< Mithali 16 >

1 Mipango ya moyoni ni ya mwanadamu, bali jibu la ulimi hutoka kwa Bwana.
Mipango ya moyo ni ya mtu, bali Yehova hutoa jawabu kutoka kwenye ulimi wake.
2 Njia zote za mtu huonekana safi machoni pake mwenyewe, bali makusudi hupimwa na Bwana.
Njia zote za mtu ni safi kwenye macho yake mwenyewe, bali Yehova huipima mioyo.
3 Mkabidhi Bwana lolote ufanyalo, nayo mipango yako itafanikiwa.
Kabidhi kwa Yehova kazi zako zote na mipango yako itafanikiwa.
4 Bwana hufanya kila kitu kwa kusudi lake mwenyewe; hata waovu kwa siku ya maangamizi.
Yehova alifanya kila kitu kwa kusudi lake, hata waovu kwa ajili ya siku ya taabu.
5 Bwana huwachukia sana wote wenye kiburi cha moyo. Uwe na hakika kwa hili: Hawataepuka kuadhibiwa.
Yehova anamchukia kila mtu mwenye moyo wa majivuno, ingawa wanasimama imara, hawakosi kupata adhabu.
6 Kwa upendo na uaminifu uovu huondolewa; kwa kumcha Bwana mtu hujiepusha na ubaya.
Kwa agano la uaminifu na udhamini uovu husafishwa na kwa kumcha Yehova watu hujitenga na ubaya.
7 Njia za mtu zinapompendeza Bwana, huwafanya hata adui zake waishi naye kwa amani.
Njia za mtu zinapompendeza Yehova, huwafanya hata adui zake huyo mtu wawe na amani naye.
8 Afadhali kitu kidogo pamoja na haki kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu.
Bora kitu kidogo pamoja na haki, kuliko mapato makubwa pamoja na udhalimu.
9 Moyo wa mtu huifikiri njia yake, bali Bwana huelekeza hatua zake.
Katika moyo wake mtu hunuia njia yake, bali Yehova huziongoza hatua zake.
10 Midomo ya mfalme huzungumza kwa hekima ya kiungu, wala kinywa chake hakipotoshi haki.
Mshauri yupo katika midimo ya mfalme, katika hukumu kinywa chake hakisemi kwa udanganyifu.
11 Vipimo na mizani za halali hutoka kwa Bwana; mawe yote ya kupimia yaliyo katika mfuko ameyafanya yeye.
Vipimo vya kweli hutoka kwa Yehova; uzito wote kwenye gunia ni kazi yake.
12 Wafalme huchukia sana kutenda maovu, kwa maana kiti cha ufalme hufanywa imara kwa njia ya haki.
Wafalme wanapofanya mambo maovu, hicho ni kitu cha kudharauliwa, kwa maana utawala huimarishwa kwa kutenda haki.
13 Wafalme hufurahia midomo ya uaminifu; humthamini mtu asemaye kweli.
Mfalme hufurahia midomo ambayo husema haki na anampenda mwenye kusema waziwazi.
14 Ghadhabu ya mfalme ni mjumbe wa mauti, bali mtu mwenye hekima ataituliza.
Hasira ya mfalme ni mjumbe wa mauti lakini mtu mwenye busara atajaribu kutuliza hasira yake.
15 Uso wa mfalme ungʼaapo, inamaanisha uhai; upendeleo wake ni kama wingu la mvua wakati wa vuli.
Katika nuru ya uso wa mfalme ni uzima na fadhila yake ni kama wingu linaloleta mvua ya masika.
16 Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu, kuchagua ufahamu kuliko fedha!
Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu. Kuchagua kupata ufahamu ni zaidi kuliko fedha.
17 Njia kuu ya wanyofu huepuka ubaya; yeye aichungaye njia yake, huchunga maisha yake.
Njia kuu ya watu waadilifu hujitenga na ubaya; mwenye kuyahifadhi maisha yake huilinda njia yake.
18 Kiburi hutangulia maangamizi, roho ya majivuno hutangulia maanguko.
Kiburi hutangulia kabla ya uharibifu na moyo wa kujivuna kabla ya maangamizi.
19 Ni afadhali kuwa mnyenyekevu katika roho miongoni mwa walioonewa kuliko kugawana nyara pamoja na wenye kiburi.
Ni bora kunyenyekea miongoni mwa watu masikini kuliko kugawana ngawira pamoja watu wenye kiburi.
20 Yeyote anayekubali mafundisho hustawi, tena amebarikiwa yeye anayemtumaini Bwana.
Mwenye kutafakari yaliyofundishwa hupata kilicho chema na wenye kumtumaini Yehova watafurahi.
21 Wenye hekima moyoni huitwa wenye ufahamu, na maneno ya kupendeza huchochea mafundisho.
Mwenye hekima moyoni anaitwa ufuhamu na utamu wa hotuba huongeza uwezo wa kufundisha.
22 Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwa wale walio nao, bali upumbavu huleta adhabu kwa wapumbavu.
Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwake ambaye nayo, bali adhabu ya wapumbavu ni upumbavu wao.
23 Moyo wa mtu mwenye hekima huongoza kinywa chake, na midomo yake huchochea mafundisho.
Moyo wa mtu mwenye hekima hutoa busara katika kinywa chake na huongeza ushawishi katika midomo yake.
24 Maneno ya kupendeza ni kama sega la asali, ni matamu kwa nafsi na uponyaji kwenye mifupa.
Maneno yenye kufaa ni sega la asali -matamu kwenye nafsi na huponya mifupa.
25 Iko njia ionekanayo kuwa sawa kwa mtu, bali mwisho wake huelekeza mautini.
Kuna njia ambayo huonekana sawa kwa mtu, bali mwisho wake ni njia ya mauti.
26 Shauku ya mfanyakazi humhimiza kufanya kazi; njaa yake humsukuma aendelee.
Hamu ya kibarua humfanyia kazi; njaa yake humsihi kuendelea.
27 Mtu mbaya kabisa hupanga mabaya, maneno yake ni kama moto uunguzao.
Mtu duni huchimba madhara na usemi wake ni kama moto unaounguza.
28 Mtu mpotovu huchochea ugomvi, nayo maongezi ya upuzi hutenganisha marafiki wa karibu.
Mtu mkaidi huchochea mafarakano na umbeya huwafarakanisha marafiki.
29 Mtu mkali humvuta jirani yake na kumwongoza katika mapito yale mabaya.
Mtu wa vurugu humdanganya jirani yake na kumwongoza kwenye mapito ambayo si mema.
30 Yeye akonyezaye kwa jicho lake anapanga upotovu; naye akazaye midomo yake amenuia mabaya.
Yule anayekonyeza kwa jicho anapanga njama za mambo ya ukaidi; wenye kuandama midomo yao watapitisha mabaya.
31 Mvi ni taji ya utukufu; hupatikana kwa maisha ya uadilifu.
Mvi ni taji ya utukufu; hupatikana kwa kuishi katika njia ya haki.
32 Ni afadhali mtu mstahimilivu kuliko shujaa, mtu anayeitawala hasira yake kuliko yule autekaye mji.
Ni bora kukawia kuwa na hasira kuliko kuwa shujaa na mwenye kutawala roho yake ni imara zaidi kuliko yule anayeuteka mji.
33 Kura hupigwa kwa siri, lakini kila uamuzi wake hutoka kwa Bwana.
Kura hurushwa kwenye mkunjo, bali maamuzi hutoka kwa Yehova.

< Mithali 16 >