< Mithali 20 >

1 Mvinyo ni mdhihaki na kileo ni mgomvi; yeyote apotoshwaye navyo hana hekima.
Divai ni dhihaka na kinywaji kikali ni mgomvi; anayepotea kwa kunywa hana busara.
2 Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; yeye amkasirishaye hupoteza uhai wake.
Kumwogopa mfalme ni kama kumwogopa simba kijana aungurumaye, yeyote anayemkasirisha hutoa fidia ya maish yake.
3 Ni kwa heshima ya mtu kujitenga ugomvi, bali kila mpumbavu ni mwepesi kugombana.
Ni heshima kwa mtu yeyote kujiepusha na mafarakano, bali kila mpumbavu hurukia kwenye mabishano.
4 Mvivu halimi kwa majira; kwa hiyo wakati wa mavuno hutazama lakini hapati chochote.
Mtu mvivu halimi majira ya kipupwe; hutafuta mazao wakati wa mavuno lakini hapati kitu.
5 Makusudi ya moyo wa mwanadamu ni maji yenye kina, lakini mtu mwenye ufahamu huyachota.
Makusudi ndani ya moyo wa mtu ni kama maji yenye kina, bali mtu mwenye ufahamu huyateka.
6 Watu wengi hujidai kuwa na upendo usiokoma, bali mtu mwaminifu ni nani awezaye kumpata?
Mara nyingi mtu husema yeye ni mwaminifu, lakini ni nani awezaye kumpata yule mwaminifu?
7 Mtu mwenye haki huishi maisha yasiyo na lawama, wamebarikiwa watoto wake baada yake.
Mtu atendaye haki hutembea katika uaminifu wake na wana wake wanaofuata baada yake wanafuraha.
8 Wakati mfalme aketipo katika kiti chake cha enzi kuhukumu, hupepeta ubaya wote kwa macho yake.
Mfalme anayeketi kwenye kiti cha hukumu akifanya kazi za kuhukumu hupembua kwa macho yake mabaya yote yaliyoko mbele yake.
9 Ni nani awezaye kusema, “Nimeuweka moyo wangu safi; mimi ni safi na sina dhambi?”
Nani anayeweza kusema, “Nimeuweka safi moyo wangu; nipo huru na dhambi zangu”?
10 Mawe ya kupimia yaliyo tofauti na vipimo tofauti, Bwana huchukia vyote viwili.
Mizani tofauti na vipimo visivyosawa - Yehova huvichukia vyote.
11 Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake, kama tabia yake ni safi na adili.
Hata kijana hujulikana kwa matendo yake, kwa mwenendo wake kama ni safi na uadilifu.
12 Masikio yasikiayo na macho yaonayo, Bwana ndiye alivifanya vyote viwili.
Masikio yanayosikia na macho yanayoona- Yehova aliyafanya yote.
13 Usiupende usingizi la sivyo utakuwa maskini, uwe macho nawe utakuwa na chakula cha akiba.
Usipende usingizi au utakuwa masikini; fumbua macho yako na utakuwa na vyakula tele.
14 “Haifai, haifai!” asema mnunuzi, kisha huondoka akijisifia ununuzi wake.
“Mbaya! Mbaya!” anasema mnunuzi, lakini akiondoka anajisifu.
15 Dhahabu kunayo, na marijani kwa wingi, lakini midomo inenayo maarifa ni kito cha thamani kilicho adimu.
Ipo dhahabu na mawe ya thamani, lakini midomo yenye maarifa ni kito cha thamani.
16 Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo kwa ajili ya mwanamke mpotovu.
Chukua vazi kama mmiliki wake ataweka fedha kama dhamana kwa deni la mgeni, na lichukue kama anaweka dhamana kwa uzinifu.
17 Chakula kilichopatikana kwa hila ni kitamu kwa mwanadamu, bali huishia na kinywa kilichojaa changarawe.
Mkate uliopatikana kwa ulaghai unaladha tamu, lakini baadaye kinywa chake kitajaa kokoto.
18 Fanya mipango kwa kutafuta mashauri, ukipigana vita, tafuta maelekezo.
Mipango huimarishwa kwa ushauri na kwa mwongozo wa busara utapigana vita.
19 Maneno ya kusengenya husababisha kutokuaminika, kwa hiyo mwepuke mtu anayezungumza kupita kiasi.
Mmbea hufunua siri na kwa hiyo hupaswi kushirikiana na watu ambao huongea sana.
20 Ikiwa mtu atamlaani baba yake au mama yake, taa yake itazimwa katika giza nene.
Kama mtu atamlaani baba yake au mama yake, taa yake itapulizwa katikati ya giza.
21 Urithi upatikanao haraka mwanzoni, hautabarikiwa mwishoni.
Urithi uliopatikana mwanzoni kwa haraka utakuwa na mema kidogo mwishoni.
22 Usiseme, “Nitakulipiza kwa ajili ya kosa hili!” Mngojee Bwana, naye atakuokoa.
Usiseme “Mimi nitakulipiza kwa kosa hili” Msubiri Yehova na yeye atakuokoa.
23 Bwana anachukia sana mawe ya kupimia ya udanganyifu, nazo mizani zisizo halali hazimpendezi.
Yehova huchukia mizani isiyo sawa na vipimo vya udanganyifu si vizuri.
24 Hatua za mtu huongozwa na Bwana. Anawezaje basi mtu yeyote kuelewa njia yake mwenyewe?
Hatua za mtu huongozwa na Yehova; namna gani basi ataifahamu njia yake?
25 Ni mtego kwa mtu kuweka wakfu kitu kwa haraka na baada ya kitambo kidogo kufikiria tena nadhiri zake.
Ni mtego kwa mtu kusema kwa pupa, “Kitu hiki ni kitakatifu” na kuanza kufikiri juu yake kwamba kina maana gani baada ya kufanya kiapo.
26 Mfalme mwenye hekima hupepeta waovu, hulipitisha gurudumu la kupuria juu yao.
Mfalme mwenye busara huwapepeta waovu na huligeuza juu yao gurudumu la kupuria.
27 Taa ya Bwana huchunguza roho ya mwanadamu, huchunguza utu wake wa ndani.
Roho ya mtu ni taa ya Yehova, hutafiti sehemu zake zote za ndani kabisa.
28 Upendo na uaminifu humweka mfalme salama, kwa njia ya upendo, kiti chake cha enzi huwa salama.
Agano la uaminifu na udhamini humhifadhi mfalme; kiti chake cha enzi hufanywa thabiti kwa upendo.
29 Utukufu wa vijana ni nguvu zao, mvi ni fahari ya uzee.
Utukufu wa watu vijana ni nguvu zao na fahari ya watu wazee ni mvi zao.
30 Mapigo na majeraha huusafisha ubaya, nayo michapo hutakasa utu wa ndani.
Mapigo yanayoleta kidonda huusafisha ubaya na vichapo hufanya sehemu za ndani kabisa kuwa safi.

< Mithali 20 >