< Hesabu 28 >

1 Bwana akamwambia Mose,
BWANA akanena na Musa akamwambia,
2 “Wape Waisraeli agizo hili na uwaambie: ‘Hakikisheni kwamba mnaniletea mimi kwa wakati uliowekwa chakula kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa moto, kama harufu nzuri ya kupendeza.’
“Waamuru wana wa Isrseli uwaambie, 'Mtanitolea sadaka kwa wakati uliopangwa, chakula cha sadaka yangu kilichotengenezwa kwa moto ili kutoa harufu nzuri kwa ajili yangu.
3 Waambie: ‘Hii ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto mnayomtolea Bwana: wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja wasio na dosari, kama sadaka ya kawaida ya kuteketezwa kila siku.
Pia uwaambie, 'Hii ni sadaka iliyotengenezwa kwa moto ambayo mtaitoa kwa BWANA- mwanakondoo dume wa mwaka mmoja asiyekuwa na waa, wawili kila siku kuwa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku.
4 Andaa mwana-kondoo mmoja asubuhi na mwingine jioni,
Mwanakodoo mmoja atatolewa sadaka asubuhi, na mwingine atatolewa sadaka jioni.
5 kila mmoja atolewe pamoja na sadaka ya nafaka sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa pamoja na robo ya hini ya mafuta ya zeituni.
Mtatoa sadaka ya sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta yaliyokamuliwa.
6 Hii ni sadaka ya kawaida ya kuteketezwa iliyoanzishwa katika Mlima Sinai kama harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto.
Hii ni sadaka ya ya kuteketezwa ya kila siku iliyoamriwa mlima Sinai ili kutoa harufu nzuri, sadaka iliyotengenezwa kwa moto kwa ajili ya BWANA.
7 Sadaka ya kinywaji itakayotolewa pamoja na kila mwana-kondoo ni robo ya hini ya kinywaji kilichochachuka. Mimina sadaka ya kinywaji kwa Bwana mahali patakatifu.
Pamoja na robo ya hini ya sadaka ya kinywaji kwa mmoja wa hao wanakondoo. Utaimimina mahali patakatifu hiyo sadaka ya kinywaji kwa BWANA.
8 Andaa yule mwana-kondoo wa pili jioni, pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka ya kinywaji kama ulivyofanya kwa ile sadaka nyingine ya asubuhi. Hii ni sadaka iliyotolewa kwa kuteketezwa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Bwana.
Yule mwanakondoo mwingine utamtoa sadaka jioni pamoja na sadaka ya unga kama kama yule wa asubuhi alivyotolewa. Pia utatoa tena sadaka ya kinywaji pamoja naye, sadaka iliyotengenezwa kwa moto ili kutoa harufu nzuri kwa BWANA.
9 “‘Siku ya Sabato, utatoa sadaka ya wana-kondoo wawili wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari pamoja na sadaka yake ya kinywaji na sadaka ya nafaka yenye uzito wa sehemu mbili za kumi za efa za unga laini uliochanganywa na mafuta.
Katika siku ya Sabato utatoa wanakondoo dume wawili, wa umri wa mwaka mmoja kila mmoja wasiokuwa na dosari, na sehemu ya kumi mbili ya efa ya unga mwembamba kwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, pamoja na sadaka ya kinywaji.
10 Hii ni sadaka ya kuteketezwa itakayotolewa kwa ajili ya kila Sabato, pamoja na sadaka ya kawaida ya kuteketezwa na sadaka yake ya kinywaji.
Hii itakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa kila siku ya Sabato, kama nyongeza ya ile sadaka ya kila siku pamoja na ile sadaka ya kinywaji.
11 “‘Siku ya kwanza ya kila mwezi, mtamletea Bwana sadaka ya kuteketezwa ya fahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja na wana-kondoo saba wa mwaka mmoja, wote wasiokuwa na dosari.
Kila mwanzo wa mwezi, mtatoa sadaka za kuteketezwa kwa BWANA. Utatoa sadaka ya fahari wawili wachanga, kondoo dume mmoja, na wanakondoo dume saba wa umri wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari.
12 Pamoja na kila fahali, kutakuwa na sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi za efa, uliochanganywa na mafuta, pamoja na kondoo dume mmoja, sadaka ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta;
Pia mtatoa sehemu ya kumi tatu ya efa unga mwembamba kuwa sadaka ya unga uliochanganywa na mafuta kwa kila fahari, na sehemu za kumi mbili za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga uliochanganywa na mafuta kwa yule kondoo mume mmoja.
13 pamoja na kila mwana-kondoo, sadaka ya nafaka yenye uzito wa sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta. Hii ni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri, sadaka ya kuteketezwa iliyotolewa kwa moto kwa Bwana.
Pia mtatoa sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga kwa kila mwanakondoo. Hii itakuwa sadaka ya kuteketezwa, ya kutoa harufu nzuri, sadaka iliyotengenezwa kwa moto kwa ajilI ya BWANA.
14 Pamoja na kila fahali kutakuwa na sadaka ya kinywaji nusu ya hini ya divai; pamoja na kila kondoo dume, theluthi moja ya hini, na pamoja na kila mwana-kondoo robo hini. Hii ni sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi itakayotolewa kila mwandamo wa mwezi kwa mwaka.
Sadaka ya kinywaji ya watu itakuwa nusu ya hini ya divai ya yule fahari, sehemu ya tatu ya hini ya kondoo dume, na robo ya hini ya mwanakondoo. Hii ndiyo itakuwa sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi kwa miezi yote ya mwaka.
15 Zaidi ya sadaka ya kawaida ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya kinywaji, mbuzi mmoja dume atatolewa kwa Bwana kama sadaka ya dhambi.
Mtatoa beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi kwa BWANA. Hii itakuwa nyongeza kwa ile sadaka ya kila siku pamoja na ile sadaka ya viinywaji.
16 “‘Katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, itafanyika Pasaka ya Bwana.
Katika siku kumi na nne, ya mwezi wa kwanza itakuwa Pasaka ya BWANA.
17 Katika siku ya kumi na tano ya mwezi huo itakuwa sikukuu; kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu.
Katika sku ya kumi na tano ya mwezi huu kutakuwa na sikukuu. Mtakuka mikate isiyo na chachu kwa siku saba.
18 Katika siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu, msifanye kazi za kawaida.
Katika siku ya kwanza kutakuwa na kusanyiko takatifu la kumheshimu BWANA. Katika siku hiyo msifanye kazi zenu za kila siku
19 Leteni mbele za Bwana sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya kuteketezwa ya mafahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja na wana-kondoo dume saba wenye umri wa mwaka mmoja, wote wasio na dosari.
Hata hivyo, mtatoa sadaka iliyotengenezwa kwa moto, sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA. Mtatoa sadaka ya fahari wawili, kondoo dume mmoja, na kondoo dume saba wa umri wa mwaka mmoja wakamilifu.
20 Pamoja na kila fahali, andaa sadaka ya nafaka sehemu tatu za kumi za efa za unga laini uliochanganywa na mafuta; pamoja na kondoo dume, andaa sehemu mbili za kumi za efa;
Pamoja na yule fahari, mtatoa sadaka sehemu za tatu efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, pamoja na yule kondoo mume sehemu za pili za kumi.
21 pia pamoja na kila mmoja wa wale wana-kondoo saba, andaa sehemu ya kumi ya efa.
Kwa kila wale wanakondoo saba, mtatoa sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta,
22 Pia mtoe beberu mmoja kama sadaka ya dhambi ambaye atafanya upatanisho kwa ajili yenu.
na beberu mmoja kuwa sdaka ya dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
23 Andaa hizi licha ya zile sadaka za kawaida za kuteketezwa za kila asubuhi.
Mtotoa hivi vitu kama sadaka ya nyongeza katika ile sadaka ya kila siku inayotakiwa kila asubuhi.
24 Kwa njia hii andaa chakula cha sadaka ya kuteketezwa kila siku, kwa siku saba kama harufu nzuri impendezayo Bwana. Hii itaandaliwa licha ya ile sadaka ya kawaida ya kuteketezwa ya kila siku pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
Kama ilivyofafanuliwa hapa, mtatoa sadaka hizi kila siku, kwa zile siku saba za Pasaka, kile chakula cha sadaka kilichotengenezwa kwa moto kuwa harufu nzuri kwa BWANA. Hiki kitatolewa kuwa sadaka ya nyongeza ya ile sadaka ya kuteketezwa na pamoja na ile sadaka ya vinywaji.
25 Siku ya saba mwe na kusanyiko takatifu na msifanye kazi zenu za kawaida.
Siku ya saba mtakuwa na kusanyiko takatifu ili kumheshimu BWANA, na katika siku hiyo msifanye zile kazi zenu zakila siku.
26 “‘Siku ya malimbuko, mnapomletea Bwana sadaka ya nafaka mpya wakati wa Sikukuu ya Majuma, mwe na kusanyiko takatifu na msifanye kazi zenu za kawaida.
Pia katika siku ya malimbuko, mtakapokuwa mnatoa sadaka ya unga mpya katika sikukuu zenu za Majuma, mtakuwa na kusanyiko takatifu la kumheshimu BWANA, na katika siku hiyo msifanye kazi zenu za kila siku.
27 Mlete sadaka ya kuteketezwa ya mafahali wawili wachanga, kondoo dume mmoja, na pia wana-kondoo saba wenye umri wa mwaka mmoja, kama harufu nzuri ya kumpendeza Bwana.
Mtatoa sadaka ya kuteketezwa ili kutoa harufu nzuri kwa BWANA. Mtatoa fahari wawili wachanga, kondoo mume mmoja, na wanakondoo saba waume wa mwaka mmoja.
28 Pamoja na kila fahali itatolewa sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi za efa uliochanganywa na mafuta; pamoja na kondoo dume, andaa sehemu mbili za kumi za efa za unga laini;
Pamoja na hiyo mtatoa sadaka ya unga: unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu tatu za kumi za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kwa kila fahari na sehemu kumi mbili za yule kondoo mume.
29 na sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kwa kila mmoja wa wana-kondoo saba.
Toeni sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kwa kila wale wanakondoo saba,
30 Ongeza beberu mmoja kwa kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
na beberu mmoja ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
31 Andaa hizi sadaka pamoja na sadaka zake za vinywaji, kuwa nyongeza ya sadaka za kawaida za kuteketezwa, pamoja na sadaka yake ya nafaka. Hakikisha kuwa wanyama hao hawana dosari.
Mtakapotoa hao wanyama wasio na dosari, pamoja na sadaka zake za vinywaji, hii itakuwa sadaka ya nyongeza katika zile sadaka za kila siku na pamoja na zile sadaka za unga.'”

< Hesabu 28 >