< Wafilipi 3 >
1 Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana! Mimi kuwaandikia mambo yale yale hakuniudhi, kwa maana ni kinga kwa ajili yenu.
2 Jihadharini na mbwa, wale watenda maovu, jihadharini na wale wajikatao miili yao, wasemao ili kuokoka ni lazima kutahiriwa.
3 Kwa maana sisi ndio tulio tohara, sisi tumwabuduo Mungu katika Roho, tunaona fahari katika Kristo Yesu, ambao hatuweki tumaini letu katika mwili,
4 ingawa mimi mwenyewe ninazo sababu za kuutumainia mwili. Kama mtu yeyote akidhani anazo sababu za kuutumainia mwili, mimi zaidi.
5 Nilitahiriwa siku ya nane, mimi ni Mwisraeli wa kabila la Benyamini, Mwebrania wa Waebrania. Kwa habari ya sheria, ni Farisayo,
6 kwa habari ya juhudi, nilikuwa nalitesa kanisa, kuhusu haki ipatikanayo kwa sheria, mimi nilikuwa sina hatia.
7 Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.
8 Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi cha kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo.
9 Nami nionekane mbele zake bila kuwa na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu kwa njia ya imani.
10 Nataka nimjue Kristo na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake,
11 ili kwa njia yoyote niweze kufikia ufufuo wa wafu.
12 Si kwamba nimekwisha kufikia, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha! Bali nakaza mwendo ili nipate kile ambacho kwa ajili yake, nimeshikwa na Kristo Yesu.
13 Ndugu zangu, sijihesabu kuwa nimekwisha kushika. Lakini ninafanya jambo moja: Ninasahau mambo yale yaliyopita, nakaza mwendo kufikia yale yaliyo mbele.
14 Nakaza mwendo nifikie ile alama ya ushindi iliyowekwa ili nipate tuzo ya mwito mkuu wa Mungu ambao nimeitiwa huko juu mbinguni katika Kristo Yesu.
15 Hivyo sisi sote tuliokuwa kiroho tuwaze jambo hili, hata mkiwaza mengine katika jambo lolote, Mungu ataliweka wazi hilo nalo.
16 Lakini na tushike sana lile ambalo tumekwisha kulifikia.
17 Ndugu zangu, kwa pamoja fuateni mfano wangu na kuwatazama wale wanaofuata kielelezo tulichowawekea.
18 Kwa maana, kama nilivyokwisha kuwaambia mara nyingi kabla, nami sasa nasema tena hata kwa machozi, watu wengi wanaishi kama adui wa msalaba wa Kristo.
19 Mwisho wa watu hao ni maangamizi, Mungu wao ni tumbo, na utukufu wao ni aibu, na mawazo yao yamo katika mambo ya dunia.
20 Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani, Bwana Yesu Kristo,
21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.