< Zaburi 102 >
1 Maombi ya mtu aliyechoka. Anapoteseka na kumimina malalamiko yake kwa Bwana. Ee Bwana, usikie maombi yangu, kilio changu cha kuomba msaada kikufikie.
2 Usinifiche uso wako ninapokuwa katika shida. Unitegee sikio lako, ninapoita, unijibu kwa upesi.
3 Kwa kuwa siku zangu zinatoweka kama moshi, mifupa yangu inaungua kama kaa la moto.
4 Moyo wangu umefifia na kunyauka kama jani, ninasahau kula chakula changu.
5 Kwa sababu ya kusononeka kwangu kwa uchungu, nimebakia ngozi na mifupa.
6 Nimekuwa kama bundi wa jangwani, kama bundi kwenye magofu.
7 Nilalapo sipati usingizi, nimekuwa kama ndege mpweke kwenye paa la nyumba.
8 Mchana kutwa adui zangu hunidhihaki, wale wanaonizunguka hutumia jina langu kama laana.
9 Ninakula majivu kama chakula changu na nimechanganya kinywaji changu na machozi
10 kwa sababu ya ghadhabu yako kuu, kwa maana umeniinua na kunitupa kando.
11 Siku zangu ni kama kivuli cha jioni, ninanyauka kama jani.
12 Lakini wewe, Ee Bwana, umeketi katika kiti chako cha enzi milele, sifa zako za ukuu zaendelea vizazi vyote.
13 Utainuka na kuihurumia Sayuni, kwa maana ni wakati wa kumwonyesha wema; wakati uliokubalika umewadia.
14 Kwa maana mawe yake ni ya thamani kwa watumishi wako, vumbi lake lenyewe hulionea huruma.
15 Mataifa wataogopa jina la Bwana, wafalme wote wa dunia watauheshimu utukufu wako.
16 Kwa maana Bwana ataijenga tena Sayuni na kutokea katika utukufu wake.
17 Ataitikia maombi ya mtu mkiwa, wala hatadharau hoja yao.
18 Hili na liandikwe kwa ajili ya kizazi kijacho, ili taifa litakaloumbwa baadaye waweze kumsifu Bwana:
19 “Bwana alitazama chini kutoka patakatifu pake palipo juu, kutoka mbinguni alitazama dunia,
20 kusikiliza vilio vya uchungu vya wafungwa na kuwaweka huru wale waliohukumiwa kufa.”
21 Kwa hiyo jina la Bwana latangazwa huko Sayuni na sifa zake katika Yerusalemu,
22 wakati mataifa na falme zitakapokusanyika ili kumwabudu Bwana.
23 Katika kuishi kwangu alivunja nguvu zangu, akafupisha siku zangu.
24 Ndipo niliposema: “Ee Mungu wangu, usinichukue katikati ya siku zangu; miaka yako inaendelea vizazi vyote.
25 Hapo mwanzo uliweka misingi ya dunia, nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.
26 Hizi zitatoweka, lakini wewe utadumu, zote zitachakaa kama vazi. Utazibadilisha kama nguo nazo zitaondoshwa.
27 Lakini wewe, U yeye yule, nayo miaka yako haikomi kamwe.
28 Watoto wa watumishi wako wataishi mbele zako; wazao wao wataimarishwa mbele zako.”