< Mithali 4 >
1 Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba yenu; sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu.
Wanangu, sikilizeni, fundisho la baba, na zingatieni ili mjue maana ya ufahamu.
2 Ninawapa mafundisho ya maana, kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu.
Mimi ninawapa mafundisho mazuri; msiyaache mafundisho yangu.
3 Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu, ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu,
Mimi nilikuwa mwana kwa baba yangu, mpole na mtoto pekee kwa mama yangu,
4 baba alinifundisha akisema, “Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote; yashike maagizo yangu na wewe utaishi.
baba alinifundisha akiniambia, “Moyo wako uzingatie sana maneno yangu; shika amri zangu nawe uishi.
5 Pata hekima, pata ufahamu; usiyasahau maneno yangu wala usiyaache.
Jipatie hekima na ufahamu; usisahau na kuyakataa maneno ya kinywa changu;
6 Usimwache hekima naye atakuweka salama; mpende, naye atakulinda.
usiiache hekima nayo itakulinda; ipenda nayo itakuhifadhi salama.
7 Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima. Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu.
Hekima ni kitu cha muhimu sana, hivyo jipatie hekima na tumia namna zote kuweza kupata ufahamu.
8 Mstahi, naye atakukweza; mkumbatie, naye atakuheshimu.
Tunza hekima nayo itakutukuza; ikumbatie nayo itakuheshimu.
9 Atakuvika shada la neema kichwani mwako na kukupa taji ya utukufu.”
Hekima itaweka kilemba cha heshima juu ya kichwa chako; itakupa taji zuri.
10 Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia, nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi.
Mwanangu, sikiliza, na kuzingatia maneno yangu, nawe utapata miaka mingi ya maisha yako.
11 Ninakuongoza katika njia ya hekima na kukuongoza katika mapito yaliyonyooka.
Ninakuelekeza katika njia ya hekima, nimekuongoza katika mapito yaliyonyooka.
12 Utembeapo, hatua zako hazitazuiliwa; ukimbiapo, hutajikwaa.
Unapotembea, hakuna atakayesimama katika njia yako na kama ukikimbia hutajikwaa.
13 Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike, maana yeye ni uzima wako.
Shika mwongozo wala usiuache, utakuongoza, maana ni uzima wako.
14 Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu wala usitembee katika njia ya watu wabaya.
Usifuate njia ya waovu wala usiende katika njia ya watendao uovu.
15 Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo; achana nayo, na uelekee njia yako.
Jiepushe nayo, usipite katika njia hiyo; geuka na upite njia nyingine.
16 Kwa kuwa hawawezi kulala mpaka watende uovu; wanashindwa hata kusinzia mpaka wamwangushe mtu.
Maana hawawezi kulala mpaka wafanye ubaya na hupotewa na usingizi hadi wasababishe mtu kujikwaa.
17 Wanakula mkate wa uovu, na kunywa mvinyo wa jeuri.
Maana wao hula mkate wa uovu na hunywa divai ya vurugu.
18 Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko, ambayo hungʼaa zaidi na zaidi mpaka mchana mkamilifu.
Bali njia ya mwenye kutenda haki ni kama mwanga ung'aao, huangaza zaidi na zaidi hadi mchana inapowasili kwa ukamilifu.
19 Lakini njia ya waovu ni kama giza nene; hawajui kinachowafanya wajikwae.
Njia ya waovu ni kama giza - hawajui ni kitu gani huwa wanajikwaa juu yake.
20 Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia; sikiliza kwa makini maneno yangu.
Mwanangu, zingatia maneno yangu; sikiliza kauli zangu.
21 Usiruhusu yaondoke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako;
Usiziache zikaondoka machoni pako; uzitunze katika moyo wako.
22 kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata na afya kwa mwili wote wa mwanadamu.
Maana maneno yangu ni uzima kwa wenye kuyapata na afya katika mwili wao.
23 Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo, maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
Ulinde salama moyo wako na uukinge kwa bidii zote; kwa kuwa katika moyo hububujika chemichemi za uzima.
24 Epusha kinywa chako na ukaidi; weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako.
Jiepushe na kauli za udanganyifu na ujiepushe na mazungumzo ya ufisadi.
25 Macho yako na yatazame mbele, kaza macho yako moja kwa moja mbele yako.
Macho yako yatazame mbele kwa unyoofu na kwa uthabiti tazama mbele sawasawa.
26 Sawazisha mapito ya miguu yako na njia zako zote ziwe zimethibitika.
Usawazishe pito la mguu wako; na njia zako zote zitakuwa salama.
27 Usigeuke kulia wala kushoto; epusha mguu wako na ubaya.
Usigeuke upande wa kulia au kushoto; ondoa mguu wako mbali na uovu.