake hapalikumbuki tena.
Upepo hulipiga, nalo hutoweka, na hakuna hata mmoja awezaye kuelezea mahali lilipokua.
17 Lakini kutoka milele hata milele upendo wa Bwana uko kwa wale wamchao, nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao:
Lakini agano la uaminifu wa Yahwe uko kwa wale wamchao yeye milele hata milele. Haki yake ni endelevu kwa uzao wao.
18 kwa wale walishikao agano lake na kukumbuka kuyatii mausia yake.
Wanashika agano lake na kukumbuka kutii maagizo yake.
19 Bwana ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni, ufalme wake unatawala juu ya vyote.
Yahwe ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, na ufalme wake watawala juu ya kila mtu.
20 Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, ninyi mlio mashujaa mnaozitii amri zake, ninyi mnaotii neno lake.
Msifuni Yahwe, enyi malaika zake, ninyi hodari wenye nguvu na mtendao neno lake, na kutii sauti ya neno lake.
21 Mhimidini Bwana, ninyi jeshi lake lote la mbinguni, ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake.
Msifuni Yahwe, enyi jeshi la malaika wote, ninyi ni watumishi mfanyao mapenzi yake.
22 Mhimidini Bwana, kazi zake zote kila mahali katika milki yake. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Msifuni Yahwe, viumbe wake wote, mahali popote atawalapo. Nitamsifu Yahwe maisha yangu yote.