< Hesabu 36 >
1 Viongozi wa jamaa ya ukoo wa Gileadi mwana wa Makiri, mwana wa Manase, waliokuwa wametoka katika koo za wazao wa Yosefu, walikuja na kuzungumza mbele ya Mose na viongozi, wakuu wa jamaa ya Waisraeli.
2 Wakasema, “Bwana alipomwamuru bwana wangu kuwapa Waisraeli nchi kama urithi kwa kura, alikuamuru kutoa urithi wa ndugu yetu Selofehadi kwa binti zake.
3 Sasa ikiwa wataolewa na watu wa makabila mengine ya Kiisraeli, itakuwa kwamba urithi wao utaondolewa kutoka urithi wa mababu zetu na kuongezwa katika urithi wa kabila ambalo dada hao wameolewa. Kwa hiyo sehemu ya urithi tuliyogawiwa itachukuliwa kutoka kwetu.
4 Wakati mwaka wa Yubile kwa Waisraeli utafika, urithi wao utaongezwa kwa lile kabila ambalo wameolewa, na mali yao itaondolewa kutoka urithi wa kabila la mababu zetu.”
5 Ndipo kwa agizo la Bwana Mose akatoa amri ifuatayo kwa Waisraeli: “Kile wazao wa kabila la Yosefu wanachosema ni kweli.
6 Hivi ndivyo Bwana anavyoamuru kwa binti za Selofehadi: Wanaweza kuolewa na mtu yeyote wampendaye, mradi tu waolewe miongoni mwa koo za kabila za baba yao.
7 Hakuna urithi katika Israeli utakaohamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila Mwisraeli atatunza ardhi ya kabila lake aliyoirithi kutoka kwa baba zake.
8 Kila binti atakayerithi ardhi katika kabila lolote la Israeli ni lazima aolewe na mtu kutoka kabila na ukoo wa baba yake, ili kila Mwisraeli amiliki urithi wa baba zake.
9 Hakuna urithi uwezao kuhamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila kabila la Israeli litatunza nchi linayorithi.”
10 Kwa hiyo binti za Selofehadi wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Mose.
11 Binti za Selofehadi, ambao ni Mahla, Tirsa, Hogla, Milka na Noa, wakaolewa na waume, wana wa ndugu za baba yao.
12 Waliolewa ndani ya koo za wazao wa Manase mwana wa Yosefu, na urithi wao ukabaki katika ukoo na kabila la baba yao.
13 Haya ndiyo maagizo na masharti ambayo Bwana aliwapa Waisraeli kupitia Mose katika tambarare za Moabu, karibu na Yordani ngʼambo ya Yeriko.