< Mithali 22 >
1 Heri kuchagua jina jema kuliko utajiri mwingi, kuheshimiwa ni bora kuliko fedha au dhahabu.
Jina jema huchaguliwa dhidi ya utajiri mwingi na fadhila ni bora kuliko fedha na dhahabu.
2 Tajiri na maskini wanafanana kwa hili: Bwana ni Muumba wao wote.
Watu matajiri na masikini wanafanana katika hili - Yehova ni muumba wao wote.
3 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha, bali mjinga huendelea mbele kama kipofu nayo ikamtesa.
Mtu mwenye hekima huiona taabu na kujificha mwenyewe, bali mjinga huendelea mbele na huumia kwa ajili yake.
4 Unyenyekevu na kumcha Bwana huleta utajiri, heshima na uzima.
Thawabu ya unyenyekevu na kumcha Yehova ni utajiri, heshima na uzima.
5 Katika mapito ya waovu kuna miiba na mitego, bali yeye ailindaye nafsi yake hukaa mbali nayo.
Miiba na mitego hulala katika njia ya wakaidi; yeye anayelinda maisha yake atakuwa mbali navyo.
6 Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea, naye hataiacha hata akiwa mzee.
Mfundishe mtoto njia inayompasa na wakati akiwa mzee hatayaacha mafundisho hayo.
7 Matajiri huwatawala maskini naye akopaye ni mtumwa wa akopeshaye.
Watu matajiri huwatawala watu masikini na mwenye kukopa ni mtumwa wa yule anayekopesha.
8 Yeye aupandaye uovu huvuna taabu, nayo fimbo ya ghadhabu yake itaangamizwa.
Yule anayepanda udhalimu atavuna taabu na fimbo ya hasira yake itanyauka.
9 Mtu mkarimu yeye mwenyewe atabarikiwa kwa kuwa hushiriki chakula chake na maskini.
Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa, maana anashiriki mkate wake pamoja na masikini.
10 Mfukuze mwenye dhihaka, na mvutano utatoweka; ugomvi na matukano vitakoma.
Mfukuze mbali mwenye dhihaka, na ugomvi utaondoka, mashindano na matukano yatakoma.
11 Yeye apendaye moyo safi na yeye ambaye maneno yake ni ya neema, mfalme atakuwa rafiki yake.
Anayependa moyo safi na mwenye maneno ya neema, atakuwa rafiki yake mfalme.
12 Macho ya Bwana hulinda maarifa, bali huyapinga maneno ya asiye mwaminifu.
Macho ya Yehova huyaangalia maarifa, bali huyapindua maneno ya wadanganyifu.
13 Mvivu husema, “Yuko simba nje!” au, “Nitauawa katika mitaa!”
Mtu mvivu husema, “Kuna simba mtaani! Nitauwawa sehemu za njia.”
14 Kinywa cha mwanamke kahaba ni shimo refu; yeye aliye chini ya ghadhabu ya Bwana atatumbukia ndani yake.
Kinywa cha malaya ni shimo lenye kina kirefu; hasira ya Yehova huchochewa dhidi ya yule anayetumbukia ndani yake.
15 Upumbavu umefungwa ndani ya moyo wa mtoto, bali fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali naye.
Upumbavu umefungwa katika moyo wa mtoto, lakini marudi ya fimbo huutoa.
16 Yeye amwoneaye maskini ili kujiongezea mali, naye ampaye tajiri zawadi, wote huwa maskini.
Anayewanyanyasa watu masikini ili kuongeza mali yake, au kuwapa matajiri, atakuwa masikini.
17 Tega sikio na usikie misemo ya wenye hekima, elekeza moyo wako kwenye yale nifundishayo,
Tega sikio lako na usikilize maneno ya wenye busara na utumia moyo wako katika maarifa yangu,
18 kwa maana inapendeza unapoyahifadhi moyoni mwako na kuwa nayo yote tayari midomoni mwako.
maana itakuwa furaha kwako kama utayaweka ndani yako, kama yote yatakuwa katika midomo yako.
19 Ili tumaini lako liwe katika Bwana, hata wewe, ninakufundisha leo.
Basi tumaini lako liwe kwa Yehova, ninayafundisha kwako leo- hata kwako.
20 Je, sijakuandikia misemo thelathini, misemo ya mashauri na maarifa,
Sijakuandikia wewe misemo thelathini ya mafundisho na maarifa,
21 kukufundisha maneno ya kweli na ya kuaminika, ili uweze kutoa majibu sahihi kwake yeye aliyekutuma?
kwa kukufundisha kweli katika maneno haya yenye uaminifu, ili uwe na majibu yenye kutegemewa kwa waliokutuma?
22 Usiwadhulumu maskini kwa sababu ni maskini, wala kumdhulumu mhitaji mahakamani,
Usimwibie masikini kwa sababu ni masikini, au kumponda kwenye lango,
23 kwa sababu Bwana atalichukua shauri lao naye atawateka wao waliowateka.
maana Yehova ataitetea kesi yao, na atawaibia uzima wale waliowaibia masikini.
24 Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira ya haraka, usishirikiane na yule aliye mwepesi kukasirika,
Usifanye urafiki na mtu mwenye kutawaliwa na hasira na wala usiambatane pamoja na mwenye hasira kali,
25 la sivyo utajifunza njia zake na kujiingiza mwenyewe kwenye mtego.
au utajifunza njia zake na utakuwa chambo kwa nafsi yako.
26 Usiwe mwenye kupana mikono katika rehani, au kuweka dhamana kwa ajili ya madeni.
Usiwe miongoni mwao wapigao mikono, mwenye kuahidi madeni.
27 Kama ukikosa njia ya kulipa, kitanda chako kitachukuliwa ukiwa umekilalia.
Kama umekosa njia za kulipa, nini kitaweza kuzuia mtu kuchukua kitanda chako chini yako?
28 Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani lililowekwa na baba zako.
Usiondoe jiwe la mpaka la wahenga ambalo baba zako wameweka.
29 Je, unamwona mtu stadi katika kazi yake? Atahudumu mbele ya wafalme; hatahudumu mbele ya watu duni.
Je umemwona mtu aliyeuwawa kwenye kazi yake? Atasimama mbele ya wafalme; hatasimama mbele ya watu wa kawaida.