< Mithali 13 >

1 Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya babaye, bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.
Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya baba yake, bali mwenye dhihaka hatasikiliza karipio.
2 Kutoka tunda la midomo yake mtu hufurahia mambo mema, bali wasio waaminifu wanatamani sana jeuri.
Mtu hufurahia vitu vizuri kutokana na matunda ya kinywa chake, bali hamu ya wadanganyifu ni jeuri.
3 Yeye alindaye midomo yake hulinda nafsi yake, bali yeye asemaye kwa haraka ataangamia.
Yeye anayelinda kinywa chake huyalinda maisha, bali anayefumbua sana midomo yake atajiangamiza mwenyewe.
4 Mvivu hutamani sana na hapati kitu, bali nafsi ya mwenye bidii hutoshelezwa kikamilifu.
Hamu ya watu wavivu ni uchu lakini hawapati kitu, bali hamu ya watu wenye bidii hutoshelezwa sana.
5 Mwenye haki huchukia uongo, bali waovu huleta aibu na fedheha.
Atendaye haki huchukia uongo, bali mtu mwovu hukinzana mwenyewe, na kufanya ya kuaibisha.
6 Haki humlinda mtu mwadilifu, bali uovu humwangusha mwenye dhambi.
Wenye haki huwalinda wale ambao ni wakamilifu katika mapito yao, bali uovu huwaangusha wale watendao dhambi.
7 Mtu mmoja hujifanya tajiri, kumbe hana chochote; mwingine hujifanya maskini, kumbe ana utajiri mwingi.
Kuna mtu ambaye hujitajirisha mwenyewe, lakini hana chochote na kuna mtu ambaye hutoa kila kitu, bado ni tajiri kweli.
8 Utajiri wa mtu waweza kukomboa maisha yake, bali mtu maskini hasikii kitisho.
Mtu tajiri anaweza kufidia maisha yake kwa mali zake, bali mtu masikini hatapokea kitisho cha aina hiyo.
9 Nuru ya mwenye haki hungʼaa sana, bali taa ya mwovu itazimwa.
Mwanga wa mtu atendaye haki hufurahia, bali taa ya waovu itazimika.
10 Kiburi huzalisha magomvi tu, bali hekima hupatikana kwa wale wanaozingatia ushauri.
Kiburi huzaa mafarakano, bali kwa wale wasikiao shauri jema kuna hekima.
11 Fedha isiyo ya halali hupungua, bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka.
Penye majivuno mengi utajiri hufifia, bali yeye apataye pesa kwa kufanya kazi kwa mkono wake pesa zake zitaongezeka.
12 Kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua, bali tumaini lililotimizwa ni mti wa uzima.
Tumaini linapoachwa, huvunja moyo, bali kukamilishwa kwa shauku ni mti wa uzima.
13 Yeye anayedharau mafundisho anajiletea maangamizi, bali yeye anayeheshimu agizo hupewa tuzo.
Yule ambaye anadharau fundisho bado atakuwa chini ya utawala wake, bali yeye ambaye anaheshimu amri atapewa thawabu.
14 Mafundisho ya mwenye busara ni chemchemi ya uzima, ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti.
Mafundisho ya mtu mwenye hekima ni chemchemi ya uzima, yanakuondoa kutoka kwenye mitego ya mauti.
15 Ufahamu mzuri hupata upendeleo, bali njia ya asiye mwaminifu ni ngumu.
Busara njema huleta fadhila, bali njia ya wadanganyifu haina mwisho.
16 Kila mwenye busara hutenda kwa maarifa, bali mpumbavu hudhihirisha upumbavu wake.
Watu wenye busara hutenda kwa maarifa kwa kila uamuzi, bali mpumbavu huonyesha upuuzi wake.
17 Mjumbe mwovu huanguka kwenye taabu, bali mjumbe mwaminifu huleta uponyaji.
Mjumbe mbaya huangukia kwenye shida, bali balozi mwaminifu huleta upatanisho.
18 Yeye anayedharau maonyo hupata umaskini na aibu, bali yeye anayekubali maonyo huheshimiwa.
Yeye ambaye hupuuza kurudiwa atapata umasikini na aibu, bali heshima itamjia yeye ambaye hujifunza kutokana na masahihisho.
19 Tarajio lililotimizwa ni tamu kwa nafsi, bali wapumbavu huchukia sana kuacha ubaya.
Shauku iliyotambuliwa ni tamu kwa hamu, bali wapumbavu huchukia kuacha uovu.
20 Yeye atembeaye na mwenye hekima atapata hekima, bali rafiki wa mpumbavu hupata madhara.
Tembea pamoja na watu wenye hekima nawe utakuwa na hekima, bali rafiki wa wapumbavu atateseka.
21 Balaa humwandama mtenda dhambi, bali mafanikio ni thawabu kwa mwenye haki.
Maafa huwakimbilia wenye dhambi, bali wale watendao haki hupewa thawabu kwa mema.
22 Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi, bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa kwa ajili ya wenye haki.
Mtu mwema huacha urithi kwa wajukuu wake, bali mali ya mwenye dhambi huwekwa akiba kwa yule atendaye haki.
23 Shamba la mtu maskini laweza kuzalisha chakula kingi, bali dhuluma hukifutilia mbali.
Shamba la masikini lisilolimwa linaweza huzalisha chakula kingi, bali huchukuliwa kwa udhalimu.
24 Yeye aizuiaye fimbo yake hampendi mwanawe, bali yeye ampendaye huwa mwangalifu kumwadibisha.
Yeye ambaye hamrudi mwanawe humchukia, bali yule anayempenda mwanawe humjali kwa kumwadibisha.
25 Mwenye haki hula mpaka akaridhisha moyo wake, bali tumbo la mwovu hutaabika kwa njaa.
Yeye atendaye haki hula hadi kutosheleza hamu yake bali tumbo la mwovu linanjaa daima.

< Mithali 13 >