< Mithali 18 >
1 Mtu ajitengaye na wengine hufuata matakwa yake mwenyewe; hupiga vita kila shauri jema.
2 Mpumbavu hafurahii ufahamu, bali hufurahia kutangaza maoni yake mwenyewe.
3 Wakati uovu unapokuja, dharau huja pia, pamoja na aibu huja lawama.
4 Maneno ya kinywa cha mwanadamu ni kina cha maji, bali chemchemi ya hekima ni kijito kinachobubujika.
5 Sio vizuri kumpendelea mtu mwovu, au kumnyima haki asiye na hatia.
6 Midomo ya mpumbavu humletea ugomvi na kinywa chake hualika kipigo.
7 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake na midomo yake ni mtego kwa nafsi yake.
8 Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu; huingia sehemu za ndani sana za mtu.
9 Mtu aliye mlegevu katika kazi yake ni ndugu na yule anayeharibu.
10 Jina la Bwana ni ngome imara, wenye haki huikimbilia na kuwa salama.
11 Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome, wanaudhania kuwa ukuta usioweza kurukwa.
12 Kabla ya anguko moyo wa mtu hujaa kiburi, bali unyenyekevu hutangulia heshima.
13 Yeye ajibuye kabla ya kusikiliza, huo ni upumbavu wake na aibu yake.
14 Roho ya mtu itastahimili katika ugonjwa bali roho iliyovunjika ni nani awezaye kuistahimili?
15 Moyo wa mwenye ufahamu hujipatia maarifa, masikio ya mwenye hekima huyatafuta maarifa.
16 Zawadi humfungulia njia mtoaji, nayo humleta mbele ya wakuu.
17 Yeye aliye wa kwanza kuleta mashtaka huonekana sahihi, hadi mwingine ajitokezapo na kumuuliza maswali.
18 Kupiga kura hukomesha mashindano na kutenganisha wapinzani wakuu wanaopingana.
19 Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuridhika kuliko mji uliozungushiwa ngome, nayo mabishano ni kama malango ya ngome yenye makomeo.
20 Tumbo la mtu litajaa kutokana na tunda la kinywa chake, atashibishwa mavuno yanayotokana na midomo yake.
21 Mauti na uzima viko katika uwezo wa ulimi, nao waupendao watakula matunda yake.
22 Apataye mke apata kitu chema naye ajipatia kibali kwa Bwana.
23 Mtu maskini huomba kuhurumiwa bali tajiri hujibu kwa ukali.
24 Mtu mwenye marafiki wengi wanaweza kumharibu, bali yuko rafiki aambatanaye na mtu kwa karibu kuliko ndugu.