< Mithali 17 >

1 Afadhali kula ukoko mkavu ukiwa na amani na utulivu kuliko kukaa kwenye nyumba ya karamu kukiwa na magomvi.
Ni bora kuwa na utulivu pamoja chembe za mkate kuliko nyumba yenye sherehe nyingi pamoja na ugomvi.
2 Mtumishi mwenye hekima atatawala juu ya mwana aaibishaye, naye atashirikiana katika urithi kama mmoja wa hao ndugu.
Mtumishi mwenye busara atatawala juu ya mwana atendaye kwa aibu na atashiriki urithi kama mmoja wa ndugu.
3 Kalibu ni kwa ajili ya fedha na tanuru ni kwa ajili ya dhahabu, bali Bwana huujaribu moyo.
Kalibu ni kwa fedha na tanuu ni kwa dhahabu, bali Yehova huisafisha mioyo.
4 Mtu mwovu husikiliza midomo mibaya; mwongo husikiliza kwa makini ulimi wa madhara.
Mtu atendaye mabaya huwasikiliza wale wanaosema maovu; muongo anausikivu kwa wale wanaosema mambo mabaya.
5 Yeye anaye mdhihaki maskini huonyesha dharau kwa Muumba wake; yeyote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa.
Mwenye kumdhihaki masikini humtukana Muumba wake na anayefurahia msiba hatakosa adhabu.
6 Wana wa wana ni taji la wazee, nao wazazi ni fahari ya watoto wao.
Wajukuu ni taji ya wazee na wazazi huleta heshima kwa watoto wao.
7 Midomo yenye uwezo wa ushawishi haimfai mpumbavu: je, ni mibaya kiasi gani zaidi midomo ya uongo kwa mtawala!
Hotuba ya ushawishi haifai kwa mpumbavu; kidogo zaidi midomo ya uongo inafaa kwa ufalme.
8 Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; kokote kigeukiapo, hufanikiwa.
Rushwa ni kama jiwe la kiini macho kwa yule ambaye atoaye; yeye anayeiacha, hufanikiwa.
9 Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo, bali yeyote arudiaye jambo hutenganisha marafiki wa karibu.
Anayesamehe kosa hutafuta upendo, bali yeye anayerudia jambo huwatenganisha marafiki wa karibu.
10 Karipio humwingia sana mtu mwenye kutambua kuliko mapigo mia kwa mpumbavu.
Karipio hupenya ndani ya mtu mwenye ufahamu kuliko mapigo mamia kwenda kwa mpumbavu.
11 Mtu mbaya hupenda kuasi tu; mjumbe asiye na huruma atatumwa dhidi yake.
Mtu mbaya hutafuta uasi tu, hivyo mjumbe katiri atatumwa dhidi yake.
12 Ni afadhali ukutane na dubu aliyenyangʼanywa watoto wake, kuliko mpumbavu katika upumbavu wake.
Ni bora kukutana na dubu aliyeporwa watoto wake kuliko kukutana na mpumbavu katika upumbavu wake.
13 Ikiwa mtu atalipa baya kwa jema, kamwe ubaya hautaondoka katika nyumba yake.
Mtu anaporudisha mabaya badala ya mema, mabaya hayatatoka katika nyumba yake.
14 Kuanzisha ugomvi ni kama kutoboa bwawa la maji; kwa hiyo acha jambo hilo kabla mabishano hayajaanza.
Mwanzo wa mafarakano ni kama mtu anayefungulia maji kila mahali, hivyo ondoka kwenye mabishano kabla ya kutokea.
15 Yeye asemaye kuwa asiye na haki ana haki, naye asemaye kuwa mwenye haki hana haki: Bwana huwachukia sana wote wawili.
Yeye ambaye huwaachilia watu waovu au kuwalaumu wale wanaotenda haki - watu hawa wote ni chukizo kwa Yehova.
16 Fedha ina faida gani mikononi mwa mpumbavu, wakati yeye hana haja ya kupata hekima?
Kwa nini mpumbavu alipe fedha kwa kujifunza hekima, wakati hana uwezo wa kujifunza?
17 Rafiki hupenda wakati wote naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.
Rafiki hupenda kwa nyakati zote na ndugu amezaliwa kwa ajili ya nyakati za taabu.
18 Mtu mjinga hupana mkono ili kuweka rehani, naye huweka dhamana kwa jirani yake.
Mtu asiyekuwa na akili hufanya ahadi zenye mashariti na kuanza kuwajibika kwa madeni ya jirani yake.
19 Yeye apendaye ugomvi apenda dhambi; naye ainuaye sana lango lake hutafuta uharibifu.
Apendaye mafarakano anapenda dhambi; ambaye hutengeneza kizingiti kirefu sana kwenye mlango wake husababisha kuvunjia kwa mifupa.
20 Mtu mwenye moyo mpotovu hawezi kufanikiwa; naye ambaye ulimi wake ni mdanganyifu huanguka kwenye taabu.
Mtu mwenye moyo wa udanganyifu hapati chochote ambacho ni chema; na mwenye ulimi wa ukaidi huanguka kwenye janga.
21 Kuwa na mwana mpumbavu huleta huzuni; hakuna furaha kwa baba wa mpumbavu.
Mzazi wa mpumbavu huleta majonzi kwake mwenyewe; baba wa mpumbavu hana furaha.
22 Moyo wenye furaha ni dawa nzuri, bali roho iliyopondeka hukausha mifupa.
Moyo mchangamfu ni dawa njema, bali roho iliyopondeka hukausha mifupa.
23 Mtu mwovu hukubali rushwa kwa siri ili kupotosha njia ya haki.
Mtu mwovu hukubali rushwa ya siri ili kupotosha njia za haki.
24 Mtu wa ufahamu huitazama hekima, lakini macho ya mpumbavu huhangaika hadi kwenye miisho ya dunia.
Mwenye ufahamu huelekeza uso wake kwenye hekima, bali macho ya mpumbavu huelekea ncha za dunia.
25 Mwana mpumbavu huleta huzuni kwa baba yake na uchungu kwa yeye aliyemzaa.
Mwana mpumbavu ni huzuni kwa baba yake na uchungu kwa mwanamke aliyemzaa.
26 Si vizuri kumwadhibu mtu asiye na hatia, au kuwapiga sana maafisa kwa ajili ya uadilifu wao.
Pia, si vizuri kumwadhibu mwenye kutenda haki; wala si vema kuwachapa mjeledi watu waadilifu wenye ukamilifu.
27 Mtu mwenye maarifa hutumia maneno kwa kujizuia, naye mtu mwenye ufahamu ana moyo wa utulivu.
Mwenye maarifa hutumia maneno machache na mwenye ufahamu ni mtulivu.
28 Hata mtu mpumbavu hudhaniwa kuwa na hekima kama akinyamaza, na mwenye ufahamu kama akiuzuia ulimi wake.
Hata mpumbavu hudhaniwa kuwa na busara kama akikaa kimya; wakati anapokaa amefunga kinywa chake, anafikiriwa kuwa na akili.

< Mithali 17 >