< Mithali 31 >
1 Misemo ya Mfalme Lemueli, usia wa mama yake aliyomfundisha:
Maneno ya mfalme Lemueli - mausia aliyofundishwa na mama yake.
2 “Ee mwanangu, ee mwana wa tumbo langu, ee mwana wa nadhiri zangu,
Mwanangu nini? Na ni nini mwana wa tumbo langu? Na ni nini mwana wa nadhiri zangu?
3 Usitumie nguvu zako kwa wanawake, uhodari wako kwa wale wanaowaharibu wafalme.
Nguvu zako usiwape wanawake; au wenye kuharibu wafalme njia zako.
4 “Ee Lemueli, haifai wafalme, haifai wafalme kunywa mvinyo, haifai watawala kutamani sana kileo,
Lemueli, kunywa divai, siyo kwa ajili ya wafalme, wala kwa watawala kuuliza, “kileo kikali kiko wapi?”
5 wasije wakanywa na kusahau vile sheria inavyoamuru na kuwanyima haki zao wote walioonewa.
Kwa sababu kama watakunywa, watasahau sheria ni nini, na kupotosha haki za wote walioonewa.
6 Wape kileo wale wanaoangamia, mvinyo wale walio na uchungu,
Wape kileo kikali watu wanaopotea na mvinyo kwa wale wenye kutaabika kwa uchungu.
7 Wanywe na kusahau umaskini wao na wasikumbuke taabu yao tena.
Atakunywa na kusahau umasikini wake na hataikumbuka taabu yake.
8 “Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea, kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa.
Ongea kwa ajili yao wasioweza kuongea, kwa madai ya wote wanaopotea.
9 Sema na uamue kwa haki, tetea haki za maskini na wahitaji.”
Ongea na uhukumu kwa vipimo vya haki na utetee dai la masikini na watu wahitaji.
10 Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata? Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani.
Mke hodari ni nani anaweza kumpata? Thamani yake ni zaidi kuliko vito.
11 Mume wake anamwamini kikamilifu wala hakosi kitu chochote cha thamani.
Moyo wa mume wake humwamini, na hatakuwa masikini.
12 Humtendea mumewe mema, wala si mabaya, siku zote za maisha yake.
Humtendea mambo mema na wala si mabaya siku zote za maisha yake.
13 Huchagua sufu na kitani naye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii.
Huchagua sufu na kitani, na hufanya kazi yake ya mikono kwa furaha.
14 Yeye ni kama meli za biashara akileta chakula chake kutoka mbali.
Yupo kama meli za wafanyabiashara; huleta chakula chake kutoka mbali.
15 Yeye huamka kungali bado giza huwapa jamaa yake chakula na mafungu kwa watumishi wake wa kike.
Huamka wakati wa usiku na kuwapa chakula watu wa kaya yake, na kugawa kazi kwa watumishi wake wa kike.
16 Huangalia shamba na kulinunua, kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu.
Hulifikiria shamba na kulinunua, kwa tunda la mikono yake hupanda shamba la mizabibu.
17 Hufanya kazi zake kwa nguvu, mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake.
Yeye mwenyewe hujivika nguvu na kuimarisha mikono yake.
18 Huona kwamba biashara yake ina faida, wala taa yake haizimiki usiku.
Huangalia ni kipi kitaleta faida nzuri kwake; usiku wote taa yake haizimishwi.
19 Huweka mikono yake kwenye pia, navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi.
Mikono yake huiweka kwenye mpini wa kisokotea nyuzi na hushikilia kisokotea nyuzi.
20 Huwanyooshea maskini mikono yake na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake.
Mkono wake huwafikia watu masikini; mikono yake huwafikia watu wahitaji.
21 Theluji ishukapo, hana hofu kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake, kwa maana wote wamevikwa nguo za kutia joto.
Haogopi theluji kwa ajili ya kaya yake, kwa maana nyumba yake yote imevika kwa nguo nyekundu.
22 Hutengeneza mazulia ya urembo ya kufunika kitanda chake, yeye huvaa kitani safi na urujuani.
Hutengeneza matandiko ya kitanda chake, na huvaa nguo za kitani ya dhambarau safi.
23 Mume wake anaheshimiwa kwenye lango la mji, aketipo miongoni mwa wazee wa nchi.
Mume wake anajulikana malangoni, anapoketi na wazee wa nchi.
24 Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza, naye huwauzia wafanyabiashara mishipi.
Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza, na naleta mishipi kwa wafanyabiashara.
25 Amevikwa nguvu na heshima, anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo.
Amevaa nguvu na heshima, na wakati ujao huucheka.
26 Huzungumza kwa hekima na mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake.
Anafumbua kinywa chake kwa hekima na sheria ya ukarimu ipo kwenye ulimi wake.
27 Huangalia mambo ya nyumbani mwake wala hali chakula cha uvivu.
Huangalia njia za nyumba yake na hawezi kula mkate wa uvivu.
28 Watoto wake huamka na kumwita aliyebarikiwa, mumewe pia humsifu, akisema:
Watoto wake huinuka na kumwita heri na mume wake humsifia, akisema,
29 “Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri, lakini wewe umewapita wote.”
“Wanawake wengi wamefanya vizuri, lakini wewe umewapita wote.”
30 Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu na uzuri unapita upesi, bali mwanamke anayemcha Bwana atasifiwa.
Madaha ni udanganyifu, uzuri ni ubatili; bali mwanamke amchaye Yehova, atasifiwa.
31 Mpe thawabu anayostahili, nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.
Mpeni tunda la mikono yake na kazi zake zimsifu katika malango.