< Mithali 28 >
1 Mtu mwovu hukimbia ingawa hakuna yeyote anayemfukuza, bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
2 Wakati nchi inapokuwa na uasi, inakuwa na viongozi wengi, bali mwenye ufahamu na maarifa hudumisha utaratibu.
3 Mtu maskini amwoneaye yeye aliye maskini zaidi ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza mazao.
4 Wale waiachao sheria huwasifu waovu, bali wale waishikao sheria huwapinga.
5 Watu wabaya hawaelewi haki, bali wale wamtafutao Bwana wanaielewa kikamilifu.
6 Afadhali maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama kuliko tajiri ambaye njia zake ni potovu.
7 Yeye ashikaye sheria ni mwana mwenye ufahamu, bali rafiki wa walafi humwaibisha baba yake.
8 Yeye aongezaye utajiri wake kwa riba kubwa mno hukusanya kwa ajili ya mwingine, ambaye atawahurumia maskini.
9 Kama mtu yeyote akikataa kusikia sheria, hata maombi yake ni chukizo.
10 Yeye ambaye humwongoza mwenye haki kwenye mapito mabaya, ataanguka kwenye mtego wake mwenyewe, bali wasio na lawama watapokea urithi mwema.
11 Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe, bali mtu maskini mwenye ufahamu atamfichua.
12 Mwenye haki ashindapo, kuna furaha kubwa, bali waovu watawalapo, watu hujificha.
13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.
14 Amebarikiwa mtu ambaye siku zote humcha Bwana, bali yeye afanyaye moyo wake kuwa mgumu huangukia kwenye taabu.
15 Kama simba angurumaye au dubu ashambuliaye, ndivyo alivyo mtu mwovu atawalaye wanyonge.
16 Mtawala dhalimu hana akili, bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu atafurahia maisha marefu.
17 Mtu mwenye kusumbuliwa na hatia ya kuua atakuwa mtoro mpaka kufa; mtu yeyote na asimsaidie.
18 Yeye ambaye mwenendo wake hauna lawama hulindwa salama, bali yeye ambaye njia zake ni potovu ataanguka ghafula.
19 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele, bali yule afuataye mambo ya upuzi atakuwa na umaskini wa kumtosha.
20 Mtu mwaminifu atabarikiwa sana, bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka hataacha kuadhibiwa.
21 Kuonyesha upendeleo si vizuri, hata hivyo mtu atafanya kosa kwa kipande cha mkate.
22 Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri, naye hana habari kuwa umaskini unamngojea.
23 Yeye amkemeaye mtu mwishoni hupata kibali zaidi, kuliko mwenye maneno ya kusifu isivyostahili.
24 Yeye amwibiaye babaye au mamaye na kusema, “Si kosa,” yeye ni mwenzi wa yule aharibuye.
25 Mtu mwenye tamaa huchochea fitina, bali yule amtegemeaye Bwana atafanikiwa.
26 Yeye ajitumainiaye mwenyewe ni mpumbavu, bali yeye atembeaye katika hekima hulindwa salama.
27 Yeye ampaye maskini hatapungukiwa na kitu chochote, bali yeye awafumbiaye maskini macho hupata laana nyingi.
28 Wakati waovu watawalapo, watu huenda mafichoni, bali waovu wanapoangamia, wenye haki hufanikiwa.