< Mithali 8 >
1 Je, hekima haitani? Je, ufahamu hapazi sauti?
Je hekima haiti? Je ufahamu hapazi sauti yake?
2 Juu ya miinuko karibu na njia, penye njia panda, ndipo asimamapo;
Juu ya kilima kando ya barabara, kwenye njia panda, hekima anasimama.
3 kando ya malango yaelekeayo mjini, kwenye maingilio, hulia kwa sauti kubwa, akisema:
Kando ya njia ya kuingilia mjini, karibu na milango ya mji, anaita kwa sauti.
4 “Ni ninyi wanaume, ninaowaita; ninapaza sauti yangu kwa wanadamu wote.
Watu, ninawaita ninyi na ninapaza sauti yangu kwa wana wa wanadamu.
5 Ninyi ambao ni wajinga, pateni akili; ninyi mlio wapumbavu, pateni ufahamu.
Ninyi wajinga, jifunzeni hekima, na ninyi mnaochukia maarifa, lazima mjipatieni moyo wa ufahamu.
6 Sikilizeni, kwa maana nina mambo muhimu ya kusema; ninafungua midomo yangu kusema lililo sawa.
Sikiliza na mimi nitasema mambo mazuri na nifumbuapo midomo yangu nitaongea haki.
7 Kinywa changu husema lililo kweli, kwa maana midomo yangu huchukia uovu.
Maana kinywa changu hunena uaminifu na midomo yangu huchukia uovu.
8 Maneno yote ya kinywa changu ni haki; hakuna mojawapo lililopotoka wala ukaidi.
Maneno ya kinywa changu yote ni haki; hakuna kilichogeuzwa wala kupotoshwa.
9 Kwa wenye kupambanua yote ni sahihi; hayana kasoro kwa wale wenye maarifa.
Maneno yangu yote yamenyooka kwa yule mwenye kuelewa; maneno yangu ni haki kwa wale wanaotafuta maarifa.
10 Chagua mafundisho yangu badala ya fedha, maarifa badala ya dhahabu safi,
Chagua fundisho langu badala ya fedha na maarifa kuliko dhahabu safi.
11 kwa maana hekima ina thamani kuliko marijani na hakuna chochote unachohitaji kinacholingana naye.
Maana mimi, hekima ni bora kuliko vito; hakuna unachokitamani kinaweza kulinganishwa na mimi.
12 “Mimi hekima, nakaa pamoja na busara; ninamiliki maarifa na busara.
Mimi, hekima, naishi kwa utaratibu, na ninamiliki maarifa na busara.
13 Kumcha Bwana ni kuchukia uovu; ninachukia kiburi na majivuno, tabia mbaya na mazungumzo potovu.
Hofu ya Mungu ni kuchukia uovu- nachukia majivuno na kiburi, njia ya uovu, na kauli iliyopotoka- hivyo ninavichukia.
14 Ushauri na hukumu sahihi ni vyangu; nina ufahamu na nina nguvu.
Ninaushauri mzuri na hekima sahihi; mimi ni busara; nguvu zipo kwangu.
15 Kwa msaada wangu wafalme hutawala na watawala hutunga sheria zilizo za haki,
Kwa njia yangu wafalme hutawala- pia na waungwana, na wote ambao hutawala kwa haki.
16 kwa msaada wangu wakuu hutawala, na wenye vyeo wote watawalao dunia.
Kwa njia yangu wafalme hutawala na waungwana na wote wanaotawala kwa haki.
17 Nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.
Nawapenda wale wanaonipenda, na wale wanaonitafuta kwa bidii, wataniona.
18 Utajiri na heshima viko kwangu, utajiri udumuo na mafanikio.
Kwangu kunautajiri na heshima, utajiri wa kudumu na haki.
19 Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi; kile nitoacho hupita fedha iliyo bora.
Tunda langu ni bora kuliko dhahabu, bora hata kuliko dhahabu safi.
20 Natembea katika njia ya unyofu katika mapito ya haki,
Ninazalisha kilicho bora kuliko fedha safi. Natembea katika njia ya haki,
21 nawapa utajiri wale wanipendao na kuzijaza hazina zao.
katika mapito ambayo huelekea kwenye haki, ili niwape urithi wale wanaonipenda na kuzijaza hazina zao.
22 “Bwana aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, kabla ya matendo yake ya zamani;
Yehova aliniumba tokea mwanzo- mwazoni mwa matendo yake ya nyakati za kale.
23 niliteuliwa tangu milele, tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa.
Tokea enzi za kale niliwekwa katika nafasi- tokea kwanza, tokea mwanzo wa dunia.
24 Wakati hazijakuwepo bahari, nilikwishazaliwa, wakati hazijakuwepo chemchemi zilizojaa maji;
Kabla ya bahari, mimi nilizaliwa- kabla ya kuwepo chemchemi zenye maji tele.
25 kabla milima haijawekwa mahali pake, kabla vilima havijakuwepo, nilikwishazaliwa,
Kabla ya milima na vilima kuwekwa, mimi nilizaliwa.
26 kabla hajaumba dunia wala mashamba yake au vumbi lolote la dunia.
Nilizaliwa kabla ya Yehova hajaiumba dunia wala makonde, hata mavumbi ya kwanza katika dunia.
27 Nilikuwepo alipoziweka mbingu mahali pake, wakati alichora mstari wa upeo wa macho juu ya uso wa kilindi,
Nilikuwepo alipoziimarisha mbingu, wakati alipochora mstari katika sura ya kilindi.
28 wakati aliweka mawingu juu na kuziweka imara chemchemi za bahari,
Nilikuwepo alipoimarisha anga la juu na wakati wa kutengeneza kina cha chemchemi.
29 wakati aliiwekea bahari mpaka wake ili maji yasivunje agizo lake, na wakati aliweka misingi ya dunia.
Nilikuwepo alipotengeneza mipaka ya bahari, ili maji yasisambae kuvuka pale alipoyaamuru, na wakati anaamuru misingi ya dunia sehemu ya kukaa.
30 Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake. Nilijazwa na furaha siku baada ya siku, nikifurahi daima mbele zake,
Nilikuwa kando yake, kama fundistadi mkuu, na mimi nilikuwa furaha yake siku kwa siku, nikifurahi mbele zake daima.
31 nikifurahi katika dunia yake yote nami nikiwafurahia wanadamu.
Nilikuwa nikifurahi katika dunia yake yote na furaha yangu ilikuwa kwa wana wa wanadamu.
32 “Basi sasa wanangu, nisikilizeni; heri wale wanaozishika njia zangu.
Na sasa, wanangu, nisikilizeni, maana wale wazishikao njia zangu watakuwa na furaha.
33 Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima; msiyapuuze.
Sikilizeni fundisho langu na mpate hekima; wala msilipuuze.
34 Heri mtu yule anisikilizaye mimi, akisubiri siku zote malangoni mwangu, akingoja kwenye vizingiti vya mlango wangu.
Anisikilizaye atakuwa na furaha- kila siku akitazama katika malango yangu, akinisubiri pembeni mwa milango ya masikani yangu.
35 Kwa maana yeyote anipataye mimi amepata uzima na kujipatia kibali kutoka kwa Bwana.
Maana yeyote anionaye mimi, anapata uzima, naye atapata kibali kwa Yehova.
36 Lakini yeyote ashindwaye kunipata hujiumiza mwenyewe; na wote wanichukiao mimi hupenda mauti.”
Na yeyote asiyeniona mimi, hujiumiza mwenyewe, wote wanaonichukia hupenda mauti.