< Mithali 25 >

1 Hizi ni mithali zaidi za Solomoni, zilizonakiliwa na watu wa Hezekia mfalme wa Yuda:
Hizi tena ni mithali za Sulemani, zilinakiliwa na watu wa Hezekia, mfalme wa Yuda.
2 Ni Utukufu wa Mungu kuficha jambo, bali ni utukufu wa wafalme kuchunguza jambo.
Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo, bali utukufu wa wafalme kutafiti juu ya jambo.
3 Kama mbingu zilivyo juu na nchi ilivyo chini, ndivyo ambavyo mioyo ya wafalme haichunguziki.
Kama mbingu ni kwa kimo na dunia ni kwa kina, ndivyo hivyo moyo wa wafalme hauchunguziki.
4 Ondoa takataka kwenye madini ya fedha, nako ndani yake kutatokea chombo cha mfua fedha.
Ondoa takataka kutoka kwenye fedha na mfua vyuma anaweza kutumia fedha katika ufundi wake.
5 Ondoa waovu mbele ya mfalme, nacho kiti chake cha enzi kitaimarishwa kwa njia ya haki.
Pamoja na hayo, waondoe watu waovu mbele ya mfalme na kiti chake cha enzi kitaimarishwa kwa kutenda haki.
6 Usijikweze mwenyewe mbele ya mfalme, wala usidai nafasi miongoni mwa watu wakuu;
Usijitukuze mwenyewe mbele ya mfalme na usisimame katika sehemu iliyoteuliwa kwa watu wakuu.
7 ni afadhali yeye akuambie, “Njoo huku juu,” kuliko yeye kukuaibisha mbele ya mkuu. Kile ulichokiona kwa macho yako
Ni bora yeye akuambie, “Njoo hapa” kuliko wewe kujiaibisha mbele ya mkuu.
8 usiharakishe kukipeleka mahakamani, maana utafanya nini mwishoni kama jirani yako atakuaibisha?
Usiharakishe kufanya kuhukumu, kwa kile ulichokishuhudia. Maana utafanya nini mwishoni, wakati jirani yako atakapokuaibisha?
9 Kama ukifanya shauri na jirani yako, usisaliti siri ya mtu mwingine,
Jitetee kesi yako kati ya jirani yako na wewe na usifunue siri ya mtu mwingine,
10 ama yeye aisikiaye aweza kukuaibisha na kamwe sifa yako mbaya haitaondoka.
au vinginevyo anayekusikia ataleta aibu juu yako na taarifa mbaya juu yako haiwezi kunyamazishwa.
11 Neno lisemwalo kwa wakati ufaao ni kama matunda ya mtofaa ya dhahabu yaliyowekwa kwenye vijalizo vya fedha.
Kunena maneno yenye kuchaguliwa vizuri, ni kama nakshi za dhahabu iliyoungwa kwenye fedha.
12 Kama vile kipuli cha dhahabu au pambo la dhahabu safi, ndivyo lilivyo karipio la mtu mwenye hekima kwa sikio lisikilizalo.
Kama pete ya dhahabu au kito kilichotengenezwa kwa dhahabu safi ndivyo lilivyo karipio la busara kwenye sikio linalosikia.
13 Kama vile ubaridi wa theluji wakati wa mavuno ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wale wamtumao, huburudisha roho za bwana zake.
Kama baridi ya theluji wakati wa mavuno ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wenye kumtuma; huyahifadhi maisha ya mabwana wake.
14 Kama vile mawingu na upepo pasipo mvua ndivyo alivyo mtu ajisifuye kwa zawadi ambazo hatoi.
Kama mawingu na upepo bila mvua ndivyo alivyo mwenye kujisifu kuhusu zawadi asiyoitoa.
15 Kwa njia ya uvumilivu mtawala aweza kushawishiwa, nao ulimi laini waweza kuvunja mfupa.
Kwa uvumilivu mtawala anaweza kushawishiwa na ulimi raini unaweza kuvunja mfupa.
16 Ukipata asali, kula kiasi tu cha kukutosha, ukila zaidi, utatapika.
Kama utapata asali, kula ya kutosha- vingenevyo, ukila nyingi sana, utaitapika.
17 Ingiza mguu wako nyumbani kwa jirani yako mara chache, ukizidisha, atakukinai na atakuchukia.
Usiweke mguu wako kwenye nyumba ya jirani yako mara nyingi, anaweza kuchoshwa nawe na kukuchukia.
18 Kama vile rungu au upanga au mshale mkali ndivyo alivyo mtu atoaye ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake.
Mtu anayetoa ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake ni kama rungu lililotumiwa katika vita, au upanga, au mshale mkali.
19 Kama vile jino bovu au mguu uliolemaa, ndivyo ilivyo kumtegemea mtu asiye mwaminifu wakati wa shida.
Kumtumaini mtu asiye mwaminifu wakati wa taabu ni kama jino bovu au mguu unaoteleza.
20 Kama vile avuaye mavazi siku ya baridi, au kama siki iliyomwagwa juu ya magadi, ndivyo alivyo yeye amuimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito.
Kama mtu anayevua nguo katika hali ya baridi, au kama siki iliyotiwa kwenye magadi, ndivyo alivyo anayeimba wimbo kwa mwenye moyo mzito.
21 Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale; kama ana kiu, mpe maji anywe.
Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale na kama ana kiu, mpe maji ya kunywa,
22 Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake, naye Bwana atakupa thawabu.
maana utamwekea mkaa juu ya kichwa chake na Yehova atakupa thawabu.
23 Kama vile upepo wa kaskazini uletavyo mvua, ndivyo ulimi usingiziao uletavyo uso wa hasira.
Ni hakika upepo wa kaskazini huleta mvua, ndivyo mtu anayesema siri hufanya sura zikasirike.
24 Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.
Ni bora kuishi kwenye pembe ya darini kuliko kuchangia nyumba pamoja na mwanamke mgomvi.
25 Kama vile maji baridi kwa nafsi iliyochoka ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali.
Kama maji ya baridi kwa mwenye kiu, ndivyo ilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali.
26 Kama vile chemchemi iliyotibuliwa matope au kisima kilichotiwa taka ndivyo alivyo mtu mwenye haki akishiriki na waovu.
Kama chemchemi iliyochafuliwa au kisima kilichoharibiwa ndivyo alivyo mtu mwema ambaye huyumbayumba mbele ya watu waovu.
27 Si vyema kula asali nyingi sana, wala si heshima kujitafutia heshima yako mwenyewe.
Si vema kula asali nyingi mno; hivyo ni kama kutafuta heshima baada heshima.
28 Kama vile mji ambao kuta zake zimebomoka ndivyo alivyo mtu ambaye hawezi kujitawala mwenyewe.
Mtu bila kujitawala ni kama mji ulibomolewa na usiokuwa na kuta.

< Mithali 25 >