< Mithali 20 >
1 Mvinyo ni mdhihaki na kileo ni mgomvi; yeyote apotoshwaye navyo hana hekima.
2 Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; yeye amkasirishaye hupoteza uhai wake.
3 Ni kwa heshima ya mtu kujitenga ugomvi, bali kila mpumbavu ni mwepesi kugombana.
4 Mvivu halimi kwa majira; kwa hiyo wakati wa mavuno hutazama lakini hapati chochote.
5 Makusudi ya moyo wa mwanadamu ni maji yenye kina, lakini mtu mwenye ufahamu huyachota.
6 Watu wengi hujidai kuwa na upendo usiokoma, bali mtu mwaminifu ni nani awezaye kumpata?
7 Mtu mwenye haki huishi maisha yasiyo na lawama, wamebarikiwa watoto wake baada yake.
8 Wakati mfalme aketipo katika kiti chake cha enzi kuhukumu, hupepeta ubaya wote kwa macho yake.
9 Ni nani awezaye kusema, “Nimeuweka moyo wangu safi; mimi ni safi na sina dhambi?”
10 Mawe ya kupimia yaliyo tofauti na vipimo tofauti, Bwana huchukia vyote viwili.
11 Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake, kama tabia yake ni safi na adili.
12 Masikio yasikiayo na macho yaonayo, Bwana ndiye alivifanya vyote viwili.
13 Usiupende usingizi la sivyo utakuwa maskini, uwe macho nawe utakuwa na chakula cha akiba.
14 “Haifai, haifai!” asema mnunuzi, kisha huondoka akijisifia ununuzi wake.
15 Dhahabu kunayo, na marijani kwa wingi, lakini midomo inenayo maarifa ni kito cha thamani kilicho adimu.
16 Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo kwa ajili ya mwanamke mpotovu.
17 Chakula kilichopatikana kwa hila ni kitamu kwa mwanadamu, bali huishia na kinywa kilichojaa changarawe.
18 Fanya mipango kwa kutafuta mashauri, ukipigana vita, tafuta maelekezo.
19 Maneno ya kusengenya husababisha kutokuaminika, kwa hiyo mwepuke mtu anayezungumza kupita kiasi.
20 Ikiwa mtu atamlaani baba yake au mama yake, taa yake itazimwa katika giza nene.
21 Urithi upatikanao haraka mwanzoni, hautabarikiwa mwishoni.
22 Usiseme, “Nitakulipiza kwa ajili ya kosa hili!” Mngojee Bwana, naye atakuokoa.
23 Bwana anachukia sana mawe ya kupimia ya udanganyifu, nazo mizani zisizo halali hazimpendezi.
24 Hatua za mtu huongozwa na Bwana. Anawezaje basi mtu yeyote kuelewa njia yake mwenyewe?
25 Ni mtego kwa mtu kuweka wakfu kitu kwa haraka na baada ya kitambo kidogo kufikiria tena nadhiri zake.
26 Mfalme mwenye hekima hupepeta waovu, hulipitisha gurudumu la kupuria juu yao.
27 Taa ya Bwana huchunguza roho ya mwanadamu, huchunguza utu wake wa ndani.
28 Upendo na uaminifu humweka mfalme salama, kwa njia ya upendo, kiti chake cha enzi huwa salama.
29 Utukufu wa vijana ni nguvu zao, mvi ni fahari ya uzee.
30 Mapigo na majeraha huusafisha ubaya, nayo michapo hutakasa utu wa ndani.