< Mithali 3 >
1 Mwanangu, usisahau mafundisho yangu, bali zitunze amri zangu moyoni mwako,
Mwanangu, usizisahau amri zangu na uyatunze mafundisho yangu katika moyo wako,
2 kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako na kukuletea mafanikio.
maana ziatakuongezea siku zako na miaka ya maisha yako na amani.
3 Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe; vifunge shingoni mwako, viandike katika ubao wa moyo wako.
Usiache utiifu wa agano na uaminifu viondoke kwako, vifunge katika shingo yako, viandike katika vibao vya moyo wako.
4 Ndipo utapata kibali na jina zuri mbele za Mungu na mwanadamu.
Ndipo utapata kibali na heshima mbele Mungu na wanadamu.
5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
Mtegemee Yehova kwa moyo wako wote na wala usitegemee ufahamu wako mwenyewe,
6 katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyoosha mapito yako.
katika njia zako zote mkiri Yeye na yeye atayanyosha mapito yako.
7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe; mche Bwana ukajiepushe na uovu.
Usiwe mwenye busara machoni pako mwenyewe; mche Yehova na jiepushe na uovu.
8 Hii itakuletea afya mwilini mwako, na mafuta kwenye mifupa yako.
Itakuponya mwili wako na kukuburudisha mwili wako.
9 Mheshimu Bwana kwa mali zako na kwa malimbuko ya mazao yako yote;
Mheshimu Yehova kwa utajiri wako na kwa malimbuko ya mazao kwa kila unachozalisha,
10 ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika, viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.
na ndipo ghala zako zitajaa na mapipa makubwa yatafurika kwa divai mpya.
11 Mwanangu, usiidharau adhabu ya Bwana na usichukie kukaripiwa naye,
Mwanangu, usidharau kuadibishwa na Yohova na wala usichukie karipio lake,
12 kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao, kama vile baba afanyavyo kwa mwana apendezwaye naye.
maana Yehova huwaadibisha wale wapendao, kama baba anavyoshughulika kwa mtoto wake ampendezaye.
13 Heri mtu yule aonaye hekima, mtu yule apataye ufahamu,
Yeye apataye hekima anafuraha, naye hupata ufahamu.
14 kwa maana hekima ana faida kuliko fedha na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.
Kwani katika hekima unapata manufaa kuliko ukibadilisha kwa fedha na faida yake inafaa zaidi kuliko dhahabu.
15 Hekima ana thamani kuliko marijani; hakuna chochote unachokitamani kinachoweza kulinganishwa naye.
Hekima inathamani zaidi kuliko kito, na hakuna unachokitamani kinaweza kulinganishwa na hekima.
16 Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume; katika mkono wake wa kushoto kuna utajiri na heshima.
Yeye anasiku nyingi katika mkono wake wa kuume; na mkono wake wa kushoto ni utajiri na heshima.
17 Njia zake zinapendeza, mapito yake yote ni amani.
Njia zake ni njia za ukarimu na mapito yake ni amani.
18 Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia; wale wamshikao watabarikiwa.
Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomshikilia, wale wanaomshikilia wanafuraha.
19 Kwa hekima Bwana aliiweka misingi ya dunia, kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake;
Kwa hekima Yehova aliweka msingi wa dunia, kwa ufahamu aliziimarisha mbingu.
20 kwa maarifa yake vilindi viligawanywa, nayo mawingu yanadondosha umande.
Kwa maarifa yake vina vilipasuka na mawingu kudondosha umande wake.
21 Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara, usiache vitoke machoni pako;
Mwanangu, zingatia hukumu ya kweli na ufahamu, na wala usiache kuvitazama.
22 ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako na pambo la neema shingoni mwako.
Vitakuwa uzima wa nafsi yako na urembo wa hisani wa kuvaa shingoni mwako.
23 Kisha utaenda katika njia yako salama, wala mguu wako hautajikwaa;
Ndipo utatembea katika njia yako kwa usalama na mguu wako hautajikwaa;
24 ulalapo, hautaogopa; ulalapo usingizi wako utakuwa mtamu.
ulalapo hutaogopa; utakapolala, usingizi wako utakuwa mtamu.
25 Usiogope maafa ya ghafula au maangamizi yanayowapata waovu,
Usitishwe na hofu ya ghafula au uharibifu uliosababishwa na waovu unapotokea,
26 kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.
kwa maana Yehova utakuwa upande wako na ataulinda mguu wako usinaswe kwenye mtego.
27 Usizuie wema kwa wale wanaostahili ikiwa katika uwezo wako kutenda.
Usizuie mema kwa wale wanaoyastahili, wakati utendaji upo ndani ya mamlaka yako.
28 Usimwambie jirani yako, “Njoo baadaye, nitakupa kesho”: wakati wewe unacho kitu kile karibu nawe.
Jirani yako usimwambie, “Nenda, na uje tena, na kesho nitakupa,” wakati pesa unazo.
29 Usifanye hila ya kumdhuru jirani yako, ambaye anaishi karibu na wewe akikuamini.
Usiweke mpango wa kumdhuru jirani yako- anayeishi jirani nawe na yeye anakuamini.
30 Usimshtaki mtu bila sababu, wakati hajakutenda dhara lolote.
Usishindane na mtu pasipo sababu, ikiwa hajafanya chochote kukudhuru.
31 Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri wala kuchagua njia yake iwayo yote,
Usimhusudu mtu jeuri au kuchagua njia zake zozote.
32 kwa kuwa Bwana humchukia mtu mpotovu, lakini siri yake iko kwa mwenye haki.
Maana mtu mjanja ni chukizo kwa Yehova, bali humleta mtu mwaminifu kwenye tumaini lake.
33 Laana ya Bwana i juu ya nyumba ya mwovu, lakini yeye huibariki nyumba ya mwenye haki.
Laana ya Yehova ipo katika nyumba ya watu waovu, bali huibariki maskani ya watu wenye haki.
34 Huwadhihaki wale wanaodhihaki, lakini huwapa neema wale wanyenyekevu.
Yeye huwadhihaki wenye dhihaka, bali huwapa hisani watu wanyenyekevu.
35 Wenye hekima hurithi heshima, bali huwaaibisha wapumbavu.
Watu wenye busara huirithi heshima, bali wapumbavu huinuliwa kwa fedheha yao wenyewe.