< Mithali 6 >

1 Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa jirani yako, ikiwa umeshika mikono kwa kuweka ahadi kwa ajili ya mwingine,
Mwanangu, kama utaweka pesa zako kuwa dhamana kwa mkopo wa jirani yako; kama ukitoa ahadi yako katika mkopo wa mtu usiyemjua,
2 kama umetegwa na ulichosema, umenaswa kwa maneno ya kinywa chako,
basi umejiwekea mtego mwenyewe na umenaswa kwa maneno ya kinywa chako.
3 basi fanya hivi mwanangu, ili ujiweke huru, kwa kuwa umeanguka mikononi mwa jirani yako: Nenda ukajinyenyekeshe kwake; msihi jirani yako!
Mwanagu, ukinaswa kwa maneno yako mwenyewe, fanya haya ili kujiokoa, kwa kuwa umeangukia kwenye mikono ya jirani yako; nenda unyenyekee na ufanye shauri mbele ya jirani yako.
4 Usiruhusu usingizi machoni pako, usiruhusu kope zako zisinzie.
Usiruhusu usingizi katika macho yako wala kope za macho yako kusinzia.
5 Jiweke huru, kama swala mkononi mwa mwindaji, kama ndege kutoka kwenye mtego wa mwindaji.
Jiokoe mwenyewe kama swala kutoka katika mkono wa mwindaji, kama ndege kutoka katika mkono wa mwinda ndege.
6 Ewe mvivu, mwendee mchwa; zitafakari njia zake ukapate hekima!
Wewe mtu mvivu, mwangalie mchwa, zitafakari njia zake ili kupata busara.
7 Kwa maana yeye hana msimamizi, wala mwangalizi, au mtawala,
Hana akida, afisa au mtawala,
8 lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi na hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.
lakini huandaa chakula chake wakati wa joto na wakati wa mavuno huweka hazina ili kula baadaye.
9 Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaamka lini kutoka usingizi wako?
Ewe mtu mvivu, utalala hata lini? Wakati gani utainuka usingizini?”
10 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika:
Lala kidogo, sizia kidogo, kunja mikono kupumzika kidogo” -
11 hivyo umaskini utakuja juu yako kama mnyangʼanyi, na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.
ndipo umasikini wako utakapokujia kama mporaji na uhitaji wako kama askari wa vita.
12 Mtu mbaya sana na mlaghai, ambaye huzungukazunguka na maneno ya upotovu,
Mtu asiyefaa-mtu mwovu- huishi kwa kauli za udanganyifu wake,
13 ambaye anakonyeza kwa jicho lake, anayetoa ishara kwa miguu yake na kuashiria kwa vidole vyake,
akipepesa macho yake, akiashilia kwa miguu yake na kusonta kwa videle vyake.
14 ambaye hupanga ubaya kwa udanganyifu moyoni mwake: daima huchochea fitina.
Hufanya njama za uovu kwa hila ya moyo wake; daima huchochea faraka.
15 Kwa hiyo maafa yatamkumba ghafula; ataangamizwa mara, pasipo msaada.
Kwa hiyo msiba wake utamkumba kwa ghafula, punde atavunjika vibaya wala hatapona.
16 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana, naam, viko saba vilivyo chukizo kwake:
Kuna vitu sita ambavyo Yehova huvichukia, saba ambavyo ni chukizo kwake.
17 macho ya kiburi, ulimi udanganyao, mikono imwagayo damu isiyo na hatia,
Macho ya mtu mwenye kiburi, ulimi wa uongo, mikono inayomwaga damu ya watu maasumu,
18 moyo uwazao mipango miovu, miguu iliyo myepesi kukimbilia uovu,
moyo unaobuni njama mbaya, miguu inayokimbilia maovu upesi,
19 shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo, na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.
shahidi asemaye uongo na apandaye faraka kati ya ndugu.
20 Mwanangu, zishike amri za baba yako, wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
Mwanangu, itii amri ya baba yako na wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
21 Yafunge katika moyo wako daima, yakaze kuizunguka shingo yako.
Uyafunge katika moyo wako siku zote; yafunge kwenye shingo yako.
22 Wakati utembeapo, yatakuongoza; wakati ulalapo, yatakulinda; wakati uamkapo, yatazungumza nawe.
utembeapo, yatakuongoza; ulalapo yatakulinda, na uamkapo yatakufundisha.
23 Kwa maana amri hizi ni taa, mafundisho haya ni mwanga na maonyo ya maadili ni njia ya uzima,
Maana amri ni taa, na mafundisho ni nuru; kinga za kuadilisha za njia ya uzima.
24 yakikulinda na mwanamke aliyepotoka, kutokana na maneno laini ya mwanamke aliyepotoka.
Yanakulinda dhidi ya mwanamke malaya, dhidi ya maneno laini ya uzinzi.
25 Moyo wako usitamani uzuri wake wala macho yake yasikuteke,
Moyoni mwako usiutamani uzuri wake wala usitekwe katika kope zake.
26 kwa maana kahaba atakufanya uwe maskini, hata ukose kipande cha mkate, naye mwanamke mzinzi huwinda maisha yako hasa.
Kulala na malaya inaweza kugharimu bei ya kipande cha mkate, lakini mke wa mtu mwingine inagharimu uzima wako wote.
27 Je, mtu aweza kuchotea moto kwenye paja lake bila nguo zake kuungua?
Je mtu anaweza kubeba moto katika kifua chake bila kuuguza mavazi yake?
28 Je, mtu aweza kutembea juu ya makaa ya moto yanayowaka bila miguu yake kuungua?
Je mtu anaweza kutembea juu ya makaa bila kuchomwa miguu yake?
29 Ndivyo alivyo mtu alalaye na mke wa mwanaume mwingine; hakuna yeyote amgusaye huyo mwanamke ambaye hataadhibiwa.
Ndivyo alivyo mtu alalaye na mke wa jirani yake; yule alalaye na huyo mke hatakosa adhabu.
30 Watu hawamdharau mwizi kama akiiba kukidhi njaa yake wakati ana njaa.
Watu hawawezi kumdharau mwizi kama anaiba ili kukidhi hitaji lake la njaa.
31 Pamoja na hayo, kama akikamatwa, lazima alipe mara saba, ingawa inamgharimu utajiri wote wa nyumba yake.
Walakini akimatwa, atalipa mara saba ya kile alichoiba; lazima atoe kila kitu cha thamani katika nyumba yake.
32 Lakini mwanaume aziniye na mwanamke hana akili kabisa; yeyote afanyaye hivyo hujiangamiza mwenyewe.
Mtu anayefanya uzinzi hana akili; hufanya hiyo kwa uharibifu wake mwenyewe.
33 Mapigo na aibu ni fungu lake na aibu yake haitafutika kamwe;
Anasitahili aibu na majeraha na fedheha yake haiwezi kuondolewa.
34 kwa maana wivu huamsha ghadhabu ya mume, naye hataonyesha huruma alipizapo kisasi.
Maana vivu humghadhibisha mtu; hatakuwa na huruma wakati wa kulipa kisasi chake.
35 Hatakubali fidia yoyote; atakataa malipo, hata yakiwa makubwa kiasi gani.
Ujapompa zawadi nyingi, hatakubali mbadala wa kusuruhishwa wala kulipwa.

< Mithali 6 >