< Mithali 15 >

1 Jawabu la upole hugeuza ghadhabu, bali neno liumizalo huchochea hasira.
Jawabu la upole huondoa ghadhabu, bali neno la ukatili huchochea hasira.
2 Ulimi wa mwenye hekima husifu maarifa, bali kinywa cha mpumbavu hufoka upumbavu.
Ulimi wa watu mwenye hekima husifu maarifa, bali kinywa cha wapumbavu humwaga upuuzi.
3 Macho ya Bwana yako kila mahali, yakiwaangalia waovu na wema.
Macho ya Yehova yapo kila mahali, yakiwatazama juu ya waovu na wema.
4 Ulimi uletao uponyaji ni mti wa uzima, bali ulimi udanganyao huponda roho.
Ulimi unaoponya ni mti wa uzima, bali ulimi wa udanganyifu huvunja moyo.
5 Mpumbavu hubeza maonyo ya baba yake, bali yeyote akubaliye maonyo huonyesha busara.
Mpumbavu hudharau marudi ya baba yake, bali yeye anayejifunza kutokana na masahihisho ni mwenye hekima.
6 Nyumba ya mwenye haki ina hazina kubwa, bali mapato ya waovu huwaletea taabu.
Katika nyumba ya wale watendao haki kuna hazina kubwa, bali mapato ya watu waovu huwapa taabu.
7 Midomo ya mwenye hekima hueneza maarifa, bali sivyo ilivyo mioyo ya wapumbavu.
Midomo ya wenye hekima husambaza maarifa, bali mioyo ya wapumbavu haifanyi hivyo.
8 Bwana huchukia sana dhabihu za waovu, bali maombi ya wanyofu humfurahisha Mungu.
Yehova anachukia sadaka za watu waovu, bali maombi ya watu waadilifu ndiyo furaha yake.
9 Bwana huchukia sana njia ya waovu, bali huwapenda wale wafuatao haki.
Yehova anachukia njia ya watu waovu, bali anampenda yule ambaye huandama haki.
10 Adhabu kali humngoja yeye aachaye njia; yeye achukiaye maonyo atakufa.
Marudi ya ukatili hungojea kwa yeyote ambaye huiacha njia na yule ambaye huchukia masahihisho atakufa.
11 Mauti na Uharibifu viko wazi mbele za Bwana: je, si zaidi sana mioyo ya wanadamu! (Sheol h7585)
Kuzimu na uharibifu vipo wazi mbele za Yehova; je si zaidi sana mioyo ya wana wa wanadamu? (Sheol h7585)
12 Mwenye mzaha huchukia maonyo; hatataka shauri kwa mwenye hekima.
Mwenye mzaha huchukia masahihisho; hatakwenda kwa wenye hekima.
13 Moyo wenye furaha hufanya uso uchangamke, bali maumivu ya moyoni huponda roho.
Moyo wenye furaha husababisha uchangamfu wa uso, bali huzuni huvunja moyo.
14 Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa, bali kinywa cha mpumbavu hujilisha upumbavu.
Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa, bali kinywa cha wapumbavu hujilisha kwenye upuuzi.
15 Siku zote za wanaoonewa ni za taabu, bali moyo mchangamfu una karamu ya kudumu.
Siku zote za watu waliokandamizwa ni taabu, bali moyo wenye furaha unakaramu daima.
16 Afadhali kuwa na kidogo pamoja na kumcha Bwana, kuliko mali nyingi pamoja na ghasia.
Bora kitu kidogo pamoja na kumcha Mungu kuliko hazina kubwa pamoja na ghasia.
17 Afadhali chakula cha mboga mahali palipo na upendo kuliko nyama ya ndama iliyonona pamoja na chuki.
Bora mlo wenye mboga kukiwa na upendo kuliko kuandaliwa ndama aliyenona kwa chuki.
18 Mtu mwepesi wa hasira huchochea ugomvi, bali mtu mvumilivu hutuliza ugomvi.
Mtu mwenye hasira huchochea mabishano, bali mtu ambaye hukawia kukasirika hutuliza ugomvi.
19 Njia ya mvivu imezibwa na miiba, bali njia ya mwenye haki ni barabara kuu.
Mapito ya mtu goigoi ni kama sehemu yenye uwa wa miiba, bali mapito ya mtu mwadilifu ni njia kuu iliyojengwa imara.
20 Mwana mwenye hekima huleta furaha kwa baba yake, bali mtu mpumbavu humdharau mama yake.
Mwana mwenye busara huleta furaha kwa baba yake, bali mtu mpumbavu humdharau mama yake.
21 Upumbavu humfurahisha mtu ambaye hana akili, bali mtu mwenye ufahamu hushika njia iliyonyooka.
Upuuzi humfurahia mtu ambaye amepungukiwa akili, bali mwenye ufahamu hutembea katika njia nyofu.
22 Mipango hushindwa kufanikiwa kwa ajili ya kukosa ushauri, bali kukiwa na washauri wengi hufanikiwa.
Mipango huharibika ambapo hakuna ushauri, bali washauri wengi wanafanikiwa.
23 Mtu hupata furaha katika kutoa jibu linalofaa: je, ni zuri namna gani neno lililotoka kwa wakati wake!
Mtu anapata furaha wakati anapotoa jibu la kufaa; je ni zuri kiasi gani neno kwa wakati muafaka!
24 Mapito ya uzima huelekea juu kwa ajili ya wenye hekima kumwepusha asiende chini kaburini. (Sheol h7585)
Njia ya uzima huwapeleka juu watu wenye hekima, ili waondoke kutoka chini kuzimu. (Sheol h7585)
25 Bwana hubomoa nyumba ya mtu mwenye kiburi, bali huilinda mipaka ya mjane isiguswe.
Yehova hurarua urithi wa mwenye kiburi, bali huzilinda mali za mjane.
26 Bwana huchukia sana mawazo ya mwovu, bali mawazo ya wale walio safi humfurahisha yeye.
Yehova huyachukia mawazo ya watu waovu, bali maneno ya upole ni safi.
27 Mtu mwenye tamaa huletea jamaa yake taabu, bali yeye achukiaye rushwa ataishi.
Mporaji huleta shida kwenye familia yake, bali yeye ambaye huchukia rushwa ataishi.
28 Moyo wa mwenye haki hupima majibu yake, bali kinywa cha mwovu hufoka ubaya.
Moyo wa yule atendaye haki hutafakari kabla ya kujibu, bali kinywa cha watu waovu humwanga ubaya wake wote.
29 Bwana yuko mbali na waovu, bali husikia maombi ya wenye haki.
Yehova yupo mbali na watu waovu, bali husikia maombi ya wale watendao haki.
30 Mtazamo wa tabasamu huleta furaha moyoni, nazo habari njema huipa mifupa afya.
Nuru ya macho huleta furaha moyoni na habari njema ni afya kwenye mwili.
31 Yeye asikilizaye maonyo yatoayo uzima atakuwa miongoni mwa wenye hekima.
Kama utazingatia wakati mtu anapokurekebisha jinsi ya kuishi, utabaki miongoni mwa watu wenye busara.
32 Yeye anayedharau maonyo hujidharau mwenyewe, bali yeyote anayekubali maonyo hupata ufahamu.
Yeye anayekataa karipio hujidharau mwenyewe, bali yule asikilizaye masahihisho hujipatia ufahamu.
33 Kumcha Bwana humfundisha mtu hekima, nao unyenyekevu huja kabla ya heshima.
Kumcha Yehova hufundisha hekima na unyenyekevu huja kabla ya heshima.

< Mithali 15 >