< Mithali 9 >
1 Hekima amejenga nyumba yake; amechonga nguzo zake saba.
2 Ameandaa nyama na kuchanganya divai yake; pia ameandaa meza yake.
3 Amewatuma watumishi wake wa kike, naye huita kutoka mahali pa juu sana pa mji.
4 Anawaambia wale wasio na akili, “Wote ambao ni wajinga na waje hapa!
5 Njooni, mle chakula changu na mnywe divai niliyoichanganya.
6 Acheni njia zenu za ujinga nanyi mtaishi; tembeeni katika njia ya ufahamu.
7 “Yeyote anayemkosoa mwenye mzaha hukaribisha matukano; yeyote anayekemea mtu mwovu hupatwa na matusi.
8 Usimkemee mwenye mzaha la sivyo atakuchukia; mkemee mwenye hekima naye atakupenda.
9 Mfundishe mtu mwenye hekima naye atakuwa na hekima zaidi; mfundishe mtu mwadilifu naye atazidi kufundishika.
10 “Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima, na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu.
11 Kwa maana kwa msaada wangu siku zako zitakuwa nyingi, na miaka itaongezwa katika maisha yako.
12 Kama wewe una hekima, hekima yako itakupa tuzo; kama wewe ni mtu wa mzaha, wewe mwenyewe ndiwe utateseka.”
13 Mwanamke aitwaye Mpumbavu ana kelele; hana adabu na hana maarifa.
14 Huketi kwenye mlango wa nyumba yake, juu ya kiti katika mahali pa juu sana pa mji,
15 akiita wale wapitao karibu, waendao moja kwa moja kwenye njia yao.
16 Anawaambia wale wasio na akili, “Wote ambao ni wajinga na waje hapa ndani!”
17 “Maji yaliyoibiwa ni matamu; chakula kinacholiwa sirini ni kitamu!”
18 Lakini hawajui hata kidogo kuwa wafu wako humo, kwamba wageni wake huyo mwanamke wako katika vilindi vya kuzimu. (Sheol )