< Mithali 2 >

1 Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,
Mwanangu, kama ukiyapokea maneno yangu na kuzitunza amri zangu,
2 kutega sikio lako kwenye hekima na kuweka moyo wako katika ufahamu,
usikilize hekima na utaelekeza moyo wako katika ufahamu.
3 na kama ukiita busara na kuita kwa sauti ufahamu,
kama utalilia ufahamu na kupaza sauti yako kwa ajili ya ufahamu,
4 na kama utaitafuta kama fedha na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,
kama utautafuta kama fedha na kupekua ufahamu kama unatafuta hazina iliyojificha,
5 ndipo utakapoelewa kumcha Bwana na kupata maarifa ya Mungu.
ndipo utakapofahamu hofu ya Yehova na utapata maarifa ya Mungu.
6 Kwa maana Bwana hutoa hekima, na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.
Kwa kuwa Yohova hutoa hekima, katika kinywa chake hutoka maarifa na ufahamu.
7 Anahifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu, yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama,
Yeye huhifadhi sauti ya hekima kwa wale wampendezao, yeye ni ngao kwa wale waendao katika uadilifu,
8 kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki na kuhifadhi njia ya waaminifu wake.
huongoza katika njia za haki na atalinda njia ya waaminifu kwake.
9 Ndipo utafahamu lipi lililo kweli na haki na sawa: yaani kila njia nzuri.
Ndipo utakapoelewa wema, haki, usawa na kila njia njema.
10 Kwa maana hekima itaingia moyoni mwako, nayo maarifa yataifurahisha nafsi yako.
Maana hekima itaingia moyoni mwako na maarifa yataipendeza nafsi yako.
11 Busara itakuhifadhi na ufahamu utakulinda.
Busara itakulinda, ufahamu utakuongoza.
12 Hekima itakuokoa kutoka njia za waovu, kutoka kwa watu ambao maneno yao yamepotoka,
Vitakuokoa kutoka katika njia ya uovu, kutoka kwa wale waongeao mambo potovu.
13 wale waachao mapito yaliyonyooka wakatembea katika njia za giza,
Ambao huziacha njia za wema na kutembea katika njia za giza.
14 wale wapendao kutenda mabaya na kufurahia upotovu wa ubaya,
Hufurahia wanapotenda maovu na hupendezwa katika upotovu.
15 ambao mapito yao yamepotoka na ambao ni wapotovu katika njia zao.
Hufuata njia za udanganyifu na kwa kutumia ghilba huficha mapito yao.
16 Itakuokoa pia kutokana na mwanamke kahaba, kutokana na mke aliyepotoka mwenye maneno ya kushawishi kutenda ubaya,
Busara na hekima zitakuokoa kutoka kwa mwanamke malaya, kutoka kwa mwanamke anayetafuta visa na mwenye maneno ya kubembeleza.
17 aliyemwacha mwenzi wa ujana wake na kupuuza agano alilofanya mbele ya Mungu.
Yeye humwacha mwenzi wa ujana wake na kusahau agano la Mungu wake.
18 Kwa maana nyumba yake huelekea kwenye kifo na mapito yake kwenye roho za waliokufa.
Maana nyumba yake huinama na kufa na mapito yake yatakupeleka kwa wale walioko kaburini.
19 Hakuna yeyote aendaye kwake akarudi, au kufikia mapito ya uzima.
Wote waiendeao njia yake hawatarudi tena na wala hawataziona njia za uzima.
20 Hivyo utatembea katika njia za watu wema na kushikamana na mapito ya wenye haki.
kwa hiyo utatembea katika njia ya watu wema na kufuata njia za wale watendao mema.
21 Kwa maana wanyofu wataishi katika nchi, nao wasio na lawama watabakia ndani yake.
Kwa wale watendao mema watafanya makazi yao katika nchi, na wale wenye uadilifu watadumu katika nchi.
22 Bali waovu watakatiliwa mbali kutoka nchi, nao wasio waaminifu watangʼolewa kutoka humo.
Lakini waovu wataondolewa katika nchi na wale wasioamini wataondolewa katika nchi.

< Mithali 2 >