< Hesabu 23 >

1 Balaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, mnitayarishie mafahali saba na kondoo dume saba.”
Balaamu akamwabia Balaki, “Jenga madhabahu saba kwa ajili yangu na uandae mafahari saba na kondoo dume saba.”
2 Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema; hao wawili kila mmoja wao akatoa fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.
Kwa hiyo Balaki akafanya kama Balaamu alivyoomba. Kisha Balaki na Balaamu wakatoa sadaka ya fahari mmoja na kondoo dume mmoja kwa kila madhabahu.
3 Kisha Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati mimi ninakwenda kando. Huenda Bwana atakuja kukutana nami. Lolote atakalonifunulia, nitakuambia.” Basi akaenda hata mahali peupe palipoinuka.
Ndipo Balaamu alipomwamiba Balaki, “Simama kwenye sadaka yako ya kuteketezwa na mimi nitaenda. Labda BWANA atakuja kukutana na mimi. Chochote atakachoniambia nitakuambia.” Kwa hiyo akaenda juu ya mlima usiokuwa na miti.
4 Mungu akakutana naye, kisha Balaamu akasema, “Nimekwisha kutengeneza madhabahu saba, na juu ya kila madhabahu nimetoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja.”
Wakati bado akiwa juu ya mlima. Mungu akakutana naye, na Balaamu akamwambia, “Nimejenga madhabahu saba, na nimetoa sadaka ya fahari na kondoo dume kwa kila madhabahu.”
5 Bwana akaweka ujumbe katika kinywa cha Balaamu na kusema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”
BWANA akaweka ujumbe kwenye kinywa cha Baalamu akasema, “Rudi kwa Balaki ukamwambie.”
6 Basi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake akiwa na wakuu wote wa Moabu.
Kwa hiyo Balaamu akarudi kwa Balaki aliyekuwa amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, na viongozi wote wa Moabu walikuwa pamoja naye.
7 Ndipo Balaamu akasema ujumbe wake: “Balaki amenileta kutoka Aramu, mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki. Akasema, ‘Njoo, unilaanie Yakobo; njoo unishutumie Israeli.’
Ndipo Balaamu alipoanza kunena unabii wake akisema, “Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka katika milima ya mashariki, 'Njoo, nilaanie Yakobo kwa ajili yangu,' alisema, 'Njoo umtie unajisi Israeli,'
8 Nitawezaje kuwalaani, hao ambao Mungu hajawalaani? Nitawezaje kuwashutumu hao ambao Bwana hakuwashutumu?
Nawezaje kuwalaani wale ambao Mungu hajawalaani? Nawezaje kuwapinga wale ambao Mungu hawapingi?
9 Kutoka vilele vya miamba ninawaona, kutoka mahali palipoinuka ninawatazama. Ninaliona taifa ambalo wanaishi peke yao, nao hawahesabiwi kama mojawapo ya mataifa.
Kwa kuwa kutoka juu ya miamba Ninamwona; kutoka kwenye milima ninamtazama. Kuna watu wanaoishi pekee yao na hawajioni wenyewe kama ni taifa la kawaida.
10 Ni nani awezaye kuhesabu mavumbi ya Yakobo, au kuhesabu robo ya Israeli? Mimi na nife kifo cha mtu mwenye haki, na mwisho wangu na uwe kama wao!”
Nani awezaye kuyahesabu mavumbi ya Yakobo au kuhesabu hata robo ya Israeli? Naomba nife kifo cha mtu mwenye haki, na mwisho wa maisha yangu uwe kama wake!”
11 Balaki akamwambia Balaamu, “Ni nini ulichonitendea? Nimekuleta ulaani adui zangu, lakini wewe badala yake umewabariki!”
Balaki akamwambia Balaamu, “Umenifanyia nini? Nilikuleta ili uwalaani maadui wangu, lakini ona, umewabariki,”
12 Balaamu akajibu, “Je, hainipasi kusema kile Bwana anachoweka katika kinywa changu?”
Balaamu akajibu akasema, “Kwa nini nisiwe mwangalifu kusema kile ambacho BWANA anaweka kinywani mwangu?”
13 Ndipo Balaki akamwambia, “Twende pamoja mahali pengine ambapo unaweza kuwaona; utawaona baadhi tu wala si wote. Nawe kutoka huko, unilaanie hao.”
Basi Balaki akamwambia, “Hebu uje nami kwenye eneo jingine ili uwaone. Utakaowaona ni wale wa karibu tu, huwezi kuwaona wote. Huko sasa unaweza kunilaania hawa watu.”
14 Basi akampeleka kwenye shamba la Sofimu, juu ya kilele cha Mlima Pisga. Pale akajenga madhabahu saba na kutoa sadaka ya fahali na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.
Kwa hiyo akampeleka Balaamu kwenye shamba la Zofimu, lililo juu ya Mlima Pisiga, na kule akajenga madhabau zingine saba. Akatoa sadaka ya fahari mmoja na kondoo dume kwa kila madhabahu.
15 Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati ninapokwenda kuonana na Mungu kule.”
Kisha Balaamu akamwambia Balaki, “Simama hapa karibu na sadaka zako, wakati mimi naenda kukutana na BWANA kule.”
16 Bwana akakutana na Balaamu, akaweka ujumbe katika kinywa chake akasema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”
Kwa hiyo BWANA akakutana na Balaamu na kumwekea ujumbe kinywani mwake. Alimwambia, “Rudi kwa Balaki ukamwambie huu ujumbe toka kwangu.”
17 Basi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake, akiwa na wakuu wa Moabu. Balaki akamuuliza, “Je, Bwana amesema nini?”
Balaamu akamrudia, na tazama, alikuwa amesimama karibu na sadaka zake za kuteketezwa, na vionigozi wa Moabu walikuwa pamoja naye. Balaki akamwuliza, “BWANA amekwambiaje?”
18 Ndipo Balaamu akasema ujumbe wake: “Balaki, inuka na usikilize, nisikie mimi, wewe mwana wa Sipori.
Balaamu akaanza kutoa unabii. Akasema, “Inuka, Balaki na usikilize. Nisikilize mimi wewe mwana wa Zippori.
19 Mungu si mtu, hata aseme uongo, wala yeye si mwanadamu, hata ajute. Je, anasema, kisha asitende? Je, anaahidi, asitimize?
Mungu siyo mtu, kwamba umdanganye, au mwanadamu awezaye kubadili mawazo. Je, alishawahi kuahidi kitu pasipo kukitekeleza? Je, alishawahi kusema kuwa atafanya kitu bila kufanya kama alivyosema?
20 Nimepokea agizo kubariki; amebariki, nami siwezi kubadilisha.
Tazama, Mimi nimeamriwa kuwabariki. Mungu ametoa baraka, nami siwezi kuibadilisha.
21 “Haijaonekana bahati mbaya katika Yakobo, wala taabu katika Israeli. Bwana, Mungu wao yu pamoja nao, nayo sauti kuu ya Mfalme imo katikati yao.
Hajawahi kuona magumu katika Yakobo au tabu katika Israeli. BWANA Mungu wao yuko pamoja nao, na kelele za wafalme wao ziko pamoja nao.
22 Mungu aliwatoa kutoka Misri; wao wana nguvu za nyati.
Mungu aliwatoa Misri kwa nguvu kama za nyati.
23 Hakuna uchawi dhidi ya Yakobo, wala hakuna uaguzi dhidi ya Israeli. Sasa itasemwa kuhusu Yakobo na Israeli, ‘Tazama yale Mungu aliyotenda!’
Hakuna uganga utakaofanikiwa dhidi ya Yakobo, na hakuna uchawi utakaomwumiza Israeli. Badala yake, itasemwa juu ya Yakobo na Israeli, 'Tazama kile ambacho Mungu amefanya!'
24 Taifa lainuka kama simba jike; linajiinua kama simba ambaye hatulii mpaka amalize kurarua mawindo yake na kunywa damu ya mawindo yake.”
Tazama, watu wanainuka kama simba jike, kama vile simba ainukavyo na kuvamia. Halali chini mpaka ale windo lake na kunywa damu ya windo lake,”
25 Kisha Balaki akamwambia Balaamu, “Usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa!”
Kisha Balaki akamwambia Balaamu, “Kamwe usiwalaani wala kuwabariki.”
26 Balaamu akajibu, “Je, sikukuambia ni lazima nifanye lolote analosema Bwana?”
Lakini Balaamu akamjibu Balaki, “Sijakuambia kuwa nitasema yote ambayo BWANA ananiambia kusema?
27 Basi Balaki akamwambia Balaamu, “Njoo, nikupeleke mahali pengine. Huenda itampendeza Mungu kukuruhusu unilaanie hao watu kutoka mahali hapo.”
Balaki akamwambia Balaamu, “Njoo sasa, Nami nitakupeleka mahali pengine. Labda kule itampendeza Mungu kunilaania hawa hawa watu.”
28 Balaki akamchukua Balaamu juu ya Mlima Peori, unaotazamana na nyika.
Kwa hiyo Balaki akampeleka Balaamu juu ya Mlima Peori, ambao unalitazama chini lile jangwa,
29 Balaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, uandae mafahali saba na kondoo dume saba kwa ajili yangu.”
Balaamu akamwambia Balaki, “Nijengee madhabahu saba hapa na uniandalie mafahari saba na kondoo duume saba.
30 Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema, kisha akatoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.
“Kwa hiyo Balaki akafanya kama alivyoambiwa; akatoa sadaka ya fahari na kondoo mume kwenye kila madhabahu.

< Hesabu 23 >