< Hesabu 22 >
1 Kisha Waisraeli wakasafiri katika tambarare za Moabu na kupiga kambi kando ya Mto Yordani, ngʼambo ya Yeriko.
Watu wa Israeli wakasafiri mpaka wakaweka kambi kwenye uwanda wa Moabu karibu na Yeriko, kwenye upande mwingine wa mto Yorodani kutoka mji ule.
2 Basi Balaki mwana wa Sipori, aliona mambo yale yote ambayo Israeli aliwatendea Waamori,
Balaki mwana wa Zippori aliona yote ambayo Israeli aliwafanyia Waamori. Moabu aliogopa sana hao watu kwa sababu walikuwa wengi sana,
3 Moabu aliogopa, kwa kuwa walikuwepo watu wengi sana. Hakika, Moabu alijawa na hofu kubwa kwa sababu ya Waisraeli.
na Moabu alIwahofia wana wa Israeli.
4 Wamoabu wakawaambia wazee wa Midiani, “Umati huu wa watu unakwenda kuramba kila kitu kinachotuzunguka, kama maksai arambavyo majani ya shambani.” Kwa hiyo Balaki mwana wa Sipori, ambaye alikuwa mfalme wa Moabu wakati huo,
Mfalme wa Moabu akawaambia wazee wa Midiani, “Huu umati utakula kila kitu tulicho nacho na maksai hula nyasi za kondeni.” Sasa Balaki mwana wa Zippori alikuwa mfalme wa Moabu.
5 akatuma wajumbe kwenda kumwita Balaamu mwana wa Beori, ambaye alikuwa huko Pethori, karibu na Mto Frati, katika nchi yake ya kuzaliwa. Balaki akasema: “Taifa limekuja kutoka Misri, nao wamefunika uso wa nchi, nao wametua karibu nami.
Akatuma wajumbe kwenda kwa Balamu mwana wa Beori, kule Petho ambayo iko karibu na mto Frati, katika nchi ya taifa lake na watu wake. Akamwita na kumwambia, “Tazama, Kuna taifa ambalo wamekuja hapa tokea Misiri. Wanafunika uso wa dunia na sasa wananifuatia mimi.
6 Sasa uje kuwalaani watu hawa, kwa kuwa wana nguvu sana kuniliko. Kisha huenda nikaweza kuwashinda na kuwatoa nje ya nchi. Kwa kuwa ninajua kwamba, wale unaowabariki wanabarikiwa na wale unaowalaani wanalaaniwa.”
Tafadhali naomba uje unilaanie hili taifa, kwa sababu wana nguvu kuliko mimi. Labda nitaweza kuwavamia na kuwafukuza watoke katika nchi yangu. Najua kuwa yeyote unayembariki hubarikiwa na yeyote unayemlaani atalaaniwa.”
7 Wazee wa Moabu na wa Midiani wakaondoka, wakiwa wamechukua ada ya uaguzi. Walipokwenda kwa Balaamu, wakamweleza kile Balaki alikuwa amesema.
Kwa hiyo wazee wa Moabu na wale wa Midiani wakaondoka, pamoja nao wakachukua malipo ya uganga. Wakafika kwa Balaamu wakamwambia maneno ya Balaki.
8 Balaamu akawaambia, “Mlale hapa usiku huu, nami nitawaletea jibu lile Bwana atakalonipa.” Kwa hiyo wakuu wa Moabu wakakaa naye.
Balaamu akawaambia, “Bakini hapa usiku wa leo. Kesho nitawaletea atakachoniambia BWANA.” Kwa hiyo wale viongozi wa Moabu wakabaki na Balaamu kwa usiku huo.
9 Mungu akamjia Balaamu na kumuuliza, “Watu gani hawa walio pamoja nawe?”
Mungu akaja kwa Balaamu na kumwambia, “Ni akina nani hawa waliokuja kwako?”
10 Balaamu akamwambia Mungu, “Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alinipelekea ujumbe huu:
Balaamu akamjibu Mungu, “Balaki mwana wa Zippori, Mfalme wa Moabu amewatuma kwangu. Alisema,
11 ‘Taifa ambalo limekuja kutoka Misri limefunika uso wa nchi. Sasa uje unilaanie hao watu. Kisha huenda nitaweza kupigana nao na kuwafukuza.’”
'Tazama hawa watu waliotoka Misri wanafunika uso wa nchi yangu. Sasa naomba uje unilaanie hawa watu. Labada nitaweza kuwa kuwashinda na kuwafukuza.'”
12 Lakini Bwana akamwambia Balaamu, “Usiende pamoja nao. Hupaswi kulaani watu hao, kwa kuwa wamebarikiwa.”
Mungu akamjiu Balaam, “Usiambatane na hao wanaume. Na usiwalaani hawa wana wa Israeli kwa sababu wamebarikiwa.”
13 Asubuhi iliyofuata Balaamu akaamka, akawaambia wakuu wa Balaki, “Rudini katika nchi yenu, kwa kuwa Bwana amenikataza nisiende pamoja nanyi.”
Balaamu akaamka asubuhi na kuwaambia wale viongozi wa Balaki, “Rudini nchini kwenu kwa sababu BWANA amenikataza kuambatana nanyi.”
14 Kwa hiyo wakuu wa Moabu wakarudi kwa Balaki na kumwambia, “Balaamu amekataa kuja pamoja nasi.”
Kwa hiyo wale viongozi wa Moabu wakaondoka na kurudi kwa Balaki. Wakamwambia, “Balaamu amekataa kuambatana nasi.”
15 Kisha Balaki akatuma wakuu wengine, wengi zaidi na wanaoheshimiwa zaidi kuliko wale wa kwanza.
Balaki akatuma viongozi wengine waliokuwa wanaheshimiwa zaidi kuliko kundi lile la awali.
16 Wakafika kwa Balaamu na kumwambia: “Balaki mwana wa Sipori amesema hivi: Usiruhusu kitu chochote kikuzuie kuja kwangu,
Wakaja kwa Balaamu na kumwambia, “Balaki mwana wa Zippori anasema hivi, 'Tafadhali hebu kitu chochote kisikuzuie kuja kwangu,
17 kwa sababu nitakulipa vizuri sana na kufanya lolote usemalo. Njoo unilaanie watu hawa.”
kwa sababu nitakulipa malipo mazuri sana na kukupa heshima kubwa, nami nitakufanyia chochote utakachoniambia. Tafadhali sana uje unilaanie hawa watu.'”
18 Lakini Balaamu akawajibu, “Hata kama Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, singeweza kufanya kitu chochote kikubwa au kidogo ili kutenda kitu nje ya agizo la Bwana Mungu wangu.
Balaamu akawajibu watu wa Balaki akawaambia, “Hata kama Balaki atanipa ikulu yake ikiwa imejaa fedha na dhahabu, sitaweza kufanya dhidi ya maneno ya BWANA, Mungu wangu na kufanya pungufu au zaidi ya kile anachoniambia.
19 Mlale hapa usiku huu kama wale wengine walivyofanya, nami nitatafuta ni nini kingine Bwana atakachoniambia.”
Sasa basi, tafadhali subirini hapa usiku wa leo pia, ili kwamba nipate kujifunza kitu zaidi ambacho BWANA ananiambia.”
20 Usiku ule Bwana akamjia Balaamu na kumwambia, “Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita wewe, nenda nao, lakini ufanye tu lile nitakalokuambia.”
BWANA akaja kwa Balaamu usiku ule na kumwambia, “kwa kuwa hawa watu wamekuja kukuita, inuka uende nao. Lakini utafanya tu kile nitakachokuambia kufanya.”
21 Balaamu akaamka asubuhi, akatandika punda wake akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.
Balaamu akainuka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na viongozi wa Moabu.
22 Lakini Mungu alikasirika sana alipokwenda, naye malaika wa Bwana akasimama barabarani kumpinga. Balaamu alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye.
Lakini kwa sababu alienda, hasira za Mungu zikawaka. Malaika wa BWANA akasimama barabarani kama adui wa Balaamu, aliyekuwa akimpanda yule punda. Watumishi wawili wa Balaamu walikuwa pamoja naye.
23 Wakati punda alipomwona malaika wa Bwana akiwa amesimama barabarani akiwa na upanga uliofutwa mkononi mwake, punda akageukia upande kuelekea shambani. Balaamu akampiga ili amrudishe barabarani.
Yule punda alimwona yule malaika wa BWANA akiwa amesimama barabarani akiwa na upanga mkononi mwake. Yule punda akageuka na kwenda shambani. Balaamu akampiga yule punda ili arudi barabarani.
24 Ndipo malaika wa Bwana akasimama katika njia nyembamba iliyo kati ya mashamba mawili ya mizabibu, yakiwa na kuta pande zote mbili.
Sasa malaika wa BWANA akasimama kwenye njia nyembamba katikati ya mashamba ya mizabibu, na kushoto kwake kulikuwa na ukuta.
25 Punda alipomwona malaika wa Bwana, alijisukumiza karibu na ukuta, na kugandamiza mguu wa Balaamu ukutani. Ndipo Balaamu akampiga tena punda.
Yule punda akamwona yule malaika wa BWANA tena. Akasogea zaidi ukutani na kuubana mguu wa Balaamu ukutani. Balaamu akampiga tena yule punda.
26 Kisha malaika wa Bwana akaendelea mbele na kusimama mahali pembamba ambapo hapakuwepo nafasi ya kugeuka, upande wa kulia wala wa kushoto.
Yule malaika wa BWANA akasogea mbele zaidi kwenye eneo jingine jembamba zaidi ambalo haikuwezekana kugeuka upande mwingine.
27 Punda alipomwona malaika wa Bwana, alilala chini Balaamu angali amempanda, naye Balaamu akakasirika na kumpiga kwa fimbo yake.
Yule Punda akamwona tena yule malaika wa BWANA, akalala chini ya Balaamu. Hasira za Balaamu zikawaka, akampiga yule punda kwa fimbo yake.
28 Kisha Bwana akakifungua kinywa cha punda, akamwambia Balaamu, “Nimekutendea nini kinachokufanya unipige mara hizi tatu?”
Kisha BWANA akafungua kinywa cha punda na akaongea. Akamwambia Balaamu, “Nimekukosea nini kiasi kwamba umenipiga mara tatu?”
29 Balaamu akamjibu punda, “Umenifanya mjinga! Kama ningelikuwa na upanga mkononi mwangu, ningelikuua sasa hivi.”
Balaamu akamjibu yule punda, “Ni kwa sababu umenitendea kwa ujinga. Natamani kama ningekuwa na upanga mkononi mwangu, kama ningekuwa nao, sasa hivi ningekuwa nimekuua.”
30 Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si punda wako mwenyewe, ambaye umenipanda siku zote, hadi leo? Je, nimekuwa na tabia ya kufanya hivi kwako?” Akajibu, “Hapana.”
Yule punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si punda wako ambaye umenipanda maishani mwako mwote mpaka hivi sasa? Je, nimewahi kuwa na tabia ya kukufanyia hivi hapo awali?” Balaamu akasema “hapana.”
31 Kisha Bwana akafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika wa Bwana amesimama barabarani akiwa ameufuta upanga wake. Balaamu akainama, akaanguka kifudifudi.
Basi BWANA akafungua macho ya Balaamu, na akamwona malaika wa BWANA amesimama barabarani akiwa na upanga mkononi mwake. Balaamu akainamisha kichwa chake chini.
32 Malaika wa Bwana akamuuliza Balaamu, “Kwa nini umempiga punda wako mara tatu hizi? Nimekuja kukuzuia kwa sababu njia yako imepotoka mbele yangu.
Yule malaika wa BWANA akamwambia, “Kwa nini umempiga punda wako mara tatu? Tazama, Nimekuja kama adui yako kwa sababu matendo yako kwangu yamekuwa maovu.
33 Punda aliniona na kunikwepa mara hizi tatu. Kama punda hangenikwepa, hakika ningekuwa nimeshakuua sasa, lakini ningemwacha punda hai.”
Yule punda aliniona na akageuka kutoka kwangu mara tatu. Kama asingekuwa amegeuka kutoka kwangu, hakika ningekuwa nimekua na yeye kumwacha hai.
34 Balaamu akamwambia malaika wa Bwana, “Nimetenda dhambi. Sikutambua kuwa umesimama barabarani kunizuia. Basi kama haikupendezi, nitarudi.”
Balaamu akamwambia malaika wa BWANA, nimetenda dhambi. Sikujua kuwa ulisimama kinyume na mimi barabarani. Kwa hiyo sasa, kama haikupendezi, Nitageuka.”
35 Malaika wa Bwana akamwambia Balaamu, “Uende na watu hao, lakini useme tu lile nikuambialo.” Kwa hiyo Balaamu akaenda na wale wakuu wa Balaki.
Lakini yule malaika wa BWANA akamwambia Balaamu, “endelea na wale watu. Lakini utasema maneno nitakayokwambia tu.”Kwa hiyo Balaamu akaendelea na wale vioingozi wa Balaki.
36 Balaki aliposikia kuwa Balaamu anakuja, akatoka kumlaki katika mji wa Moabu, katika mpaka wa Arnoni, ukingoni mwa nchi yake.
Balaki aliposikia kuwa Balaamu alikuwa amekuja, alienda kukutana naye kule mjini Moabu pale Amoni, ambao uko mpakani.
37 Balaki akamwambia Balaamu, “Je, sikukupelekea jumbe za haraka? Kwa nini hukuja kwangu? Hivi kweli mimi siwezi kukulipa?”
Balaki akamwambia Balaamu, “Je, mimi sikutuma watu kukuita? Basi kwa nini hukuja kwangu? Je, mimi sina uwezo wa kukufanya uheshimike?”
38 Balaamu akajibu, “Vema, sasa nimekuja kwako. Lakini kwani nina uwezo wa kusema tu chochote? Ni lazima niseme tu kile ambacho Mungu ataweka kinywani mwangu.”
Ndipo Balaamu alipomjibu Balaki, “Tazama, mimi nimekuja kwako. Je mimi sina mamlaka ya kusema chochote? Mimi ninaweza kusema maneno ambayo Mungu ameweka kinywani mwangu.”
39 Kisha Balaamu alikwenda na Balaki mpaka Kiriath-Husothi.
Balaamu akaenda na Balaki, na Wakafika Kiriathi Huzothi.
40 Balaki akatoa dhabihu ya ngʼombe na kondoo; baadhi yake akampa Balaamu na wakuu waliokuwa pamoja naye.
Kisha Balaki akatoa sadaka ya maksai na kondoo na kumpatia Balaamu baadhi ya hiyo nyama na wale viongozi waliokuwa pamoja naye.
41 Asubuhi iliyofuata Balaki akamchukua Balaamu mpaka Bamoth-Baali, na kutoka huko Balaamu akawaona baadhi ya watu.
Kesho yake asubuhi, Balaki akampeleka Balaamu mpaka juu mahali pa Baali. Kule juu Balaamu aliweza kuona sehemu tu ya kambi za Waisraeli.