< Mithali 23 >
1 Uketipo kula chakula na mtawala, angalia vyema kile kilicho mbele yako,
Unapoketi kula pamoja na mtawala, angalia kwa uangalifu kilichopo mbele yako,
2 na utie kisu kooni mwako kama ukiwa mlafi.
na kama ni mtu unayependa kula chakula sana weka kisu kooni.
3 Usitamani vyakula vyake vitamu kwa kuwa chakula hicho ni cha hila.
Usitamani vinono vyake maana ni chakula cha uongo.
4 Usijitaabishe ili kuupata utajiri, uwe na hekima kuonyesha kujizuia.
Usifanye kazi sana ili kupata mali; uwe na busara ya kutosha ili ujue wakati wa kuacha.
5 Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka, huwa kama umepata mabawa ghafula, ukaruka na kutoweka angani kama tai.
Je utaruhusu macho yako yaangaze juu yake? Itaondoka, maana itawaa mabawa kama tai na kuruka angani.
6 Usile chakula cha mtu mchoyo, usitamani vyakula vyake vitamu,
Usile chakula cha yule mwenye jicho baya- na usiwe na shauku ya vinono vyake,
7 kwa maana yeye ni aina ya mtu ambaye kila mara anafikiri juu ya gharama. Anakuambia, “Kula na kunywa,” lakini moyo wake hauko pamoja nawe.
maana ni mtu mwenye kuhesabu gharama ya chakula. “Kula na kunywa!” anakuambia, lakini moyo wake haupo pamoja nawe.
8 Utatapika kile kidogo ulichokula, nawe utakuwa umepoteza bure maneno yako ya kumsifu.
Utatapika kiasi kidogo ulichokula na utakuwa umepoteza sifa zako njema.
9 Usizungumze na mpumbavu, kwa maana atadhihaki hekima ya maneno yako.
Usiongee katika usikivu wa mpumbavu, maana atadharau hekima ya maneno yako.
10 Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani wala kunyemelea kwenye mashamba ya yatima,
Usihamishe jiwe la mpaka wa kale au kunyang'anya mashamba ya yatima,
11 kwa kuwa Mtetezi wao ni mwenye nguvu, atalichukua shauri lao dhidi yako.
maana Mkombozi wao ni imara na atatetea kesi yao dhidi yako.
12 Elekeza moyo wako kwenye mafundisho na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.
Elekeza moyo wako katika mafundisho na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.
13 Usimnyime mtoto adhabu, ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa.
Usizuie kuadilisha mtoto, maana ukimchapa kwa fimbo, hatakufa.
14 Mwadhibu kwa fimbo na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini. (Sheol )
Ni wewe unayepaswa kumchapa kwa fimbo na kuikoa nafsi yake kuzimu. (Sheol )
15 Mwanangu, kama moyo wako una hekima, basi moyo wangu utafurahi,
Mwanangu, kama moyo wako una busara, basi moyo wangu utafurahi pia;
16 utu wangu wa ndani utafurahi, wakati midomo yako itakapozungumza lililo sawa.
sehemu zangu ndani kabisa zitafurahi sana midomo yako inaponena haki.
17 Usiuruhusu moyo wako kuwaonea wivu wenye dhambi, bali kila mara uwe na bidii katika kumcha Bwana.
Usiruhusu moyo wako kuwahusudu wenye dhambi, lakini endelea kumcha Yehova siku zote.
18 Hakika kuna tumaini la baadaye kwa ajili yako, nalo tarajio lako halitakatiliwa mbali.
Hakika tumaini lako halitaondolewa na siku zako za hapo baadaye.
19 Sikiliza, mwanangu na uwe na hekima, weka moyo wako kwenye njia iliyo sawa.
Sikia- wewe! - mwanangu, na uwe mwenye busara na uelekeze moyo wako katika njia.
20 Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo, au wale walao nyama kwa pupa,
Usishirikiane pamoja na walevi, au pamoja na walaji wa nyama walafi,
21 kwa maana walevi na walafi huwa maskini, nako kusinzia huwavika matambara.
maana mlevi na mlafi wanakuwa masikini na usingizi utawavika kwa matambara.
22 Msikilize baba yako, aliyekuzaa, wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.
Msikilize baba yako ambaye alikuzaa na usimdharau mama yako wakati akiwa mzee.
23 Nunua kweli wala usiiuze, pata hekima, adabu na ufahamu.
Inunue kweli, lakini usiiuze; nunua hekima, nidhamu, na ufahamu.
24 Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa, naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.
Baba yake mwenye haki atafurahia sana, na yule amzaaye mtoto mwenye busara atamfurahia.
25 Baba yako na mama yako na wafurahi, mama aliyekuzaa na ashangilie!
Mfurahishe baba yako na mama yako na yule aliyekuzaa afurahie.
26 Mwanangu, nipe moyo wako, macho yako na yafuate njia zangu,
Mwanangu, nipe moyo wako na macho yako yachunguze njia zangu.
27 kwa maana kahaba ni shimo refu na mwanamke mpotovu ni kisima chembamba.
Maana malaya ni shimo refu, na mke wa mume mwingine ni kisima chembamba.
28 Kama mnyangʼanyi, hungojea akivizia, naye huzidisha wasio waaminifu miongoni mwa wanaume.
Anavizia kama mnyang'anyi na huongeza idadi ya wadanganyifu miongoni mwa wanadamu.
29 Ni nani mwenye ole? Ni nani mwenye huzuni? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye malalamiko? Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu? Ni nani mwenye macho mekundu?
Nani mwenye taabu? Nani mwenye huzuni? Nani mwenye mapigano? Nani mwenye malalamiko? Nani mwenye majeraha bila sababu? Nani mwenye macho mekundu?
30 Ni hao wakaao sana kwenye mvinyo, hao waendao kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa.
Ni wale ambao huzengea kwenye mvinyo, wale wanaojaribu kuchanganya mvinyo.
31 Usiukodolee macho mvinyo wakati ukiwa mwekundu, wakati unapometameta kwenye bilauri, wakati ushukapo taratibu!
Usiutazame mvinyo ukiwa mwekundu, wakati unametameta kwenye kikombe na kutelemka kwa uraini.
32 Mwishowe huuma kama nyoka na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu.
Mwisho wake unauma kama nyoka na sumu yake kama kifutu.
33 Macho yako yataona mambo mageni na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka.
Macho yako yataona vitu vigeni na moyo wako utatamka vitu vya ukaidi.
34 Utakuwa kama alalaye katikati ya bahari, alalaye juu ya kamba ya merikebu.
Utakuwa kama anayelala kwenye bahari au anayelala juu ya mlingoti. “
35 Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia! Wamenichapa, lakini sisikii! Nitaamka lini ili nikanywe tena?”
Wamenipiga,” utasema, “lakini sikuumia. Wamenichapa, lakini sikuwa na hisia. Nitaamka lini? Nitatafuta kinywaji kingine.”