< Mithali 28 >

1 Mtu mwovu hukimbia ingawa hakuna yeyote anayemfukuza, bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
Waovu hukimbia wakati hakuna mtu anayewafukuza, bali wale watendao haki ni thabiti kama simba kijana.
2 Wakati nchi inapokuwa na uasi, inakuwa na viongozi wengi, bali mwenye ufahamu na maarifa hudumisha utaratibu.
Kwa sababu ya uhalifu wa nchi, kuna wakuu wengi, bali kwa mtu mwenye ufahamu na maarifa, itadumu kwa muda mrefu.
3 Mtu maskini amwoneaye yeye aliye maskini zaidi ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza mazao.
Mtu masikini mwenye kukandamiza watu wengine masikini ni kama mvua inayopiga ambayo haisazi chakula.
4 Wale waiachao sheria huwasifu waovu, bali wale waishikao sheria huwapinga.
Wale wanaokataa sheria huwatukuza watu waovu, bali wale wenye kuitunza sheria hupigana dhidi yao.
5 Watu wabaya hawaelewi haki, bali wale wamtafutao Bwana wanaielewa kikamilifu.
Watu wabaya hawafahamu haki, bali wale wanaomtafuta Yehova wanafahamu kila kitu.
6 Afadhali maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama kuliko tajiri ambaye njia zake ni potovu.
Ni bora mtu masikini ambaye anatembea katika uadilifu, kuliko mtu tajiri ambaye ni mdanganyifu katika njia zake.
7 Yeye ashikaye sheria ni mwana mwenye ufahamu, bali rafiki wa walafi humwaibisha baba yake.
Yeye anayetunza sheria ni mwana mwenye ufahamu, bali mwenye ushirika na walafi humwaibisha baba yake.
8 Yeye aongezaye utajiri wake kwa riba kubwa mno hukusanya kwa ajili ya mwingine, ambaye atawahurumia maskini.
Anayepata mafanikio kwa kutoza riba kubwa anakusanya utajiri wake kwa ajili ya mwingine ambaye atakuwa na huruma kwa watu masikini.
9 Kama mtu yeyote akikataa kusikia sheria, hata maombi yake ni chukizo.
Kama mtu atageuzia mbali sikio lake kusikia sheria, hata maombi yake ni chukizo.
10 Yeye ambaye humwongoza mwenye haki kwenye mapito mabaya, ataanguka kwenye mtego wake mwenyewe, bali wasio na lawama watapokea urithi mwema.
Yeye anayempotosha mwenye uadilifu katika njia ya uovu ataangukia kwenye shimo lake mwenyewe, bali wakamilifu watapata urithi mwema.
11 Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe, bali mtu maskini mwenye ufahamu atamfichua.
Mtu tajiri anaweza kuwa mwenye hekima machoni pake mwenyewe, bali mtu masikini mwenye ufahamu atamtafuta.
12 Mwenye haki ashindapo, kuna furaha kubwa, bali waovu watawalapo, watu hujificha.
Kunapokuwa na ushindi kwa wenye kutenda haki, kunafuraha kuu, bali wanapoinuka waovu, watu hujificha wenyewe.
13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.
Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali mwenye kutubu na kuziacha ataonyeshwa rehema.
14 Amebarikiwa mtu ambaye siku zote humcha Bwana, bali yeye afanyaye moyo wake kuwa mgumu huangukia kwenye taabu.
Anafuraha ambaye huishi kwa unyenyekevu, bali anayeufanya moyo wake ataanguka katika taabu.
15 Kama simba angurumaye au dubu ashambuliaye, ndivyo alivyo mtu mwovu atawalaye wanyonge.
Kama simba anayeunguruma au dubu anayeshabulia ni kama mtawala mwovu juu ya watu masikini.
16 Mtawala dhalimu hana akili, bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu atafurahia maisha marefu.
Mtawala anayekosa ufahamu ni mkandamizaji katili, bali mwenye kuchukia aibu atadumu katika siku zake.
17 Mtu mwenye kusumbuliwa na hatia ya kuua atakuwa mtoro mpaka kufa; mtu yeyote na asimsaidie.
Kama mtu anahatia kwa sababu amemwaga damu ya mtu, atakuwa mkimbizi hadi kifo na hakuna atakayemsaidia.
18 Yeye ambaye mwenendo wake hauna lawama hulindwa salama, bali yeye ambaye njia zake ni potovu ataanguka ghafula.
Mwenye kuenenda kwa ukaminifu atakuwa salama, bali mwenye njia ya udanganyifu ataanguka ghafla.
19 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele, bali yule afuataye mambo ya upuzi atakuwa na umaskini wa kumtosha.
Anayefanya kazi kwenye shamba lake atapata chakula kingi, bali afuataye shughuli za upuuzi atapata umasikini mkubwa.
20 Mtu mwaminifu atabarikiwa sana, bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka hataacha kuadhibiwa.
Mtu mwaminifu atapata baraka nyingi bali apataye utajiri wa haraka hawezi kukosa adhabu.
21 Kuonyesha upendeleo si vizuri, hata hivyo mtu atafanya kosa kwa kipande cha mkate.
Siyo vema kuonyesha upendeleo, lakini kwa kipande cha mkate mtu atafanya ubaya.
22 Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri, naye hana habari kuwa umaskini unamngojea.
Mtu mchoyo huharakisha kwenye utajiri, lakini hajui ni umasikini gani utakuja juu yake.
23 Yeye amkemeaye mtu mwishoni hupata kibali zaidi, kuliko mwenye maneno ya kusifu isivyostahili.
Anayemkaripia mtu baadaye atapata fadhila zaidi kutoka kwake kuliko mwenye kumsifia sana kwa ulimi wake.
24 Yeye amwibiaye babaye au mamaye na kusema, “Si kosa,” yeye ni mwenzi wa yule aharibuye.
Yule anayemwibia baba yake na mama yake na kusema, “Hiyo siyo dhambi,” ni mshirika wa mwenye kuharibu.
25 Mtu mwenye tamaa huchochea fitina, bali yule amtegemeaye Bwana atafanikiwa.
Mtu mwenye tamaa huchochea mafarakano, bali anayemtumaini Yehova atafanikiwa.
26 Yeye ajitumainiaye mwenyewe ni mpumbavu, bali yeye atembeaye katika hekima hulindwa salama.
Yule anayeutumaini moyo wake mwenyewe ni mpumbavu, bali anayekwenda kwa hekima atajilinda mbali na hatari.
27 Yeye ampaye maskini hatapungukiwa na kitu chochote, bali yeye awafumbiaye maskini macho hupata laana nyingi.
Mwenye kuwapa masikini hatapungukiwa kitu, bali anayewafumbia macho atapokea laana nyingi.
28 Wakati waovu watawalapo, watu huenda mafichoni, bali waovu wanapoangamia, wenye haki hufanikiwa.
Watu waovu wanapoinuka, watu hujificha wenyewe, lakini watu waovu wataangamia, wale watendao haki wataongezeka.

< Mithali 28 >