< Mithali 10 >

1 Mithali za Solomoni: Mwana mwenye hekima huleta furaha kwa baba yake, lakini mwana mpumbavu huleta huzuni kwa mama yake.
Mithali za Sulemani. Mwana mwenye hekima humfurahisha baba yake lakini mwana mpumbavu huleta majonzi kwa mama yake.
2 Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai, lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.
Hazina zilizolimbikizwa kwa uovu hakosa thamani, bali kwa kutenda haki hujilinda mbali na kifo.
3 Bwana hawaachi waadilifu kukaa njaa, lakini hupinga tamaa ya mtu mwovu.
Yehova hawaachi wale watendao haki wapate njaa, bali hamu ya waovu huizuia.
4 Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.
Mkono mlegevu humfanya mtu awe masikini, bali mkono wa mtu mwenye bidii hupata utajiri.
5 Yeye akusanyaye mazao wakati wa kiangazi ni mwana mwenye hekima, lakini yeye alalaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.
Mwana mwenye busara hukusanya mazao wakati wa kiangazi, bali ni aibu kwake alalaye wakati wa mavuno.
6 Baraka huwa taji kichwani mwa mwenye haki, lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.
Zawadi kutoka kwa Mungu zipo juu ya kichwa cha wale watendao haki; bali kinywa cha uovu hufunikwa kwa jeuri.
7 Kumbukumbu ya mwenye haki itakuwa baraka, lakini jina la mwovu litaoza.
Mtu atendaye haki anatufurahisha tunapomkumbuka, bali jina la mwovu litaoza.
8 Mwenye hekima moyoni hupokea maagizo, lakini mpumbavu apayukaye huangamia.
Wale wenye akili hukubali maagiza, bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataangamia.
9 Mtu mwadilifu hutembea salama, lakini mtu aendaye katika njia zilizopotoka atagunduliwa.
Yeye anayetembea katika uadilifu hutembea katika usalama, bali yule anayepotosha njia zake, ataonekana.
10 Yeye akonyezaye kwa nia mbaya husababisha huzuni, naye mpumbavu apayukaye huangamia.
Yeye ambaye hukonyeza kwa jicho lake huleta majonzi, bali mpumbavu mwenye maneno mengi atatupwa chini.
11 Kinywa cha mwenye haki ni chemchemi ya uzima, lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.
Kinywa cha mwenye kutenda haki ni kama chemchemi ya maji ya uzima, bali kinywa cha uovu hufunikwa kwa jeuri.
12 Chuki huchochea faraka, lakini upendo husitiri mabaya yote.
Chuki huchochea mafarakano, bali upendo hufunika juu ya makwazo yote.
13 Hekima hupatikana katika midomo ya wenye kupambanua, lakini fimbo ni kwa ajili ya mgongo wake asiye na ufahamu.
Hekima inapatikana kwenye kinywa cha mtu mwenye ufahamu, bali fimbo ni kwa ajili ya mgongo wa yule asiye na akili.
14 Wenye hekima huhifadhi maarifa, bali kinywa cha mpumbavu hualika maangamizi.
Watu wenye hekima hutunza maarifa, bali kinywa cha mpumbavu huleta uharibifu karibu.
15 Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome, bali ufukara ni maangamizi ya maskini.
Mali ya mtu tajiri ni mji wake mwenye ngome; ufukara wa masikini ni uharibifu wao.
16 Ujira wa wenye haki huwaletea uzima, lakini mapato ya waovu huwaletea adhabu.
Mshahara wa watenda haki huelekea kwenye uzima; manufaa ya waovu huelekea dhambini.
17 Anayekubali kuadibishwa yuko katika njia ya uzima, lakini yeyote anayepuuza maonyo hupotosha wengine.
Kuna njia kwenda kwenye uzima kwa yule anayefuata maongozo, bali anayekataa maonyo hupotea.
18 Yeye afichaye chuki yake ana midomo ya uongo, na yeyote anayeeneza uchonganishi ni mpumbavu.
Yeye afichaye chuki anamidomo ya uongo, na yeye anayesambaza kashfa ni mpumbavu.
19 Wakati maneno ni mengi, dhambi haikosekani, lakini yeye ambaye huzuia ulimi wake ni mwenye busara.
Katika maneno mengi, hapakosi uhalifu, bali aliyemwangalifu katika usemi wake ni mwenye busara.
20 Ulimi wa mwenye haki ni fedha iliyo bora, bali moyo wa mwovu una thamani ndogo.
Ulimi wa yule atendaye haki ni fedha safi; kuna thamani ndogo katika moyo wa mbaya.
21 Midomo ya mwenye haki hulisha wengi, lakini wapumbavu hufa kwa kukosa ufahamu.
Midomo ya yule atendaye haki huwastawisha wengi, bali wapumbavu hufa kwa sababu ya kukosa akili.
22 Baraka ya Bwana hutajirisha, wala haichanganyi huzuni.
Zawadi njema za Yehova huleta utajiri na haweki maumivu ndani yake.
23 Mpumbavu hufurahia tabia mbaya, lakini mtu mwenye ufahamu hupendezwa na hekima.
Uovu ni mchezo achezao mpumbavu, bali hekima ni furaha kwa mtu mwenye ufahamu.
24 Kile anachoogopa mwovu ndicho kitakachompata; kile anachoonea shauku mwenye haki atapewa.
Hofu ya mwenye uovu humkumba ghafla, bali shauku ya mwenye haki itatimizwa.
25 Tufani inapopita, waovu hutoweka, lakini wenye haki husimama imara milele.
Waovu ni kama dhoruba inayopita, na hawapo tena, bali mwenye haki ni msingi unaodumu milele.
26 Kama siki ilivyo kwa meno na moshi kwa macho, ndivyo alivyo mvivu kwa wale waliomtuma.
Kama siki kwenye meno na moshi kwenye macho, ndivyo alivyo mvivu kwa wale waliomtuma.
27 Kumcha Bwana huongeza urefu wa maisha, lakini miaka ya mwovu inafupishwa.
Hofu ya Yehova huongeza maisha, bali miaka ya waovu itakuwa mifupi.
28 Tarajio la mwenye haki ni furaha, bali matumaini ya mwovu huwa si kitu.
Matumaini ya wale watendao haki ndiyo furaha yao, bali miaka ya waovu itakuwa mifupi.
29 Njia ya Bwana ni kimbilio kwa wenye haki, lakini ni maangamizi ya wale watendao mabaya.
Njia ya Yehova huwalinda wale wenye uadilifu, bali kwa waovu ni uhalibifu.
30 Kamwe wenye haki hawataondolewa, bali waovu hawatasalia katika nchi.
Wale watendao haki hawataondolewa, bali waovu hawatabaki katika nchi.
31 Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima, bali ulimi wa upotovu utakatwa.
Katika kinywa cha wale watendao haki hutoka tunda la hekima, bali ulimi wa kupotosha utakatwa.
32 Midomo ya wenye haki inajua kile kinachofaa, bali kinywa cha mwovu hujua kile kilichopotoka tu.
Midomo ya wale watendao mema huyajua yanayokubalika, bali kinywa cha waovu, huyajua yanayopotosha.

< Mithali 10 >