< Mithali 19 >
1 Afadhali mtu maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama, kuliko mpumbavu ambaye midomo yake imepotoka.
Bora mtu masikini ambaye huenenda katika uadilifu wake kuliko mwenye ukaidi katika maneno yake na ni mpumbavu.
2 Sio vizuri kuwa na juhudi bila maarifa, wala kufanya haraka na kuikosa njia.
Tena, si vizuri kuwa na hamu bila maarifa na mwenye kukimbia haraka sana hukosea njia.
3 Upumbavu wa mtu mwenyewe huharibu maisha yake hata hivyo moyo wake humkasirikia Bwana.
Upuuzi wa mtu unaharibu maisha yake na moyo wake hughadhabika dhidi ya Yehova.
4 Mali huleta marafiki wengi, bali rafiki wa mtu maskini humwacha.
Utajiri huongeza marafiki wengi, bali mtu masikini hutengwa na rafiki zake.
5 Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa, naye amwagaye uongo hataachwa huru.
Shahidi wa uongo hatakosa adhabu na mwenye kupumua uongo hataokoka.
6 Wengi hujipendekeza kwa mtawala na kila mmoja ni rafiki wa mtu atoaye zawadi.
Wengi wataomba fadhila kutoka kwa mtu mkarimu na kila mtu ni rafiki wa yule anayetoa zawadi.
7 Mtu maskini huepukwa na ndugu zake wote: Je, marafiki zake watamkwepa kiasi gani! Ingawa huwafuata kwa kuwasihi, hawapatikani popote.
Mtu masikini huchukiwa na ndugu zake wote; je marafiki wengi kiasi gani hujitenga kutoka kwake! Anawaita, lakini wameondoka.
8 Yeye apataye hekima huipenda nafsi yake mwenyewe, yeye ahifadhiye ufahamu hustawi.
Anayepata hekima huyapenda maisha yake mwenyewe; yeye atunzaye ufahamu atapata kilicho chema.
9 Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa, naye amwagaye uongo ataangamia.
Shahidi wa uongo hatakosa kuadhibiwa, bali mwenye kupumua uongo ataangamia.
10 Haistahili mpumbavu kuishi katika anasa, itakuwa vibaya kiasi gani kwa mtumwa kuwatawala wakuu.
Haifai kwa mpumbavu kuishi kwa anasa- wala kwa mtumwa kutawala juu ya wafalme.
11 Hekima ya mtu humpa uvumilivu, ni kwa utukufu wake kusamehe makosa.
Busara humfanya mtu achelewe kukasirika na utukufu wake ni kusamehe kosa.
12 Ghadhabu ya mfalme ni kama mngurumo wa simba, bali wema wake ni kama umande juu ya nyasi.
Ghadhabu ya mfalme ni kama muungurumo wa simba kijana, bali fadhila yake ni kama umande kwenye majani.
13 Mwana mpumbavu ni maangamizi ya babaye, naye mke mgomvi ni kama kutonatona kusikoisha.
Mwana mpumbavu ni uharibifu kwa baba yake na mke mgomvi ni maji yanayochuruzika daima.
14 Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi, bali mke mwenye busara hutoka kwa Bwana.
Nyumba na utajiri ni urithi kutoka kwa wazazi, bali mke mwenye busara hutoka kwa Yehova.
15 Uvivu huleta usingizi mzito, naye mtu mzembe huona njaa.
Uvivu unamtupa mtu kwenye usingizi mzito, bali asiyetamani kufanya kazi atakwenda njaa.
16 Yeye ambaye hutii mafundisho huulinda uhai wake, bali yeye anayezidharau njia zake atakufa.
Yeye anayetii amri huyaongoza maisha yake, bali mtu asiyefikiri juu ya njia zake atakufa.
17 Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye atamtuza kwa aliyotenda.
Mwenye ukarimu kwa masikini humkopesha Yehova na atalipwa kwa kile alichofanya.
18 Mrudi mwanao, kwa maana katika hiyo kuna tumaini, usiwe mshirika katika mauti yake.
Mrudi mwanao wakati kuna matumaini na usiwe na shauku ya kumweka katika mauti.
19 Mtu mwenye kukasirika haraka ni lazima atapata adhabu yake, kama utamwokoa, itakubidi kufanya hivyo tena.
Mtu mwenye hasira kali lazima alipe adhabu; kama ukimwokoa, utafanya hivyo mara mbili.
20 Sikiliza mashauri na ukubali mafundisho, nawe mwishoni utakuwa na hekima.
Sikiliza ushauri na ukubali maelekezo, ili uweze kuwa na hekima mwishoni mwa maisha yako.
21 Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu, lakini kusudi la Bwana ndilo litakalosimama.
Moyoni mwa mtu kuna mipango mingi, bali kusudi la Yehova ndilo litakalo simama.
22 Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho, afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo.
Shauku ya mtu ni uaminifu na mtu masikini ni bora kuliko muongo.
23 Kumcha Bwana huongoza kwenye uzima, kisha mtu hupumzika akiwa ameridhika, bila kuguswa na shida.
Kumheshimu Yehova huwaelekeza watu kwenye uzima; mwenye nayo atashibishwa na hatadhurika kwa madhara.
24 Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani, lakini hawezi hata kuupeleka kwenye kinywa chake!
Mtu goigoi huuzika mkono wake ndani ya dishi; hataurudisha juu ya kinywa chake.
25 Mpige mwenye mzaha, naye mjinga atajifunza busara, mkemee mwenye ufahamu naye atapata maarifa.
Kama utampiga mwenye mzaha, wajinga watakuwa na hekima; mwelekeze mwenye ufahamu, naye atapata maarifa.
26 Yeye amwibiaye baba yake na kumfukuza mama yake ni mwana aletaye aibu na fedheha.
Anayempora baba yake na kumfukuza mama yake ni mwana anayeleta aibu na shutuma.
27 Mwanangu, ukiacha kusikiliza mafundisho, utatangatanga mbali na maneno ya maarifa.
Mwanangu, kama utaacha kusikiliza maelekezo, utapotea kutoka kwenye maneno ya maarifa.
28 Shahidi mla rushwa hudhihaki hukumu na kinywa cha mtu mwovu humeza ubaya kwa upesi.
Shahidi mpotofu huidhihaki haki na kinywa cha waovu humeza uovu.
29 Adhabu zimeandaliwa kwa ajili ya wenye dhihaka na mapigo kwa ajili ya migongo ya wapumbavu.
Hukumu ipo tayari kwa wenye dhihaka na mjeledi kwa migongo ya wapumbavu.