< Mithali 12 >
1 Yeyote apendaye kuadibishwa hupenda maarifa, bali yeye achukiaye kuonywa ni mpumbavu.
Anayependa mafundisho hupenda maarifa, bali yule anayechukia maonyo ni mpumbavu.
2 Mtu mwema hupata kibali kutoka kwa Bwana, bali Bwana humhukumu mwenye hila.
Yehova humpa fadhila mtu mwema, bali mtu ambaye hufanya mipango ya ufisada atahukumiwa.
3 Mtu hathibitiki kutokana na uovu, bali mwenye haki hataondolewa.
Mtu hawezi kuimarishwa kwa uovu, bali wale watendao haki hawawezi kung'olewa.
4 Mke mwenye tabia nzuri ni taji ya mumewe, bali aaibishaye ni kama uozo katika mifupa ya mumewe.
Mke mwema ni taji ya mume wake, bali yule aletaye aibu ni kama ugonjwa unaoozesha mifupa yake.
5 Mipango ya mtu mwadilifu ni ya haki, bali ushauri wa mwovu ni udanganyifu.
Mipango ya wale watendao haki ni adili, bali shauri la mwovu ni udanganyifu.
6 Maneno ya waovu huotea kumwaga damu, bali maneno ya waadilifu huwaokoa.
Maneno ya watu waovu ni uviziaji unaosubiri nafasi ya kuua, bali maneno ya mwenye haki yatawatunza salama.
7 Watu waovu huondolewa na kutoweka, bali nyumba ya mwenye haki husimama imara.
Watu waovu wametupwa na kuondolewa, bali nyumba ya wale watendao haki itasimama.
8 Mtu husifiwa kulingana na hekima yake, bali watu wenye akili zilizopotoka hudharauliwa.
Mtu husifiwa kwa kadri ya hekima yake, bali yule anayechagua ukaidi hudharauliwa.
9 Heri mtu wa hali ya chini mwenye mtumishi, kuliko kujifanya mtu wa hali ya juu nawe huna chakula.
Bora kuwa na cheo duni- kuwa mtumishi tu- kuliko kujisifu kuhusu ukuu wako bila kuwa na chakula.
10 Mtu mwenye haki hujali mahitaji ya mnyama wake, bali matendo ya huruma ya mwovu ni ukatili.
Yule atendaye haki anajali mahitaji ya mnyama wake, bali huruma ya mwovu ni ukatili.
11 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele, bali yeye afuataye mambo ya upuzi hana akili.
Yule atendaye kazi katika shamba lake atapata chakula tele, bali anayesaka miradi duni hana akili.
12 Waovu hutamani mateka ya watu wabaya, bali shina la mwenye haki hustawi.
Watu waovu hutamani wanavyoiba watu wabaya kutoka kwa wengine, bali tunda la wale watendao haki hutoka kwao mwenyewe.
13 Mtu mwovu hunaswa kwa mazungumzo yake ya dhambi, bali mwenye haki huepuka taabu.
Mtu mbaya hunaswa kwa maongezi yake mabaya, bali wale watendao haki hujinasua katika taabu.
14 Kutokana na tunda la midomo yake mtu hujazwa na mambo mema, hakika kama ilivyo kazi ya mikono yake humtunza.
Mtu hushiba vitu vyema kutokana na tunda la maneno yake, kama vile kazi ya mikono yake inavyompa thawabu.
15 Njia ya mpumbavu huonekana sawa machoni pake mwenyewe, bali mtu mwenye hekima husikiliza ushauri.
Njia ya mpumbavu ni sawa machoni pake mwenyewe, bali mtu wa hekima husikiliza ushauri.
16 Mpumbavu huonyesha kuudhika kwake mara moja, bali mtu wa busara hupuuza matukano.
Mpumbavu huonyesha hasira yake papo hapo, bali asiyejali tusi ni mwenye busara.
17 Shahidi wa kweli hutoa ushuhuda wa kuaminika, bali shahidi wa uongo husema uongo.
Asemaye ukweli huongea ilivyo haki, bali shahidi wa uongo huongea uongo.
18 Maneno ya kipumbavu huchoma kama upanga, bali ulimi wa mwenye hekima huleta uponyaji.
Maneno yake asemaye kwa pupa ni kama kurusha upanga, bali ulimi wa mwenye hekima huleta uponyaji.
19 Midomo isemayo kweli hudumu milele, bali ulimi wa uongo hudumu kwa muda mfupi tu.
Midomo yenye kweli itadumu milele, bali ulimi wa uongo ni kwa kitambo kidogo tu.
20 Upo udanganyifu katika mioyo ya wale ambao hupanga mabaya, bali kuna furaha kwa wale wanaoleta amani.
Kuna udanganyifu katika mioyo ya wale wanaopanga kutenda uovu, bali furaha hutoka kwa washauri wa amani.
21 Hakuna dhara linalompata mwenye haki, bali waovu wana taabu nyingi.
Hakuna ugonjwa utakaowajia wale watendao haki, bali watu waovu watajazwa matatizo.
22 Bwana anachukia sana midomo idanganyayo, bali hufurahia watu ambao ni wa kweli.
Yehova anachukia midomo ya uongo, bali wale ambao huishi kwa uaminifu ndiyo furaha yake.
23 Mtu mwenye busara hujihifadhia maarifa yeye mwenyewe, bali moyo wa wapumbavu hububujika upumbavu.
Mtu mwenye busara anasitiri maarifa yake, bali moyo wa wapumbavu hupiga yowe za kipumbavu.
24 Mikono yenye bidii itatawala, bali uvivu huishia katika kazi za utumwa.
Mkono wa mwenye bidii utatawala, bali watu wavivu watawekwa katika kazi za kulazimishwa.
25 Moyo wa wasiwasi humlemea mtu, bali neno la huruma humfurahisha.
Mashaka katika moyo wa mtu humwelemea, bali neno zuri humfurahisha.
26 Mtu mwenye haki ni mwangalifu katika urafiki, bali njia ya waovu huwapotosha.
Mwenye haki ni kiongozi kwa rafiki yake, bali njia ya waovu huwaongoza katika kupotea.
27 Mtu mvivu haoki mawindo yake, bali mtu mwenye bidii ana mali za thamani.
Watu wavivu hawawezi kubanika mawindo yao wenyewe, bali mtu wenye bidii atapata mali zenye thamani.
28 Katika njia ya haki kuna uzima; katika mapito hayo kuna maisha ya milele.
Wale ambao wanatembea katika njia ya haki wanapata uzima na katika mapito hayo hakuna kifo.